Mganga wa kienyeji, Zacharia Ngobeko (35),
amekamatwa na polisi mkoani hapa baada ya kukutwa akimiliki SMG na
risasi nane kinyume cha sheria.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha, alisema
tukio hilo lilitokea juzi saa 1 jioni, baada askari polisi kufanya msako
nyumbani kwake na kukamata silaha hiyo ikiwa na risasi zilizokuwamo
kwenye magazine.
Kamugisha alisema baada ya kumhoji, alidai silaha hiyo ilitumika
kufanya mauaji mbalimbali yakiwamo ya kumuua, Mary Kashidye, Februari 8,
mwaka huu, kwa kumpiga risasi kutokana na ugomvi wa kiwanja kati yake
na Jumanne Maige.
Aidha, alisema mauaji hayo yalifanyika baada ya kukodiwa vijana
wawili, Andrew Buteye (38) na Daudi Luchemela (40), kutekeleza mauaji
hayo, kisha kurejesha silaha hiyo kwa mganga huyo.
Kamanda Kamugisha alisema silaha hiyo kupitia vijana hao ilitumika
katika tukio la unyang’anyi wilayani Kahama baada ya kumpora Manyangu
Mboje, Sh. Milioni 1.5, dukani kwake Februari 13, mwaka huu.
Hata hivyo, alisema baada ya kuwahoji watuhumiwa wote walikiri
kuhusika na matukio hayo ya mauaji na unyang’anyi kwa kutumia SMG hiyo
na kisha kuihifadhi kwa mganga huyo huku wakikiri kufanya matukio
mengine mkoani Mbeya mwaka 2010 na 2012.
Alisema watuhumiwa hao, pia walikiri kufanya uhalifu wilayani
Sengerema mkoa wa Mwanza 2014, kwa kupora Sh. milioni 39. Watuhumiwa
wote wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wiki ijayo kujibu mashitaka
yanayowakabili.
No comments:
Post a Comment