Na Mwandishi Maalum, New York
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon amemteua Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mhe. Mohamed Chande Othman kuongoza jopo huru la wataalam watakaopitia taarifa mpya kuhusu kifo cha Bw. Dag Hammarskjold ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.“ Katibu Mkuu anayofuraha ya kutangaza kwamba amewateua wafuatao kuwa wajumbe wa jopo huru la wataalamu. Bw. Mohamed Chande Othman kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye atakuwa mkuu wa jopo hilo. Wajumbe wengine ni Bw. Kerryn Macaulay kutoka Australia na Bw. Henrik Ejrup Larsen kutoka Denmark” inasomeka taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu
Uteuzi wa Jopo hilo unatokana na Azimio namba 69/246 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililopitishwa tarehe 29 mwezi Desemba 2014 ambalo lilimtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuteua jopo la wataalam huru ili kuchunguza na kutathimin thamani ya taarifa mpya ( probative value)zinazohusiana na kifo cha Katibu Mkuu Dag Hammarskjold pamoja na watu waliofuatana naye.
Bw. Dag Hammarskjold na ujumbe wake alipoteza maisha katika ajali ya ndege iliyotokea mwaka 1961 wakati akitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Baadhi ya Majukumu ya Jopo hilo huru la wataalamu pamoja na mambo mengine yatakuwa kupitia na kutathmini thamani ya taarifa mpya ambazo Kamisheni ya Hammarskjold imeziwasilisha kwa Katibu Mkuu Ban Ki Moon. Vile vile litatathmini taarifa mbalimbali ambazo zimetolewa na nchi wanachama na vyanzo vingine.
Jopo hilo la wataalam huru litaanza kazi yake mwisho mwa mwezi huu wa March ( 30 March) na linatarajiwa kuwasilisha taarifa yake kwa Katibu Mkuu si Zaidi ya tarehe 30 mwezi June mwaka huu
No comments:
Post a Comment