Kamanda wa polisi mkoani Tabora, ACP Suzan Kaganda akionyesha kwa waandishi wa habari ( hawapo pichani ) milipuko aina ya Superpower 90 ambayo ilikamatwa wiki hii wilayani Nzega ikiwa na uzito wa kilo 133
Kamanda wa polisi mkoani Tabora, ACP Suzan Kaganda akiwaonyesha waandishi wa habari ( hawapo pichani ) vipande vya meno ya tembo vilivyokamatwa na jeshi hilo.
Vipande vya meno ya tembo vilivyokamatwa wilayani Sikonge mkoani Tabora wiki hii.
Na FAKIH ABDUL MAPONDELA A/INSP Mkuu wa kitengo cha habari Polisi Tabora.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, ACP Suzan Kaganda ameongea na waandishi wa habari na kuelezea mafanikio mbalimbali ambayo yamepatikana katika Operesheni ya kupambana na uhalifu na wahalifu mkoani Tabora,
Katika wilaya ya Nzega, mnamo tarehe 13/04/2014 eneo la Stendi ya mabasi walikamatwa watu watatu wakiwa na milipuko aina ya Superpower yenye uzito wa kilogramu 133 ambayo walikuwa wanasafirisha katika gari aina ya Toyota saloon ambayo inafanya shughuli za taxi mjini Nzega.
Watuhumiwa wanahojiwa na jeshi la Polisi na mara baada ya upelelezi kukamilika watafikishwa mahakamani
Pia katika wilaya ya Sikonge watu watatu walikamatwa wakiwa na vipande vya meno ya Tembo kumi na saba (17) ambavyo sawa na meno 8 ya Tembo na hivyo kufanya idadi ya Tembo wanne waliouawa.
Watu hao walikamatwa wakiwa katika gari ndogo aina ya Toyota Noah miongoni mwao mmoja ni askari wa Jeshi la wananchi Tanzania anayefanyiakazi katika ofisi ya mshauri wa mgambo mkoa wa Tabora.
Watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Aidha huko katika wilaya ya Uyui kijiji cha kigwa walikamatwa watu watatu wakiwa na Bangi magunia matatu na mara baada ya kuhojiwa walikiri kwamba wao ni wauzaji na watumiaji wa bangi hiyo.
Watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani mapema ili kujibu tuhuma zinazowakabili.
No comments:
Post a Comment