Balozi wa Marekani Nchini, Mark Childress amekutana na Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene kwa ajili ya kujadili hatua iliyofikiwa ya utekelezaji wa mpango wa kuboresha sekta ndogo ya umeme na miradi ya Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC) Ofisi za Wizara ya Nishati na Madini leo.
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (kulia) akimpokea Balozi wa Marekani Nchini, Mark Childress (kushoto) mara baada ya kuwasili kwenye ofisi za Wizara ya Nishati na Madini.
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Waziri wa Nishati na Madini George Simbachawene amesema kuwa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) lina mpango wa kufunga mita za LUKU katika ofisi za taasisi zote za serikali kama moja ya mikakati yake katika ukusanyaji wa mapato.
Simbachawene aliyasema wakati wa kikao chake na Balozi wa Marekani Nchini, Mark Childress aliyemtembelea ofisini kwake lengo likiwa ni kujadili hatua iliyofikiwa ya utekelezaji wa mpango wa kuboresha sekta ndogo ya umeme na miradi ya Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC)
Alisema kuwa kama mkakati wa kuhakikisha kuwa shirika la Tanesco halijiendeshi kihasara, shirika hilo limeweka mkakati wa ukusanyaji wa mapato, moja ya mkakati ikiwa ni kufunga mita za Luku kwenye Taasisi za Serikali, Binafsi na wateja wa kawaida.
“Tunaamini shirika likitekeleza mkakati huo, litapunguza hasara na kuwa tegemezi kwenye serikali kupitia ruzuku.” Alisema Simbachawene.
Alisema pia Tanesco itaingia mkataba na Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) kwa ajili ya ukusanyaji wa madeni yake ya nyuma na kuendelea kulipia ankara zake za kila mwezi.
Akizungumzia hatua iliyofikiwa ya utekelezaji wa miradi ya MCC Awamu ya Pili , Simbachawene alisema kuwa kazi ya uandaaji wa miradi imekamilika na kuwasilishwa katika Bodi ya MCC nchini Marekani kwa ajili ya kupata idhini ya kufadhili miradi
Alitaja mikoa itakayofaidika na miradi ya MCC Awamu ya Pili kuwa ni pamoja na Pwani, Tabora, Shinyanga na Morogoro pamoja na kuboresha utendaji kazi wa Tanesco.
Wakati huohuo Balozi wa Marekani Nchini, Mark Childress alisema kuwa amefurahishwa na hatua ya utekelezaji wa miradi ya MCC Awamu ya Pili na kusisitiza kuwa Marekani ipo tayari kushirikiana na nchi ya Tanzania kupitia miradi ya umeme ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata umeme wa uhakika ambao una mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
No comments:
Post a Comment