Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, October 19, 2011

BILA UWEKEZAJI HAKUNA MAENDELEO – RAIS KIKWETE

 
RAIS Jakaya Kikwete amesema hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana nchini kama hakuna uwekezaji wowote utakaofanyika kwa sababu hakuna Taifa lolote linaloendelea bila kukaribisha uwekezaji wa nje.
“Hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana kama hakuna uwekezaji, penye maendeleo ni lazima kuwe na utoaji wa huduma za jamii... kama hukuwekeza hakuna utakachozalisha, na kama hukuwekeza hakuna huduma utakayotoa,” alisema na kusisitiza kuwa ajenda kubwa ya serikali ni kuvutia uwekezaji nchini.
Katika hotuba yake iliyodumu kwa saa moja na nusu wakati akifungua mkutano wa siku moja wa uwekezaji wa Kanda ya Uwekezaji ya Ziwa Tanganyika, Rais Kikwete alisema Serikali itaendelea na jukumu lake la kutengeneza mazingira ya kukuza uchumi ili sekta binafsi iweze kutekeleza majukumu yake.
Alisema mikoa ya Kanda ya Ziwa Tanganyika inayojumuisha Rukwa, Kigoma na mkoa tarajiwa wa Katavi imekuwa nyuma kimaendeleo kwa sababu ya uwekezaji mdogo uliokuwepo miaka ya nyuma.
Alibainisha kwamba hali sasa itabadilika kwa sababu Serikali imeamua kuwekeza katika miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege na bandari ili kuifungua mikoa hiyo. “Katika mkoa wa Rukwa peke yake, mbali ya uwekezaji katika maeneo mengine, Serikali imewekeza sh. bilioni 490/- kwa ajili ya ujenzi wa barabara, wakati katika mkoa wa Kigoma fedha zilizowekezwa kwenye barabara ni mara mbili ya hizo,” alisema.
Akizungumza na washiriki wa kongamano hilo ambao ni mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, wawekezaji, wafanyabiashara, wakuu wa taasisi za Serikali, wabunge na baadhi ya wakuu wa mikoa, Rais Kikwete alisema angependa kuona kanda ya Ziwa Tanganyika ikishamiri kimaendeleo. (I would like to see this sleeping giant - Lake Tanganyika Zone - awakening).
Aliwataka washiriki wa mkutano huo waangalie fursa za uwekezaji zilizopo katika madini, uvuvi, safari za majini, utalii, kilimo, viwanda, usafiri wa anga na barabara, ufugaji na hata kilimo cha miwa hasa katika maeneo ya Kigoma.
Alitumia fursa hiyo kuwathibitishia wakazi wa wilaya Mpanda ambao walikuwa wakifuatilia mkutano huo kwenye mahema nje ya ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda kwamba kabla ya mwisho wa mwezi huu, mkoa mpya wa Katavi utakuwa umetangazwa baada ya taratibu zote kukamilika. Wilaya ya Mpanda ni mojawapo ya wilaya zitakazounda mkoa mpya wa Katavi.
Kuhusu bandari, Rais Kikwete alisema bandari tano kati ya 19 zilizopo katika Ziwa Tanganyika tayari ziko katika mpango wa kufanyiwa ukarabati wakati meli ya siku nyingi ya MV Lihemba iko mbioni kukarabatiwa ili kutunza historia yake ya zaidi ya miaka 100.
“Bandari za Kigoma na Kasanga zitapanuliwa na kuboreshwa ili ziwe na hadhi ya kimataifa, bandari nyingine za Kirando, Karema na nyinginezo, zitakarabatiwa kadri tunavyoendelea,” aliongeza.
Kuhusu viwanda vya ndege vya Rukwa, alisema baada ya kukamilisha ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mpanda, Serikali itafanya ukabati mwingine katika kiwanja kidogo cha ndege cha Sumbawanga (airstrip).
Kuhusu ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma, Rais Kikwete alisema mkandarasi amekwishapatikana na ukarabati wake utaanza hivi karibuni. “Ninatamani kuona uwanja wa ndege wa Kigoma ukiwa ni kitovu cha mawasiliano ya ndege zote katika ukanda wa maziwa makuu...,” alisema.
Mkutano huo ambao kaulimbiu yake ilikuwa “Kuibua Fursa za Uwekezaji katika Kanda ya Ziwa Tanganyika” (Unleashing Potentials for Lake Tanganyika Zone) ulikuwa na lengo la kuinua fursa za uwekezaji katika Kanda ya Uwekezaji ya Ziwa Tanganyika ambayo inaihusisha mikoa ya Rukwa, Kigoma na mkoa mpya-tarajiwa wa Katavi ambayo yote kwa pamoja imejaliwa maliasili nyingi zikiwemo madini, vivutio vya utalii, ardhi nzuri ya kilimo na maeneo ya uvuvi.
Rais Kikwete ameondoka Mpanda leo kurejea jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment