Pages

Monday, November 19, 2012

Majeshi ya Israel Yaendelea Kushambulia Gaza, Makao Makuu Hamas Yapigwa



Mashambulizi yakiendelea
ISRAEL imeshambulia maeneo ya wapiganaji katika ukanda wa Gaza kwa siku ya tano (Novemba 18, 2012), wakishambulia kwa ndege na jeshi la majini wakati jeshi lake lingine likijitayarisha kufanya mashambulizi ya ardhini. Misri hata hivyo inaona ishara za uwezekano wa kupatikana usitishaji wa mapigano hapo katika siku za baadaye.
Wapalestina 47, karibu nusu yao wakiwa ni raia, ikiwa ni pamoja na watoto 12, wameuwawa katika mashambulio hayo ya Israel , maafisa wa Palestina wamesema. Karibu maroketi 500 yaliyofyatuliwa kutoka Gaza yamefika nchini Israel, na kuuwa watu watatu na kuwajeruhi wengine kadha.
Israel ilianzisha mashambulizi yake makubwa ya anga siku ya Jumatano, na kumuua kiongozi mkuu wa tawi la kijeshi la Hamas, kwa lengo la kuwazuwia wapiganaji katika eneo hilo la pwani kushambulia kwa maroketi jamii inayoishi katika eneo lake la kusini mwa nchi hiyo.
Taifa hilo la Kiyahudi limeshambulia hadi sasa kwa makombora 950 kwa kutumia ndege za kijeshi dhidi ya eneo hilo dogo la pwani la Wapalestina, wakilenga vifaa vya kijeshi pamoja na kubomoa nyumba za wapiganaji na makao makuu.
Mashambulio yaliendelea usiku wa manane Jumapili, huku ndege za kivita zikishambulia maeneo kutoka baharini. Shambulio la anga lililenga katika jengo mjini Gaza ambalo ni la ofisi za chombo cha habari cha Kiarabu na kuwajeruhi waandishi watatu wa televisheni ya al Quds, kituo cha televisheni ambacho Israel inakiona kuwa kinaunga mkono kundi la Hamas, wamesema watu walioshuhudia.
Mashambulio mengine ya alfajiri dhidi ya nyumba katika kambi ya wakimbizi ya Jebalya yamesababisha kifo cha mtoto mmoja na kuwajeruhi watu wengine 12, wamesema maafisa wa hospitali. Mashambulio haya yanafuatia taarifa za kikaidi zilizotolewa na msemaji wa kijeshi wa Hamas Abu Ubaida, ambaye amesema katika mkutano na waandishi habari kuwa, “duru hii ya mapambano haitakuwa ya mwisho dhidi ya maadui wa kizayuni na ndio kwanza inaanza.”
Shambulio la Israel siku ya Jumamosi limeharibu nyumba ya kamanda wa Hamas karibu na mpaka na Misri.
Israel hata hivyo ikiwa na vifaru na vifaa vingine vya kijeshi imeweka majeshi yake katika mpaka, ikiashiria kuwa bado inafikiria uwezekano wa mashambulio ya ardhini ndani ya Gaza. Baraza la mawaziri la Israel limeamua siku ya Ijumaa, (16.11.2012) kuongeza mara dufu idadi ya wanajeshi wa akiba katika operesheni ya Gaza kufikia 75,000 na wanajeshi wa akiba wanaofikia 16,000 tayari wamekwishaitwa.
Israel imesema kuwa shule katika eneo lake la kusini zitafugwa leo Jumapili(19.11.2012) kuepuka madhara zaidi kutokana na mashambulio ya maroketi ambayo yamefika hadi katika mji mkuu Tel Aviv katika siku chache zilizopita.
Ndege za Israel zilishambulia Makao Makuu ya Hamas huko Gaza ikiwemo ofisi ya waziri mkuu baada ya baraza la mawaziri la Israel kuidhinisha kuandaliwa kwa wanajeshi wa akiba 75,000 kwa uwezekano wa kuvamia Gaza.
Ndege hizo za Israel zimeshambulia wizara ya ulinzi na jengo la ofisi ya Waziri Mkuu Ismail Haniyeh ambapo hapo Ijumaa alikutana na Waziri Mkuu wa Misri. Kwa siku kadhaa miripuko mizito imekuwa ikilitingisha eneo la Gaza linalokaliwa na idadi kubwa ya watu na kusababisha kufuka kwa moshi mzito angani.

No comments:

Post a Comment