YANGA wamemsainisha Mrisho Ngassa wakachoonga, lakini Simba
ilichofanya imetua Uganda, ikasajili bonge la beki wa kati ambaye kazi
yake itakuwa moja tu kutuliza ukuta wa Msimbazi na kuzima nyodo za
Ngassa.
Beki huyo Samuel Ssenkoomi anaichezea URA ya
Kampala na Uganda Cranes ambapo
mhariri wa michezo wa Gazeti maarufu la
Newvision la Uganda, Fred Kaweesi aliiambia Mwanaspoti jana Jumatatu
kwamba: "Simba imepata bonge la beki, Samuel anajua sana halafu hana
papara."
Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti ilizipata jana
Jumatatu na kuthibitishwa na Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph
Itang'are 'Mzee Kinesi' ni kwamba Simba imemsainisha beki huyo kwa
mkataba wa miaka miwili.
Mzee Kinesi alisema mchezaji huyo amemalizana na
Simba na atatua jijini Dar es Salaam wakati wowote tayari kujiunga na
kikosi kitakachoanza mazoezi kesho Jumatano kwenye Uwanja wa Kinesi,
jijini Dar es Salaam chini ya kocha mpya, Abdallah Kibadeni.
Simba ina imani kwamba kwa rekodi yake beki huyo
ataweza kuzuia papara za mastraika wa Yanga, Ngassa, Didier Kavumbagu na
wengine ambao Yanga inaringa nao.
Kinesi alisema: "Kocha Patrick Liewig
tumeshamalizana naye na hatutaki hata kumsikia, alikuwa ana mambo fulani
ya kubagua watu kitu ambacho si kizuri kwa kiongozi. Kibadeni
tumemchukua kwavile ametupa ubingwa mara tatu anaijua Simba na
atatujengea timu nzuri."
"Alishafanya hivyo kwenye timu ya vijana na mpaka
sasa inafanya vizuri,"alisisitiza kiongozi huyo na kusema timu itaanza
mazoezi kesho Jumatano kujiandaa na michuano ya Kombe la Kagame mwezi
ujao nchini Sudan. Simba imepangwa kuanza na El Merreikh Juni 21.
Simba tayari imeshawasajili beki Issa Rashid wa
Mtibwa, kipa Andrew Ntala wa Kagera, viungo Zahoro Pazi wa JKT Ruvu na
Twaha Ibrahim wa Coastal. Wengine walioongezewa mkataba ni Haruna
Chanongo, Ramadhani Singano na Abdallah Seseme.
Simba imepanga kuachana na kiungo wa Uganda, Mussa
Mude kutokana na kutoridhishwa na kiwango chake. Hiyo ina maanisha
kwamba kwa sasa Simba itakuwa na wachezaji wawili tu wa kigeni ambao ni
Samuel na Abel Dhaira wote wa Uganda.
Felix Sunzu wa Zambia pamoja na Komanbilli Keita wa Mali wametemwa kama atakavyofanyiwa Mude.
source-mwanaspoti
source-mwanaspoti
No comments:
Post a Comment