KIUNGO wa Yanga, Haruna Niyonzima, ameshinda Tuzo ya Mwanasoka Bora 2012/13.
Tuzo ya Mwanaspoti Bora wa Soka Tanzania 2012/13
iliandaliwa na gazeti bora la michezo Afrika Mashariki, Mwanaspoti kwa
udhamini wa Vodacom na Clouds Media Group.
Niyonzima alishinda tuzo hiyo katika hafla maalumu
iliyofanyika jana Ijumaa usiku katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar
es Salaam na kuhudhuriwa na mgeni rasmi Naibu Waziri wa Sayansi,
Mawasiliano na Teknolojia, Januari Makamba.
Niyonzima aliwashinda wachezaji wengine wanne
waliokuwa wameingia katika fainali ambao ni Shomari Kapombe (Simba),
Amri Kiemba (Simba), Kelvin Yondani (Yanga) na Themi Felix wa Kagera
Sugar.
Katika mchujo wa mwisho walioingia tatu bora
walikuwa Niyonzima, Kapombe na Kiemba. Licha ya kupewa Sh5 milioni, pia
Niyonzima alikabidhiwa tuzo maalumu.
Tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi ilikwenda kwa
Joseph Kimwaga wa Azam aliyewashinda Juma Luzio wa Mtibwa Sugar na
Ramadhani Singano wa Simba. Kimwaga alipata Sh500,000 na tuzo maalumu.
Tuzo ya Mchezaji Bora wa Kike ilikwenda kwa Mwanahamisi Omari ambaye aliwapiku Fatuma Mustafa na Shelda Boniface.
Mwanahamisi alipata Sh500,000 na tuzo maalumu.
Niyonzima alipata tuzo nyingine ya Mchezaji Bora
wa Kigeni na kuwashinda Kipre Tchetche wa Azam na Hamis Kiiza wa Yanga.
Ushindi huu ulimpa Niyonzima tuzo maalumu.
Mbwana Samatta wa TP Mazembe ya Congo alishinda
Tuzo ya Mchezaji Bora Anayecheza Nje na kuwapiku Thomas Ulimwengu (TP
Mazembe) na Henry Joseph aliyekuwa anachezea Kongsvinger ya Norway.
Samatta pia alipewa tuzo maalumu.
Katika kipengele cha Kocha Bora, Abdalla Kibadeni
alishinda kipengele hicho kwa tiketi ya Kagera Sugar na kuwapiku Ernest
Brandts wa Yanga na Stewart Hall wa Azam. Kibadeni ambaye sasa
anafundisha Simba alipewa Sh500,000 na tuzo maalumu.
Mwamuzi mwenye beji ya Fifa, Oden Mbaga wa Dar es
Salaam alichaguliwa kuwa Mwamuzi Bora na kuwapiku Martin Saanya na
Ibrahim Kidiwa. Mbaga alipewa Sh500,000 na tuzo maalumu.chanzo mwanaspoti
No comments:
Post a Comment