Pages

Saturday, November 9, 2013

Niyonzima mchezaji bora Tanzania 2012/13




Kiungo wa Yanga Haruna Niyonzima akipokea hundi ya Sh. Milioni 5 kutoka kwa Naibu Waziri wa Sayansi Mawasiliano na Teknolojia, Januari Makamba. Wengine kulia ni Mwenyekiti wa Bodi wa MCL Zuhura Muro na Mkurugenzi Mtendaji wa MCL Tido Mhando kushoto. Picha na Mpiga Picha Wetu 

KIUNGO wa Yanga, Haruna Niyonzima, ameshinda Tuzo ya Mwanasoka Bora 2012/13.
Tuzo ya Mwanaspoti Bora wa Soka Tanzania 2012/13 iliandaliwa na gazeti bora la michezo Afrika Mashariki, Mwanaspoti kwa udhamini wa Vodacom na Clouds Media Group.
Niyonzima alishinda tuzo hiyo katika hafla maalumu iliyofanyika jana Ijumaa usiku katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mgeni rasmi Naibu Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia, Januari Makamba.
Niyonzima aliwashinda wachezaji wengine wanne waliokuwa wameingia katika fainali ambao ni Shomari Kapombe (Simba), Amri Kiemba (Simba), Kelvin Yondani (Yanga) na Themi Felix wa Kagera Sugar.
Katika mchujo wa mwisho walioingia tatu bora walikuwa Niyonzima, Kapombe na Kiemba. Licha ya kupewa Sh5 milioni, pia Niyonzima alikabidhiwa tuzo maalumu.
Tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi ilikwenda kwa Joseph Kimwaga wa Azam aliyewashinda Juma Luzio wa Mtibwa Sugar na Ramadhani Singano wa Simba. Kimwaga alipata Sh500,000 na tuzo maalumu.
Tuzo ya Mchezaji Bora wa Kike ilikwenda kwa Mwanahamisi Omari ambaye aliwapiku Fatuma Mustafa na Shelda Boniface.
Mwanahamisi alipata Sh500,000 na tuzo maalumu.
Niyonzima alipata tuzo nyingine ya Mchezaji Bora wa Kigeni na kuwashinda Kipre Tchetche wa Azam na Hamis Kiiza wa Yanga. Ushindi huu ulimpa Niyonzima tuzo maalumu.
Mbwana Samatta wa TP Mazembe ya Congo alishinda Tuzo ya Mchezaji Bora Anayecheza Nje na kuwapiku Thomas Ulimwengu (TP Mazembe) na Henry Joseph aliyekuwa anachezea Kongsvinger ya Norway. Samatta pia alipewa tuzo maalumu.
Katika kipengele cha Kocha Bora, Abdalla Kibadeni alishinda kipengele hicho kwa tiketi ya Kagera Sugar na kuwapiku Ernest Brandts wa Yanga na Stewart Hall wa Azam. Kibadeni ambaye sasa anafundisha Simba alipewa Sh500,000 na tuzo maalumu.
Mwamuzi mwenye beji ya Fifa, Oden Mbaga wa Dar es Salaam alichaguliwa kuwa Mwamuzi Bora na kuwapiku Martin Saanya na Ibrahim Kidiwa. Mbaga alipewa Sh500,000 na tuzo maalumu.chanzo mwanaspoti

No comments:

Post a Comment