Kikosi cha Taifa stars.
Na Mwandishi wetu
SIRI za kushindwa kwa timu ya soka ya taifa kufuzu katika
michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON).
Siri hiyo ya kukwama kwa timu ya taifa kwenye michuano ya
(AFCON), inadaiwa kutokana na hujuma
zilizofanywa na kundi la watu wachache kwa lengo la kumwonesha Rais wa TFF,
Jamal Malinzi hawezi kuongoza shirikisho hilo na kuipa mafanikio Stars.
Wahujumu hao wa soka nchini, wanadaiwa kutoka katika vilabu
vikubwa vya soka nchini ambao kwa sasa majina yao yamehifadhiwa.
Uchunguzi uliofanywa tangu timu ya soka ya taifa ilipotolewa
kwenye michuano hiyo na timu ya soka ya Msumbiji, unaonyesha kuwa hilo limeapa
kufanya hujuma dhidi ya timu ya taifa ili kumkomoa Malinzi kwa sababu ya chuki
na minyukano ya makundi yaliyoibuka wakati wa uchaguzi wa Rais wa TFF.
Habari kutoka ndani ya TFF zinasema kuwa katika mechi mbili
na timu ya soka ya taifa ya Msumbuji, waasi hao waliwatumia baadhi ya wachezaji
wa stars kucheza chini ya kiwango, wengine kucheza rafu za makusudi na kumwaga
fedha kwa mmoja wa waamuzi na matokeo ya mchezo huo yaliishia kwa sare ya bao
1-1.
Katika mchezo wa marudiano uliofanyika wiki mbili baadaye
mjini Maputo, Stars ilitolewa kwa kufungwa bao 2-1, huku ikinyimwa penalti na
kukataliwa bao lingine katika mazingira ya kutatanisha.
“Katika mechi zote mbili, kundi hilo liliwatumia baadhi ya
wachezaji kucheza chini ya kiwango na kumhonga mmoja wa waamuzi fedha. Fedha
hizo zilikabidhiwa kwa mchezaji mmoja wan je anayecheza soka la kulipwa katika
moja ya vilabu vikubwa nchini ambaye naye alimkabidhi mwamuzi huyo aliyeiua
Stars,” alisema mtoa habari wetu.
Uchunguzi umebaini kuwa tayari Serikali imeagiza kuunda tume
ya kuchunguza kashfa hiyo na kuapa kuwachukua hatua dhidi ya watakaobainika
kuhusika na uasi huo dhidi ya timu ya taifa.
Malinzi aliyeingia madarakani mwishoni mwa mwaka jana,
amekutana na wakati mgumu ndani ya Shirikisho hilo, licha ya kufanya maandalizi
makubwa kwa timu hiyo, kuiwezesha kushiriki michuano ya AFCON.
Katika maandalizi ya mwaka huu, stars ilipewa maandalizi
makubwa chini ya udhamini mnono wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia
kinywaji chake cha Kilimanjaro.
Licha ya udhamini huo, pia Serikali imekuwa karibu na TFF
kuhakikisha timu ya soka inafanya vyema na kuondokana na aibu ya kugeuzwa kuwa
kichwa cha Mwendawazimu.
Stars mwaka huu ilifanya maandalizi makubwa chini ya kocha
wake Mart Nooij kwa kuweka kambi takribani mwezi mzima nchini Botoswana, na pia
Tukuyu mkoani Mbeya kwa lengo la kuhakikisha inashiriki AFCON mwakani nchini
Morocco.
“Hii hali
inasikitisha sana. Kama mtu ana bifu na Malinzi, hamfanyie yeye lakini sio
kuihujumu timu ya taifa. Kwa taarifa yako hao watu wataanikwa muda si mrefu
maana wanajulikana,” alisema mtoa habari wetu.
Alipoulizwa juu ya kuwapo kwa hujuma hizo, Rais wa TFF
Malinzi, hakukubali wala kukataa na badala yake alisema kama kweli kuna watu wa
aina hiyo, taifa litakuwa limefika mahali pabaya.
“Mimi katika hilo,
sina cha kusema, lakini kama kuna ukweli ndani yake, nitasikitika sana, maana
hii timu siyo yangu mimi ni timu ya Taifa,”alisema Malinzi.
chanzo Moblog
No comments:
Post a Comment