Stori na Deogratius Mongela na Chande Abdallah
Kibano! Jamaa mmoja ambaye jina halikupatikana mara moja,
amejikuta akinusa kifo baada ya kula kipigo ‘hevi’ wakati akifanya jaribio la
wizi wa fedha kiasi cha shilingi laki 450,000 kupitia huduma za fedha kwa
mitandao ya simu.
Akiomba kuachiwa baada ya kupewa kichapo kikali.
Tukio hilo lililoshuhudiwa na Ijumaa Wikienda lilijiri
wikiendi iliyopita maeneo ya Kijitonyama jijini Dar ambapo jamaa huyo alidaiwa
kuingia kwenye duka moja akijifanya anataka kutoa shilingi laki nne na nusu
(450,000/=) jambo lililomfanya wakala kumuonesha namba za kutolea kwa
uchangamfu akijua ni mteja wa kawaida.
Dakika chache baadaye wakati wateja wengine wakiendelea
kuhudumiwa, jamaa huyo alionesha meseji kuwa ametoa kiasi hicho cha fedha
kupitia moja ya mitandao ya simu.
Wakala huyo alipoichukua meseji ya jamaa huyo ili
kuhakikisha muamala wake alishangaa kuona meseji hiyo kuwa ni ya mtandao
mwingine tofauti na alioutaja huku ikionesha imeandikwa au kutumwa na namba ya
kawaida ya simu badala ya namba ya huduma hiyo ya mtandao husika.
Wakizidi kumshushia kichapo.
Wakala huyo, Maulid Vedasto alishangaa na kuamua kumshikilia
jamaa huyo akimuitia mwizi ndipo wananchi wenye hasira kali walipofika na
kumzingira wakimtaka atoe maelezo ya kutosha ambapo
njemba huyo ilikiri kutaka
kuiba jambo lililoamsha hasira za watu walioamua kumshushia kipigo hevi nusura
afe.
Akizungumza na Ijumaa Wikienda, wakala huyo alisema kuwa
jamaa huyo alifika mara ya kwanza siku hiyo dukani kwake akitaka kutoa shilingi
elfu sabini lakini alighairi na kurudi baada ya muda mfupi akitaka kufanya
jaribio hilo la wizi.
Kichapo kikiendelea.
“Nilianza kumtilia shaka mara ya kwanza alipokuja na
kujifanya anataka kutoa fedha huku akiwa na wasiwasi na kila mara alipokuwa
akiwaona watu wengi ndipo alipokuwa akiniongelesha akijifanya ana haraka ya
kutoa fedha, akiona watu wachache anasubiri,” alisema wakala huyo.Baada ya
kunaswa jamaa huyo alipekuliwa kwenye simu yake ambapo iligundulika kuwa kweli
meseji hiyo haikuwa ya mtandao husika huku akiwa hana salio.
Katika kuhakikisha hilo, wakala huyo aliwapigia simu makao
makuu ya mtandao huo na kupata taarifa kuwa hakuna salio la aina hiyo
lililohamishwa kutoka kwenye simu ya jamaa huyo.Katika utetezi wake, jamaa huyo
aliomba watu wasimuue kwa kuwa ni tamaa za kidunia zilimponza huku akikiri
kufanya utapeli huo kwa kushirikiana na wenzake watatu ambapo wamefanikiwa
kutapeli mawakala kibao jijini Dar.
“Jamani inatosha mlivyonipiga, naomba msiniue ni shetani tu
amenipitia. Kweli nakiri kuwa nimewaibia mawakala wengi sana lakini nimekoma.
Nipelekeni polisi msiniue,” alisema jamaa huyo ambaye alikuwa akivuja damu
chapachapa kisha kupelekwa Kituo cha Polisi cha Kijitonyama ‘Mabatini’ kusubiri
sheria kuchukua mkondo wake.
No comments:
Post a Comment