Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, October 27, 2011

IGP SAID MWEMA ATOA TAARIFA JUU YA TISHIO LA UGAIDI AFRIKA MASHARIKI

 
Mkuu wa jeshi la polisi nchini IGP Said Mwema akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo katika makao makuu ya Jeshil hilo jijini Dar es salaam.
1. Awali ya yote napenda niwashukuru kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuelimisha jamii kuhusu mambo mbalimbali ya maendeleo na hasa suala la kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu hapa nchini.
2. Nimewaiteni leo kwa ajili ya kutaka kuwapa taarifa za mambo mbalimbali zikiwemo za matishio ya ugaidi yaliyoanza kujitokeza katika nchi ya jirani ya Kenya, Uharamia unaojitokeza katika ukanda wa Bahari ya Hindi na matukio mengine yanayojitokeza yakiwemo ya ajali za barabarani.
3. Jeshi la Polisi linapenda kuwaondoa wasiwasi wananchi juu ya Ugaidi unaoendelea katika nchi ya jirani ya Kenya, kwamba, tayari tumejipanga vyema kwa kuimarisha ulinzi na hasa maeneo yote ya mipakani na kazi hii inafanyika kwa ushirikiano na vyombo vingine vyote vya ulinzi na usalama.
4. Vile vile, kuna matukio ya uharamia na uhamiaji haramu ambayo yamekuwa yakijitokeza katika ukanda wa Bahari ya Hindi hususani katika mikoa ya Pwani, Mtwara na Lindi. Katika kipindi cha mwaka huu maharamia wapatao 13 wamekamatwa na tayari wamefikishwa mahakamani.
5. Tunatoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhali ya watu ama makundi ya watu watakaowatilia mashaka kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa ili hatua za haraka za kiusalama ziweze kuchukuliwa. Watumie namba za simu zifuatazo 0787 668306, 0222138177, 111, 112 na namba za Makamanda wa mikoa, wakuu wa Polisi wa Wilaya (OCDs) na RTOs zilizokwishasambazwa hadi ndani ya mabasi.
6. Jeshi la Polisi linawashukuru wananchi wote ambao wamekuwa wakitupa taarifa ambazo zimefanikisha kukamatwa kwa baadhi ya wahalifu hao. Tunawaomba wananchi wote kuiga mfano huo wa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi katika kufichua uhalifu wa aina yoyote ile na hasa matukio ya kikatili yanayofanyika kwa watu wenye ulemavu wa ngozi na madereva wazembe wanaosababisha ajali barabarani.

No comments:

Post a Comment