Serikali yatoa tamko kuhusu mikesha ya CHADEMA mkoani Arusha
Wakati jeshi la Polisi mkoani Arusha
likiwa limefanikiwa kuwasambaratisha wafuasi wa CHADEMA, ambao walikuwa
wamejikusanya katika viwanja vya NMC, jijini hapo kwa lengo la kufanya
mikesha ya amani, serikali mkoani humo, imetoa tamko zito kuhusu vurugu
za kisiasa zinazoendelea kushamiri mkoani humo na hivyo kuhatarisha
ustawi wa shughuli za kiuchumi.
Mwanzoni mwa wiki hii, maelfu ya wafuasi
wa CHADEMA, walikusanyana katika viwanja vya NMC, maarufu kama Unga
Limited, jijini Arusha, katika mkutano wa hadhara ambao chama hicho
kupitia kwa katibu mkuu wake, kilitoa tamko la kufanya mikesha ya amani
mahali hapo kwa lengo la kuishinikiza mahakama kumuachia huru mbunge wa
jimbo la Arusha, Godbless Lema, ambaye anashikiliwa rumande kwa kukataa
dhamana, katika kesi inayomkabili yeye na wafuasi wengine 18 wa CHADEMA.
Hatua hiyo, ililikwaza jeshi la Polisi
ambalo liliingilia kati na kuwasambaza wafuasi hao wa CHADEMA, katika
zoezi ambalo lilifanyika alfajiri ya jumanne, huku katibu mkuu wa chama
hicho, Dk. Wilbroad Slaa na mbunge mwingine wa chama hicho, Tundu Lissu,
wakikamatwa na Polisi, katika tukio ambalo inaelezwa kuwa mwenyekiti
wao, Freeman Mbowe, alifanikiwa kukimbia eneo la tukio kabla ya
kukamatwa.
Viongozi hao pamoja na wanachama wengine
20, walifikishwa mahakamani mchana wa leo ambako walisomewa mashtaka ya
kufanya mkusanyiko bila kibali, ambapo baadae Dk. Slaa na Lissu,
waliachiwa kwa dhamana sanjari na wafuasi wengine 9, huku wengine 11
wakibakia rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Akizungumza na Jukwaa Huru, kwa njia ya
simu jioni ya leo, mkuu wa mkoa wa Arusha, Magesa S. Mulongo, amesema
kuwa Jeshi la Polisi mkoani mwake lilifanikiwa kusambaratisha wafuasi
hao wa CHADEMA, bila kusababisha majeruhi kwa mtu yeyote yule, na
akalipongeza jeshi kwa ufanisi na busara walizozitumia katika
kufanikisha zoezi hilo.
“Zoezi la kuwatawanya wafuasi wa
CHADEMA, lilifanywa kwa utulivu mkubwa sana, na zaidi ya mabomu ya
machozi, hakukuwa na matumizi ya silaha zingine za moto wala hakukuwa na
wananchi wowote waliojeruhiwa katika tukio hilo na hivi tunavyoongea
hali iko shwari huku wananchi wakiendelea na shughuli zao za uzalishaji
mali kama kawaida” alisema mkuu wa mkoa.
Mkuu huyo wa mkoa amemuambia mwandishi
wa Jukwaa Huru kwa njia ya simu kuwa, serikali imesikitishwa na kauli za
kuchochea vurugu ambazo zimekuwa zikitolewa na viongozi wa CHADEMA, na
kwamba serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa inadhibiti
vitendo vya namna hiyo kwani licha ya kwamba havijayumbisha shughuli za
kawaida za mji wa Arusha, zinatishia kudumaza maendeleo kama zikiachwa
ziendelee.
“Ukweli ni kwamba hakujawa na athari
zinazoweza kuelezwa kuwa zimefanya shughuli fulani za kawaida kudorora
kwasababu wananchi walio wengi wangali wanaendelea na shughuli zao. Hata
takwimu kuhusu utalii na hususan kwa miezi hii, hazionyeshi kuwa kuna
anguko lolote la idadi ya watalii, lakini hatuwezi kuacha hali hii
kuendelea;
“Wananchi na hata wafuasi wengine wa
CHADEMA, tunapoongea nao wanaeleza wazi wazi kuwa wamechoshwa na hali
hii na mimi kama msemaji wa serikali katika mkoa huu, nitoa wito kwa
vyama vyote vya siasa kuachana na hizi siasa zinazoanza kushamiri za
kiuchochezi na kishabiki zaidi, ni lazima ifike mahali viongozi hawa
wajue kuwa wanatakiwa kuwatumikia wananchi na hatuwezi kuleta maendeleo
kwa mikusanyiko ya kila siku namna hii” alifafanua Bw. Magesa.
Amesema kuwa, serikali imeanza kuchukua
hatua za kuona hali mjini Arusha na katika mkoa huo kwa ujumla unarejea
katika hali ya amani ambapo tayari yeye kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali wameshaanza kufanya vikao vya kuweka mikakati ya kuhakikisha
kuwa hali ya amani na uelewano baina ya wanasiasa unarejea na kuurejesha
mkoa wake katika hali tulivu
“Tunataka kuanza upya, hatuwezi
kuendelea kuangalia siasa hizi ambazo zinatishia ustawi wa kimaendeleo
ziendelee kukua mkoani hapa. Tumeanza kukutana na wadau mbalimbali na
hususan viongozi wa kidini na tutaendelea kukutana na wadau mbalimbali
wakiwemo wanasiasa wa vyama mbalimbali kwa lengo la kuona ni njia gani
iliyo sahihi na bora ya kuendesha shughuli za kisiasa kwa lengo la
kukuza maendeleo ya mkoa na sio kusimamisha kazi za uzalishaji kila
kukicha kwa mikusanyiko isiyo na tija” aliongeza.
Endelea kufuatilia habari zetu, ambapo
tutakuletea mahojiano hayo moja kwa moja kama yalivyofanywa na mwandishi
wetu kwa njia ya simu.
No comments:
Post a Comment