Picha zaidi zinakuja wadau
MAANDAMANO ya wanahabari mkoa wa Iringa leo yatikisa mji wa Iringa baada ya wananchi kusitisha shughuli zao na kushiriki kuunga mkono maandamano hayo makubwa ya aina yake mkoani Iringa.
Katika maandamano hayo yaliyopita mitaa mbali mbali ya mji wa Iringa ikiwa ni pamoja na stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoni wasafiri walishuka katika mabasi waliyokuwa wakisubiri kuanza safari na kuungana na wanahabari hao kwa kusindikiza kwa muda maandamano hayo .
Wakitoa maoni yao juu ya maandamano hayo baadhi ya wananchi akiwemo Maneno Mbuma na mzee Said Sanga walisema kuwa hofu ya mkuu wa mkoa wa Iringa kupokea maandamano hayo haikupaswa kuwepo kutokana na utulivu na hekima ya hali ya juu iliyoonyeshwa na wanahabari hao.
Mbuma alisema kuwa jamii ya mkoa wa Iringa haipotayari kuendelea kukosa haki yao ya msingi ya kupata habari kwa ubaguzi na manyanyaso ya ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa dhidi ya wanahabari na kuwa vyombo vyote vya habari vinapaswa kupewa haki sawa ya kuhabarisha umma juu ya matukio yanayotokea katika mkoa.
Hivyo alisema kama kweli ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa haikuwa na matatizo hayo ambayo wanahabari wameamua kuyapinga basi mkuu wa mkoa Dkt Christina Ishengoma angekubali kupokea maandamano hayo ya amani ila kukimbia kupokea maandamano hayo ni sawa na kuogopa ukweli dhidi ya ofisi yake.
Huku Sanga akimtaka mkuu wa mkoa wa Iringa kulegeza msimamo wake na kukaa chini na wanahabari hao ili kujenga mahusiano mema badala ya kuendelea kujenga daraja kati ya ofisi yake na vyombo vya habari.
Akipokea maandamano hayo ya wanahabari zaidi ya 60 wa vyombo mbali mbali mkoani Iringa mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Iringa (IPC) ambao ndio walidhamini maandamano hayo ya wanahabari mkoani hapa ,Daud Mwangosi alisema kuwa wengi wamekuwa na mitazamo tofauti juu ya maandamano hayo huku baadhi ya watu wakidhani wanahabari hao wanaandamana kwa ajili ya kutetea kulipwa posho na baadhi wahusisha maandamano hayo na itikidi za kisiasa na kuwa maandamano hayo hayakuwa na mitazamo hiyo kama wanavyofikiri bali ni maandamano ya kupinga manyanyaso dhidi ya wanahabari na ubaguzi dhidi yao.
Pia alitaka wanahabari mkoani Iringa kutokubali kuendelea kunyamaza kimya kwa ubaguzi unaofanywa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa pamoja na ofisa habari wa ofisi hiyo Denis Gondwe
Alisema kuwa IPC itaendelea kuwaunga mkono wanahabari katika kupinga vitendo vyote vya ukandamizaji na manyanyaso kwa wanahabari katika mkoa wa Iringa na kuendelea kuungana na vilabu vya wanahabari kute nchini ambavyo havipo tayari kunyanyaswa na vyombo vya umma na kumwima haki yao ya kutoa habari ama kupata habari.
Mwangosi pia amewapongeza viongozi wa vilabu vya wanahabari mkoa wa Mbeya, Ruvuma , Arusha na mikoa mingine ambayo imetoa tamko la kuunga mkono maandamano hayo ya wanahabari likiwemo jukwaa la wahariri hapa nchini kwa kutoa msimamo wao wa kuunga mkono maandamano hayo ya amani ya kupinga wanahabari kunyanyaswa na kuutaka muungano wa vilabu vya wanahabari Tanzania (UTPC) kushiriki kupinga manyanyaso kwa wanahabari pia.
Katika hatua nyingine wanahabari hao mkoani Iringa wametangaza msimamo wao iwapo mkuu wa mkoa wa Iringa Dkt Ishengoma hatajibu madai yao na kuendelea na msimamo wake wa kupuuza madai ya wanahabari hao basi hawata kuwa tayari kushirikiana na ofisi yake .
Maoni ya Felix Mwakyembe kutoka mtandao wa wanabidii leo .Hata hivyo mimi nina mtazamo tofauti kidogo, sikuona haja ya kuandamana barabarani, suluhisho ilikuwa kuachana nao. Ilitosha kutoa tamko la kutoandika habari za viongozi katika mkoa huo, kwanza sio lazima sana.
Habari ziko kwa wananchi, hawa ndio wasio na jukwaa la kutolea madukuduku yao. Habari za wananchi ndizo zenye kuibua uozo wa hao viongozi, mwisho wa siku wangekuja wenyewe, wanawapigia magoti.
Sioni ninachopungukiwa napoacha kuandika habari zao. Mbeya tunatumia sana msimamo huo na unafanya kazi. Maandamano yatawapa kiburi, watajiona wao ni muhimu zaidi. Mathalani, mnalazimika kuwabembeleza polisi wawape kibali, hawa ni kundi moja.
Lazima nasi tujenge professional arrogance, watambue bila wewe hawako salama. Tuepuka kuamini kuwa tu sehemu yao, hata anapokuchekea bado sio mwema kwako katika nafasi yako ya mwanahabari.
Tukiweka kipaumbele kwa habari za wananchi, watarudi kwenye mstari.
No comments:
Post a Comment