Rais Jakaya Kikwete
NI KUJADILI MUSTAKABALI WA MAWAZIRI WALIOTAKIWA KUJIUZULU, WENYEWE WAVUNJA UKIMYA
Waandishi Wetu
WAKATI
joto la wabunge, vyama vya siasa na wanaharakati nchini kutaka mawaziri
waliohusishwa na kashfa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) wajiuzuluzu likizidi kupanda, Mwenyekiti wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete ameitisha kikao cha
ghafla cha Kamati Kuu ya chama hicho kujadili pamoja na mambo mengine,
hali ya siasa nchini.
Habari
zilizolifikia gazeti hili jana na kuthibitishwa na Katibu wa Itikadi na
Uenezi Nape Nnauye, zilieleza kuwa kikao hicho kitafanyika leo Ikulu ya
Dar es Salaam kuanzia saa 4:00 asubuhi.
Ingawa
Nape alisema hawezi kutaja ajenda za kikao hicho kwa kuwa ni siri,
habari kutoka baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM, zilidokeza kuwa
hakuna namna, Rais Kikwete akakwepa kuzungumzia shinikizo la mawaziri
hao kujiuzulu.
"Ni
kweli kesho (leo) tuna Kamati Kuu Dar es Salaam, lakini agenda za kikao
hicho haziwezi kuwekwa 'public' ujue hivyo tu inatosha," alisema Nape.
Nape
alishindwa kuthibitisha au kukanusha taarifa kwamba kikao hicho
kitajadili hatima ya mawaziri hao wanaotakiwa kujiuzulu badala yake
akasema,"Kama nilivyokwambia hakuna agenda ya kuweka 'public' wewe hayo
unayoyazungumza unayajua wewe ukitaka yangu, andika nilichokwambia."
Mawaziri
wanaotakiwa kujiuzulu ni Kepteni George Mkuchika (Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa-Tamisemi), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii),
William Ngeleja (Nishati na Madini), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa
Jamii), Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Profesa Jumanne Maghembe
(Kilimo, Chakula na Ushirika), Mhandisi Omar Nundu (Uchukuzi) pamoja
na Mkulo na Nyalandu.
Wakati
kukiwa na taarifa za Kamati Kuu kuwajadili mawaziri hao, watano kati
yao wameonekana kutokuwa tayari kujiuzulu huku baadhi wakihoji sababu za
kufanya hivyo na Waziri wa Fedha Mustafa Mkulo akisema kuwa hajui madai
ya wabunge hao dhidi yake.
Waziri
Mkulo (Fedha), Lazaro Nyalandu (Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na
Masoko) na Athuman Mfutakamba (Naibu Waziri wa Uchukuzi), walisema
hawafikirii kujiuzulu kwa kuwa hawajui makosa yao.
Shinikizo
la kutaka mawaziri nane wajiuzulu liliibuka katika Mkutano wa Saba wa
Bunge uliomalizika mjini Dodoma mwanzoni mwa wiki hii, baada ya ripoti
hiyo ya CAG kuonyesha tuhuma nzito za ufisadi katika wizara hizo huku
baadhi ya mawaziri wakionekana kuhusika moja kwa moja na maamuzi
waliyofanya.
Baadhi
ya mawaziri hao walitoa utetezi wao bungeni na wengine walipokutana kwa
nyakati tofauti na waandishi wa habari, lakini jitihada hizo za
kujisafisha hazikuzaa matunda kutokana na ongezeko la shinikizo hilo
kutoka kwa makundi mbalimbali ya kijamii.
Mkulo: Sijui kinachoendelea
Mkulo
ambaye alikuwa waziri wa kwanza kutakiwa na wabunge ajiuzulu, kutokana
na kashfa ya kuvunja Bodi ya Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC)
ili kuficha tuhuma zake ikiwemo uuzaji wa kiwanja Na.10 kwa Kampuni ya
Mohamed Enterprises (MeTL), alisema hawezi kuzungumzia suala la
kujiuzulu kwa sababu hajui kosa lake wala madai ya wabunge dhidi yake.
Waziri
huyo alisema yaliyozungumzwa na wabunge hakuyasikia kwa kuwa hakuwapo
bungeni Dodoma kwa muda mrefu kutokana na kuwa safarini.
Alipoulizwa
kama yuko tayari kujiuzulu kuhusiana na kashfa zinazoikabili wizara
yake, Mkulo alijibu, ‘ hapa, no comment," akiwa na maana kwamba hana cha
kuzungumza.
“Kwanza sifahamu tuhuma zilizotolewa na wabunge kwa sababu sikuwepo, mimi nilikuwa safari,” alisema.
Hata
alipoulizwa kuhusiana na wizara yake kuuza kiwanja hicho cha Serikali
kilichopo katika Barabara ya Nyerere, jijini Dar es Salaam kinyume cha
taratibu, Mkulo aliendelea kusema, ‘no comment, no comment kwa hilo.’
Mfutakamba
Jana
Mfutakamba aliliambia Mwananchi kuwa haoni sababu yoyote ya kujiuzulu
kwani hana tuhuma zozote ndiyo maana pia hata wabunge katika orodha yao
hawakuweza kumtaja popote.
Mfutakamba
alitoa kauli hiyo wakati ambao Waziri Nundu amemtuhumu kwamba amekuwa
akishinikiza Kampuni ya China Communication Construction Company (CCCC),
ipewe kazi ya kujenga gati namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es
Salaam kwa kuwa ilimgharamia safari kwenda nje ya nchi.
Hata
hivyo, Mfutakamba alikiri kusafirishwa na kampuni hiyo na kuongeza
kwamba alikwenda huko kutembelea miradi mbalimbali ikiwamo ya ujenzi wa
reli na magati kwa kufuata taratibu zote na aliporudi aliieleza Serikali
uwezo wa kampuni ya CCCC, Kampuni ambayo inapingwa na Nundu aliyedai
kuwa ilimsafirisha Mfutakamba baada ya yeye kukataa.
Nyalandu
Jana,
Nyalandu alisema kuwa, mpaka sasa haelewi kwanini ameingizwa kwenye
kashfa hiyo kwa sababu katika ripoti ya CAG, hakutajwa na wenyeviti wa
kamati mbalimbali za kumudu za Bunge.
“Sielewi
kwanini nimeingizwa kwenye kashfa hii kwa sababu katika ripoti ya CAG
sikuwemo. Ripoti ya Mwenyekiti wa Kamati ya POAC na PAC simo pia, lakini
nilishangaa nilipoanza kusikia jina langu,” alisema Nyalandu.
Aliongeza
kuwa baadhi ya mawaziri waliotuhumiwa kwenye kashfa hiyo waliitwa na
Kamati ya CCM kwa ajili ya mahojiano, lakini yeye hakuitwa.
Alisema
kutokana na hali hiyo anashindwa kuelewa kwanini jina lake lilikuwa
miongoni mwa watu waliotajwa wakati hayumo kwenye ripoti yoyote.
Alisema
kutokana na hali hiyo anaamini kuwa watu waliomtaja wana sababu zao
binafsi, kwamba Kamati za Bunge ndizo zenye majukumu ya kuthibitisha
ukweli kuhusu tuhuma anazopewa.
Tayari
Nyalandu alitoa waraka unaonyesha msimamo tofauti na wa bosi wake, Dk
Chami kuhusu kashfa zinazowakabili ambazo ni tuhuma alizonazo Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la Viwango (TBS), Charles Ekelege anayedaiwa
kuanzisha kampuni hewa za ukaguzi wa magari nje ya nchi hususani, Hong
Kong na Singapore.
Wakati
Nyalandu akishauri Ekelege asimamishwe kazi ili apishe uchunguzi wa CAG
na endapo hatakuwa na tuhuma za kujibu arudishwe kazini, waziri wake
(Chami) alisema kuwa Ekelege ni mteule wa rais, hivyo hawezi kwenda kwa
Rais Jakaya Kikwete kumtaka amwondoe wakati hakuna taarifa yoyote
inayoonyesha tuhuma zake.
Sakata
la kuwepo kwa kampuni hizo hewa za ukaguzi wa magari liliwekwa wazi
katika ripoti iliyotolewa na CAG na wenyeviti wa kamati za kudumu za
Bunge za Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) inayoongozwa na Zitto Kabwe
na ile ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC) ya John Momose Cheyo huku
ikielezwa kuwa wanamkingia kifua Ekelege kutokana na kushindwa
kumchukulia hatua.
Mponda aahidi kuweka mambo hadharani leo
Kwa
upande wake, Dk Mponda alipoulizwa kama atajiuzulu kutokana na kashfa
zinazoikumba wizara yake alisema atazungumzia suala hilo kesho (leo) na
kuongeza, “Njoo Ijumaa tutazungumza, leo sisemi chochote, nipigie
asubuhi ili nikupangie muda wa kuja ofisini,”alisema Dk Mponda.
Waziri
huyo anakabiliwa na kashfa ya Bohari ya Dawa (MSD) ambako ukaguzi
maalum katika bohari hiyo uliofanyika ulibaini kuwapo tofauti ya Sh
658.9 milioni ikiwa ni pungufu ya kiasi ambacho kilipokelewa na
kuripotiwa wizarani kwenda MSD, huku ushahidi wa kuzipokea kutotolewa.
Pia,
uchunguzi unaonyesha kuwapo Sh 100 milioni zilizopelekwa MSD kutoka
Wizara ya Afya na kutumiwa na bohari hiyo bila kuwepo kwa mchanganuo wa
matumizi.
Ukaguzi
pia ulibaini kuwepo kwa kiasi cha Sh 4.5 bilioni zilizotoka Hazina
kwenda Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa ajili ya kununulia dawa na
vifaa vya hospitali, lakini kiasi cha Sh 4.344 bilioni ndio
kilichopelekwa MSD ukiondoa Sh 196 milioni ambazo zilitumika bila
kuwapo kwa ushahidi wa kupokelewa MSD kutoka Wizara ya Afya.
Maige anena
Waziri
Maige juzi aliamua kueleza baadhi ya tuhuma zinazomkabili ikiwamo
umiliki wa nyumba aliyodaiwa kuinunua kwa Dola 700,000 za Marekani,
akisema nyumba hiyo aliinunua kwa dola 410,000 na siyo dola 700,000 kama
ilivyoelezwa.
Hata
hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Malisili na Mazingira,
James Lembeli alipinga kauli hiyo akisema taarifa alizonazo zinaonyesha
Maige alinunua nyumba hiyo kwa fedha taslimu dola 700,000.
Kashfa
nyingine inayomkabili Maige ni ile iliyotolewa na Kamati ya Bunge ya
Ardhi, Maliasili na Mazingira huku ikitaka awajibishwe kwa kutengeneza
mazingira ya rushwa katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji kwa kampuni
ambazo hazina sifa na kusafitishwa nje kwa wanyama wakiwamo twiga na
tembo kinyume cha sheria.
Hata
hivyo, Maige alisema hivi sasa kuna mapambano ya kisiasa baina ya
viongozi mbalimbali na kwamba habari mbaya dhidi yake zinalenga
kumchafua kutokana na kuwa mkali katika utendaji wake wa kazi na
kuongeza, kuna chuki kutokana na kwamba aliwahi kuwafukuza kazi baadhi
ya watendaji wizarani kwake jambo ambalo limewaudhi baadhi yao.
Mbunge
wa Kigoma Kaskazini (Chadema) Zitto Kabwe ndiye aliyenogesha hoja hiyo
ya kutaka mawaziri hao wajiuzulu baada ya kutaka Bunge lipige kura ya
kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kama Serikali
haitawafukuza kazi mawaziri hao.
SOURCE
Mwananchi
No comments:
Post a Comment