*SITTA ADAI WANAOKIMBILIA HUKO NI MAGAMBA YEYE SI MMOJA WAO, LOWASSA AMSHANGAA LEMA, ASEMA KUHAMIA CHADEMA SI SIRI,
SIKU chache baada ya
aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kuwataja
mawaziri wawili na mmoja aliyewahi kuwa Waziri Mkuu kwamba, wameomba
kujiunga na chama hicho cha upinzani, wawili kati yao wamejitokeza na
kuzungumzia madai hayo.
Waziri Mkuu
aliyejiuzulu, Edward Lowassa na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Samuel Sitta ambao walitajwa na Lema, jana kwa nyakati
tofauti walibeza madai hayo.
Jumamosi iliyopita, Lema
akiwa wilayani Sengerema, Mwanza alisema mawaziri watatu, akiwamo mmoja
aliyewahi kuwa waziri mkuu wameiomba kujiunga na Chadema lakini mmoja
kati yao amekataliwa na wengine mchakato wa kuyakubali maombi yao
unaendelea.
Katika mkutano huo, Lema
aliwataja mawaziri hao kwa jina moja kuwa ni Sitta, Lowassa na waziri
mwingine ambaye tunahifadhi jina lake kwa kuwa hakupatikana jana
kuzungumzia madai hayo.
Msimamo wa Sitta
Sitta alipuuza madai
hayo akiyaita ya kitoto na kueleza kuwa kwa hadhi yake, hawezi kuomba
kujiunga Chadema na kusubiri majibu kama amekubaliwa au la.
“Yaani mimi niombe
kwenda Chadema halafu nikae kabisa huku nikisubiri wanijibu! Huo ni
upuuzi na jambo hili haliwezekani na si kweli hata kidogo. Kama Lema
kasema hivyo, basi huo ni utoto na siasa za kihuni,” alisema Sitta.
Sitta huku akicheka
aliongeza: “Sasa nimeomba kwa nani na kwa njia ipi ya mdomo au
maandishi? Mimi siyo gamba. Ni mtu mwadilifu siwezi kujiunga katika
utaratibu wa kuchukua magamba ndani ya CCM.”
“Wao
Chadema wanachukua tu kila mtu. Wakienda kwenye mikutano pia wanachukua
tu watu, sasa hivi wanachukua magamba CCM. Mimi nawatakia kila heri
katika kuchukua magamba CCM.”
Sitta alisema yeye ni
mwanasiasa makini na mwadilifu hawezi kukaa chungu kimoja na magamba...
Wanalofanya kuchukua magamba ya CCM ni faraja hata kwa Katibu Mkuu
Wilson Mukama.”
Mbunge huyo wa Urambo
Mashariki, alisema kuchukua magamba CCM ni sawa na mtu ambaye anakwenda
kwa jirani ambaye nyumba yake imezungukwa na takataka kisha akamsaidia
kuzisomba kwenda kuzitupa... Hapo si lazima ufurahie bwana?
Alisema kama angekuwa
anajiunga na Chadema wangemkumbatia akisema: “Kama wanakwenda watu
wadogo wanaandaa sherehe kubwa, nikienda mimi...?
Majibu ya Lowassa
Jana, Lowassa naye
alipuuza madai hayo ya Lema akisema hajawahi kuomba kujiunga na Chadema
huku akisisitiza: “Kama ingekuwa hivyo isingekuwa siri. Ningetangaza
uamuzi wangu kupitia vyombo vya habari.”
Lowassa alitoa kauli
hiyo baada ya gazeti hili kumtaka azungumzie madai ya Lema kwamba
aliomba kujiunga na chama hicho cha upinzani lakini akakataliwa.
“Kama ningeomba kuingia
Chadema ningetangaza kwenye vyombo vya habari. Sijasikia hayo na sitaki
kusema chochote zaidi,” alisema Lowassa na kisha kukata simu.
Slaa amshangaa Lema
Alipoulizwa kuhusu madai hayo ya Lema, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema hawezi kuzungumzia kauli ya mtu.
“Tabia yangu huwa
sipendi kuzungumzia kauli aliyoitoa mtu hivyo alichokisema Lema
mtafuteni yeye mwenyewe afafanue kwani atakuwa anajua alichokisema kina
maana gani,” alisema Dk Slaa.
Dk Slaa alisema: “Badala
ya kukaa na kuzungumzia kauli ya mtu, kinachotakiwa ni kujadili jinsi
gani ya kuhakikisha tunapunguza ugumu wa maisha kwa mwananchi wa hali ya
chini.”
“Tuache kuzungumza kauli
za watu hapa sasa kinachotakiwa kila mmoja wetu kwa nafasi yake
atizame ni jinsi gani atahakikisha anamkomboa mwananchi kwa kupunguza
gharama za maisha.”
Lema ang’ang’ana
Hata hivyo, jana
alipotakiwa kufafanua kauli yake baada ya kuelezwa kwamba aliowataja
wabeza madai yake, Lema aliendelea kusisitiza kwamba alichosema ni cha
kweli.
“Wanakataa tu kisiasa,
lakini nilichosema ni cha kweli na (kesho), leo katika mkutano wangu wa
Singida, pamoja na kuwarudia hawa niliowataja nitawataja wengine pamoja
na wabunge wa CCM ambao wapo tayari kujiunga na Chadema.”
Katika madai yake ya
kwanza aliyotoa Jumamosi iliyopita katika mkutano uliofanyika kwenye
Viwanja vya Mnadani, Lema alisema viongozi wenye uchungu na taifa hili
ndani ya CCM na ambao wamekuwa hawafurahishwi na ubadhirifu wa mali za
nchi, wamekuwa wakifanya mazungumzo kutaka kujiunga na Chadema.
Alisema kwa vile chama
chake kimejiandaa kuingia madarakani kwa kutumia nguvu ya umma, ndiyo
maana mawaziri wa Serikali ya CCM wameomba kujiunga nacho ili kusaidiana
kwa pamoja kwenda kuingia madarakani mwaka 2015.
“Lakini, Lowassa
tumemkataa. Tunataka wachapa kazi na wenye mioyo ya kweli katika
mapambano ya kupigania haki na kuondoa dhuluma kwa Watanzania,” alisema
Lema.
Lema alidai kuwa
mawaziri hao (waliokubaliwa) wanasubiri muda muafaka ufike waweze
kutangaza rasmi kujiunga na chama hicho, kutokana na kile kilichodaiwa
kuchoshwa na mwenendo mzima wa uongozi na utendaji serikalini na ndani
ya CCM, hususan suala la kuwalinda watu wanaotuhumiwa kwa ubadhilifu.
|
Kilimo : EFTA Yafadhili Wakulima wa Tano kwenda Nchini Uturuki kujifunza na
kubadilishana Maarifa na Ubunifu wa Kilimo.
-
*Na Magesa Magesa, Dar es Salaam.*
Katika juhudi za kuhakikisha wakulima nchini wanapata maarifa na mafunzo
zaidi ya mbinu bora za kilimo.
Kampun...
10 hours ago
No comments:
Post a Comment