Ndugu Wananchi,
Kama ilivyo ada naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa
Rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kumaliza nusu ya kwanza ya
mwaka 2012 salama. Kwa kutumia utaratibu wetu wa kuzungumza nanyi kila
mwisho wa mwezi, leo napenda kuzungumzia mambo mawili. Jambo la kwanza
ni suala la usafirishaji haramu wa binadamu nchini na la pili ni la
mgomo wa madaktari.
Usafirishaji Haramu wa Binadamu Nchini
Ndugu Wananchi;
Bila ya shaka mtakuwa mmezisikia taarifa za tukio la kushtusha na kuhuzunisha la kukutwa maiti 43
za watu wasiojulikana, zilizotupwa katika kichaka kilichopo kijiji cha
Chitego, Wilayani Kongwa, Mkoa wa Dodoma tarehe 26 Juni, 2012. Pamoja
na maiti hao, walipatikana watu 84
wakiwa hai lakini wote wakiwa wamedhoofu na baadhi yao wakiwa
mahututi. Hatua za haraka zilichukuliwa kuwasafirisha watu hao hadi
Dodoma ambapo wale waliokuwa mahututi walifikishwa Hospitali Kuu ya Mkoa
wa Dodoma kwa matibabu na wengine walihifadhiwa katika Kituo cha Kati
cha Polisi, Dodoma. Maiti 22 zilipelekwa Dodoma na 21 zilipelekwa Morogoro kuhifadhiwa.
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa wale walionusurika zimebainisha kuwa watu
hao ni raia wa Ethiopia ambao walikuwa safarini kwenda Malawi na
baadaye Afrika ya Kusini ambako wangetengenezewa utaratibu wa kwenda
kuishi Marekani na Ulaya. Kwa mujibu wa maelezo yao, safari yao ilianza
miezi mitano iliyopita. Mwezi mmoja waliutumia Ethiopia na miezi minne
waliitumia Kenya kabla ya kuletwa Arusha ambako walipakiwa kwenye lori
na kuanza safari ya kuelekea Malawi lakini ikaishia Chitego. Lori
walilopanda lilikuwa limezibwa kabisa na hivyo kusababisha vifo kwa
kukosa hewa.
Tukio
la Chitego, Dodoma la wahamiaji haramu kukamatwa na wengine kukutwa
wamekufa si la kwanza kutokea hapa nchini. Kwa jumla, katika kipindi
cha takriban miaka 10 sasa kumekuwepo na tatizo kubwa la wahamiaji
haramu kuingia nchini. Kwa mfano, kati ya mwaka 2005 na hivi sasa jumla
ya wahamiaji haramu 19,683 wamekamatwa. Karibu wote wameshaondoshwa nchini na hivi sasa wapo karibu watu 1,500
tu magerezani wanaotumikia adhabu na kusubiri kurejeshwa makwao. Wengi
wa watu hao wanatoka Ethiopia na Somalia na baadhi kutoka Pakistan na
Bangladesh.
Wahamiaji haramu wamekuwa wanaingia nchini kwa kupitia
njia zisizo rasmi. Wapo wanaotumia nchi kavu hasa kupitia mikoa ya
Mara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga. Na, wapo wanaopitia baharini kwa
kutumia fukwe za Pemba, Unguja na za mikoa ya ukanda wa Pwani ya
Tanzania Bara yaani Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara.
Ndugu Wananchi;
Kwa mujibu wa kauli zao, watu hao wamekuwa wanaeleza kuwa hawaji nchini kuhamia bali wao ni wapita njia tu.
Wanaelekea Afrika ya Kusini ambako wameahidiwa kuwa watatengenezewa
mipango ya kuhamia Marekani na Ulaya. Watu hao pia wamethibitisha
kuwepo kwa watu maalum wanaojihusisha
na usafiri wao tangu nchi watokako na zote wanazopitia mpaka kule
waendako. Aidha, wamesema kuwa wao wanawalipa watu hao ili
wawasafirishe na hakika si kiwango kidogo. Kwa jumla ni kwamba hili si
suala la uhamiaji haramu bali ni la biashara haramu ya kusafirisha binadamu.
Ndugu Wananchi;
Kufuatia
vyombo vyetu vya usalama kuwa makini
na watu wengi kukamatwa ndipo wasafirishaji walipobuni njia za
kuwasafirisha kama mizigo. Makontena, malori yaliyofunikwa nyuma na
matenki ya mafuta na ya maji yamekuwa yanatumika kwa ajili hiyo.
Usafiri wa aina hiyo ndiyo uliosababisha vifo vilivyotokea Dodoma tarehe
26 Juni, 2012 na vya watu 21 vilivyotokea mwezi Desemba, 2011 Mkoani Morogoro, na vile vya watu 12 vilivyotokea katika matukio mawili ya Mkoa wa Mbeya, mwezi Mei, 2012.
Ndugu Wananchi;
|
No comments:
Post a Comment