|
Na Mwandishi Wetu
WAKATI vitendo vya uhalifu vikizidi kuongezeka sehemu mbalimbali nchini, sasa silaha kutoka nchi jirani zinadaiwa kuingia kwa wingi na kuuzwa mitaani na baadhi yake kubadilishwa na mahindi, Mwananchi Jumapili limegundua.
Uchunguzi
uliofanywa unaonyesha kuwa, kutokana na kushamiri kwa biashara hiyo ya
silaha nchini, bunduki moja aina ya Short Machine Gun (SMG) sasa inauzwa
kati ya Sh300,000 hadi Sh500,000, huku bunduki aina ya AK 47 ikiuzwa
kwa Sh700,000 hadi Sh1 milioni.
Wakati vijiji kadhaa mkoani Tabora
vilipokumbwa na uhaba wa chakula, bunduki aina ya SMG katika Kijiji
cha Usinge wilayani Urambo zilibadilishwa kwa gunia moja la mahindi,
huku AK 47 ilibadilishwa kwa magunia mawili ya mahindi.
Gazeti
hili huko nyuma liliwahi kuripoti kuuzwa kwa bastola holela mitaani
katika miji mikubwa ikiwamo Arusha, Mwanza, Moshi ambapo silaha hiyo
ilikuwa ikiuzwa kati ya Sh800,000 hadi shilingi milioni moja.
Uchunguzi
wa muda mrefu uliofanywa na Mwananchi Jumapili katika mikoa mbalimbali
iliyopo mipakani umebaini kuwa, mtandao huo wa uingizaji silaha ni
mkubwa na unawashirikisha matajiri na baadhi ya askari polisi wasiokuwa
waaminifu.
Silaha hizo huingizwa nchini kupitia mkoani Kigoma, mpakani mwa Rwanda, Kenya, na Burundi kwa kutumia njia mbalimbali ikiwamo, magari, pikipiki na boti kupitia Ziwa Victoria pamoja na baiskeli ambapo bunduki hizo hufungwa kama mzigo ya kawaida.
Chanzo
kimoja cha uhakika kililiambia Mwananchi Jumapili kuwa eneo la Usinge
ndiyo kituo kikuu cha kupokelea silaha kutoka Burundi na Rwanda ambazo
husambazwa mikoa mbalimbali nchini.
Mawakala Mmoja wa watu ambao wamewahi kufanya biashara alisema kuwa mawakala wa silaha hizo wapo katika mikoa ya Kigoma na Tabora na kwamba ni wafanyabiashara, huku baadhi wakidaiwa kuwa watu wenye asili ya kabila la Kitutsi.
Lakini kwa Usinge alimtaja mfanyabiashara mmoja ambaye
pia hukopesha fedha kwa riba (jina tunalo) ambaye inadaiwa kuwa
biashara hiyo haramu anayoifanya inajulikana na mamlaka mbalimbali za
juu serikalini.
Habari hizo zilieleza kuwa mfanyabiashara huyo
amekuwa akinunua SMG kati ya Sh300,000 hadi Sh500,000, na kwamba
huzisafirisha kwa kutumia mtandao wake hadi mikoa ya Kanda ya Ziwa na
huziuza kati ya Sh800,000 hadi Sh1,000,000.
Mbali na kutumia silaha hizo kwa ujambazi pia huzitumia kufanya uwindaji wa tembo kwenye hifadhi za taifa na mapori ya akiba.
Habari
hizo zinaeleza kuwa baada ya kuyapata meno hayo ya tembo na kukatwa
vipande, husafirisha kwa kusaidiwa na maofisa wa maliasili na askari
polisi wasiokuwa waaminifu.
Askari hao inadaiwa wanatumiwa na
wafanyabiashara wakubwa kuuza meno ambapo huwalinda watu hao wanapokuwa
wanasafirisha nyara hizo huku wakiwa wamevalia sare zao za kazi.
Zinafafanua
kwamba wanaposafirisha bidhaa hizo, huyaweka meno katika magunia ya
mkaa kutokea Wilaya za Serengeti, Bunda, Bariadi, Maswa hadi Mwanza
ambapo mtandao wa watumishi wa umma wasiokuwa waaminifu huipokea mizigo
hiyo na kuisafirisha kwenda kwa mawakala wa biashara hiyo.
Kwa
mujibu wa vyanzo huru vya habari, silaha hizo hupokewa Mwanza ambapo
huuzwa kwa wingi wilayani Serengeti kwa ajili ya kufanyia uhalifu na
uwindaji wa wanyama pori.
“Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (Tanapa)
kwa kutumia wapelelezi wao wamejitahidi kutoa taarifa Polisi lakini
wanaokamatwa baada ya muda huachiwa…, Polisi ni chanzo kikubwa hapa,”
zilieleza habari hizo.
Silaha kutokea Somalia
Inadaiwa kuwa silaha hizo zinazotokea Somalia, huingizwa nchini kwa njia ya panya kupitia Kenya kwa kutumia punda ambao huwa wanakokota mikokoteni iliyopakiwa magunia ya mahindi au karanga ambayo ndani yake huwa na silaha hizo.
Tanapa wasaka mtandao
Tangu kuuawa kwa Tembo ‘George’ maarufu kama tembo wa JK, Tanapa inadaiwa kutumia gharama kubwa kuusaka mtandao huo bila mafanikio.
Mmoja wa
maofisa wa shirika hilo kwa sababu za kiusalama jina limehifadhiwa
aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa anajua taarifa zote za upatikanaji wa
silaha wanazozikamata.
“Kuna mambo ambayo yanatusumbua sana maana
wenzetu (polisi) wanatangaza kuwa wamekamata silaha, lakini baadaye
waliokamatwa huachiwa baada ya kutoa fedha,” alisema ofisa huyo na
kuongeza:
“Kama rushwa itaendelea hali ya usalama kwa mikoa ya
Kanda ya Wiwa itakuwa mbaya maana silaha ni nyingi na zilizokamatwa ni
kidogo kuliko zilizopo.”
Ofisa huyo alikwenda mbali zaidi kwa
kufafanua kwamba baadhi ya watuhumiwa wanaouza na kusafirisha silaha
hizo wana uhusiano na baadhi ya maofisa wa polisi ambao huvujisha siri
kila inapofanyika operesheni ya kuwakamata watu hao.
“Matatizo
yote yanachangiwana maofisa wa polisi ambao hawana mpango wa kumaliza
tatizo hili hatari, nchi itageuka dampo la silaha za kivita, vyombo vya
usalama vinatakiwa kuwachunguza maofisa wanaotuhumiwa, tena wachunguzwe
mpaka mali zao kwani baadhi yao wanadaiwa kujengewa nyumba,”
kilibainisha chanzo hicho.
Kamanda Simon Sirro Kamanda wa operesheni Tanzania, Saimoni Siro aliyeendesha msako wa watuhumiwa wa ujambazi waliohusika na mauaji ya mtalii na Meneja Msaidizi wa Kambi ya Ikoma Bush na kupora vitu mbalimbali alikiri hivi karibuni kuwa, uingizaji wa silaha za kivita unazidi kushika kasi.
"Uhalifu wa
kutumia silaha unazidi kushika kasi, wengine wanahusika na ujangili
katika hifadhi na wengine kwenye matukio kama haya ya uhalifu lakini
tunakabiliana nao kuhakikisha wahusika wanakamatwa, nashukuru hata wazee
wamekerwa na hali hii na wanatoa ushirikiano mzuri maana nimeitwa hadi
kikao cha wazee wakanieleza nao mikakati yao," alisema.
RPC Mara
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Robert Boaz na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa huo, Emmanuel Lukula kwa nyakati tofauti waliliambia Mwananchi Jumapili juu ya ongezeko la silaha za kivita mkoani humo na kueleza kuwa hali hiyo inatishia usalama wa raia na mali zao, ikiwemo uwindaji haramu.
Kamanda
Boaz alisema kwa kipindi cha Januari 2011 hadi Mei 2012, bunduki 25
zimekamatwa na nyingine kusalimishwa kwa hiari ambapo kati ya hizo SMG
ni 19 na Riffle 8.
Risasi zilizokamatwa ni 686 za SMG na 630 za Riffle na short gun zikiwa 56.
“Ni
kweli silaha za kivita zinaingizwa nchini kutoka nchi jirani na idadi
hiyo ni kubwa na bado zipo nyingine hazijakamatwa ila bado tunaendelea
na uchunguzi kwa kuwa inaonyesha zinaingizwa kwa ajili ya kufanya
uhalifu,” alisema Kamanda Boaz.
Aliongeza, “Lakini wapo wanaonunua na kudai kwamba wanazitumia kwa ajili ya kulinda mifugo yao, lakini silaha za kivita hairuhusiwi kumilikiwa na mtu,” alisema.Alipoulizwa kama askari nao wanahusika katika vitendo hivyo Boaz alisema, “Ndiyo nasikia kutoka kwako, ila sina uhakika.” Akizungumzia matukio yaliyotokea Mei mwaka huu alisema zilikamatwa bunduki nne aina ya SMG pamoja na risasi 436 ambazo ziliingizwa na watu kutoka Urambo na Kigoma na kwamba, mbili kati za silaha hizo zilikuwa zimeishaingia wilayani Serengeti kwa mkazi mmoja wa Kijiji cha Bisarara ambaye awali alitoa risasi 228 na baada ya kubanwa akatoa nyingine. Inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa amenunua SMG mbili na baada ya kukamatwa alitaja mtandao wake ambao mmoja wa wenzake alikamatwa mjini Magumu na mwingine Bunda.
RPC Kagera
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Henry Salewi alikiri kuingizwa kwa silaha hizo nchini kutoka nchi za Uganda na Rwanda na kufafanua kwamba, huingizwa kupitia njia za panya na kwamba ni vigumu kuwadhibiti watu hao. “Ni kweli silaha zinaingizwa kwa njia ya mabasi na boti. Eneo la mpaka wa nchi ni kubwa hivyo kuwakamata ni kazi ila juhudi zinafanyika” alisema. Alisema silaha hizo zinatumika katika uhalifu na kuongeza, “Kwa kushirikiana na wananchi tumekamata SMG na AK 47 pamoja na watu wanaopeleka silaha hizo mikoa mbalimbali, wananchi wasikubali kukaa kimya wakati wakiwafahamu watu hawa.”
RPC Shinyanga
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Athumani Diwani aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa silaha hizo zinatoka nchi za Rwanda na Burundi na kwamba wanaoziingiza wanapitia mkoani Kigoma. “Tuna changamoto kubwa kwa kuwa kasi hiyo hasa kwa mwaka jana ilikuwa kubwa, wanaingia na silaha za kivita,” alisema Diwani. Alisema kuwa taarifa za polisi kuhusika katika matukio hayo wamezipata na wanazifanyia kazi. RPC Kigoma Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma Kamishna Msaidizi, Frasser Kashai aliliambia gazeti hili kwamba sababu kubwa ya kushamiri kwa vitendo vya uingizaji silaha inatokana na udhibiti mdogo katika maeneo ya mipaka ya nchi na kwamba jambo hilo linavisumbua vyombo vya ulinzi na usalama.
“Burundi
licha ya kuwa ni nchi ndogo, wameathiriwa na migogoro, jambo
linalowafanya waingie nchini kutafuta hifadhi, lakini wanaingia na
silaha na kufanya uhalifu huku wakisaidiwa kuhifadhiwa na wananchi,”
alisema Kashai.
Alisema kuwa bunduki aina ya SMG na AK 47 ndizo zinazotumika katika uhalifu na uwindaji wa wanyama. ”Wanakuja na nia mbalimbali lakini wakiona hali siyo nzuri wanaingia katika hifadhi. Hivi sasa tunashirikiana na Tanapa kufanya msako. Tunawaomba wananchi washirikiane na Jeshi la Polisi ili kukomesha vitendo hivi,” alisema Kashai. RPC Tabora Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora (ACP) Anthony Rutha alisema watu hao wanaingiza bunduki kwa kuzipitisha porini na kwamba huingizwa na wakimbizi ambao hurudi nchini kwa maelezo ya kuja kusalimia ndugu na jamaa. “Kambi ya Ulyanhulu inatusumbua sana kwa kuwa pale zinaingizwa silaha kali kama SMG na AK 47 na kituo chao kikubwa ni Urambo, Sikonge na hasa Usinge ambako kunatisha zaidi kutokana na kuzungukwa na mapori,” alisema. Hata hivyo alisema kwa sasa Usinge kumetulia baada ya kituo cha polisi kufunguliwa mapema mwaka huu. “Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Mwanza, Mara,Tabora, Shinyanga, Kigoma na Kagera ziliomba kibali ofisi ya Waziri Mkuu ili tufanye operesheni za pamoja lakini hatujawahi kujibiwa, bila kufanya hivyo hali itakuwa mbaya.” alisema Rutha. Rutha alisema mpaka sasa amepata taarifa kuwa baadhi ya askari wilayani Kibondo wanahusika katika matukio hayo na kwamba jambo hilo linachunguzwa. RPC Mwanza Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Liberatus Barlow alisema kuwa silaha hizo zinaingizwa kutoka nchi jirani za Rwanda na Burundi.
“Kwa
jinsi mazingira yalivyo watu hawa wanaingia nchini kwa kutumia njia za
majini, barabara pamoja na njia zisizo halali jambo linalofanya vikosi
vya ulinzi kushindwa kuwadhibiti watu hawa,” alisema.
SOURCE http://mwananchi.co.tz |
No comments:
Post a Comment