ASEMA WANAIBA HATA FEDHA ZA UKIMWI
KATIBU
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa
ameifananisha mioyo ya viongozi na watendaji wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) na mawe yasiyosikia, kuhisi wala kuona jambo lolote, liwe zuri au
baya.
Alisema
mioyo yao ni sawa na mawe, ndiyo maana wanadiriki kuiba fedha
zinazotengwa kupambana na ugonjwa wa ukimwi ilhali waathirika
wakiendelea kutaabika kwa kukosa huduma bora ya afya.
Kauli
hiyo aliitoa juzi alipokuwa akihutubia katika mikutano ya hadhara
katika vijiji vya Msowero na Dumila, ikiwa ni sehemu ya mikutano ya
Operesheni Sangara - M4C inayoendelea katika maeneo mbalimbali ya Mkoa
wa Morogoro.
“Kwenye
Serikali ya CCM hakuna viongozi wenye mioyo yenye nyama, wote mioyo yao
ni ya jiwe kwa kuwa wanaiba hata fedha zinazotengwa kwa ajili ya
kupambana na ukimwi,” alisema.
Alibainisha
kuwa, vitendo vya ubadhirifu na wizi wa rasilimali za umma ndivyo
vinavyowafanya wananchi wengi waendelee kuwa masikini, huku vigogo
wachache na familia zao wakiishi maisha ya anasa kila kukicha.
Alisema
Watanzania wanahitaji kufanya uchambuzi wa kina juu ya mapato
yanayopatikana, yanavyotumiwa na kiasi kilichobaki badala ya kusikiliza
kauli za serikali kuwa, imefanya mambo makubwa kwenye maendeleo.
Dk.
Slaa alieleza kusikitishwa na kushamiri kwa ubadhirifu na wizi wa fedha
za umma kwenye idara, taasisi na halmashauri mbalimbali hapa nchini.
Alisema
kuna uwezekano mkubwa wa kuganda kwa akili za wafanyakazi wa
Halmashauri ya Gairo iliyopo mkoani Morogoro, ambao kila kukicha kosa la
wizi na ubadhirifu wa fedha za walalahoi linajirudia pasipo watendaji
wa ofisi hiyo kuchukua hatua.
“Hivi
kwanini tusione kama akili za watendaji hawa zimeganda kwa maana
nilipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za serikali za Mitaa
tulibainisha uwepo wa upotevu wa zaidi ya sh bilioni moja katika
Halmashauri ya Kilosa, hakuna hatua iliyochukuliwa,” alisema.
Maendeleo ya taifa
Dk.
Slaa alisema Watanzania wana haki ya kudai chenji yao kwa watawala na
wasifungwe na madai kuwa kuna mambo mengi ya maendeleo yaliyofanyika
katika miaka 50 ya uhuru.
Alisema
ni ujinga kwa serikali kujinasibu kuwa imefanya maendeleo makubwa
katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru kwa sababu rasilimali zilizopo hapa
nchini hazilingani na kile kilichofanywa.
Alibainisha
kuwa, mkwamo wa maendeleo unatokana na kushamiri kwa ufisadi kuanzia
ngazi za chini, hivyo serikali haipaswi kujinasibu kuwa imejenga
kilometa 11,000 za lami.
“Ugomvi
wangu mkubwa na viongozi wa serikali, CCM ni maendeleo tuliyonayo
hayalingani na rasilimali zetu. Wao wanasema sisi ni wapotoshaji na
vipofu, hakuna anayepinga kwamba hakuna kilichofanyika kwa miaka 50 hii
ya uhuru, bali tunahoji kama inalingana na kiasi kinachoingia
serikalini,” alisema.
Alisema
watu wanapohoji chenji serikalini wanakuwa wameshafanya uchambuzi na
kulinganisha utajiri wa rasilimali zilizopo, kodi zinazokusanywa kila
siku, madini mbuga za wanyama na vinginevyo.
Amwaga chozi
Dk.
Slaa alidondosha machozi mbele ya hadhara alipokuwa akizungumzia
madhila yanayowapata wafugaji kwa kugeuzwa chanzo cha fedha na baadhi ya
askari wasiokuwa waaminifu.
Kiongozi
huyo alifikia hatua hiyo baada ya kuanza kueleza namna mmoja wa
viongozi wa wafugaji wilayani Kilosa alivyomfuata na kumweleza kuwa
askari wa Jeshi la Polisi, mgambo na viongozi wa serikali za vijiji
wanavyowanyanyasa na kuwadhalilisha wafugaji.
“Nikiwa
Kilosa mjini juzi, nilifuatwa na kiongozi wa wafugaji akaniambia baada
ya kukamatwa, wake zao au mabinti zao hufanyiwa vitendo vya
udhalilishaji mbele ya macho yao, lengo likiwa ni kuwafanya wawakomboe
kwa haraka katika mateso hayo, hii inasikitisha kuona Tanzania imefikia
hapa,” alisema.
Huku
akifuta machozi, Dk. Slaa alisema inasikitisha kuona watu waliopewa
dhamana ya kuongoza ndio walio mstari wa mbele kuwanyanyasa na kuwatesa
wananchi.
Picha na habari kwa hisani ya http://chademablog.blogspot.com
No comments:
Post a Comment