Baadhi ya walimu wa shule hiyo
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Silabu Mizeki Charahani akiwa ofisini kwake.
Na Joachim Mushi, Korogwe
WANAFUNZI
wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Silabu iliyopo Wilaya ya
Korogwe, mkoani Tanga wanasomea kwenye uchochoro unaotenganisha kati ya
darasa moja na lingine kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.
Wanafunzi
hao ambao darasa lao limekuwa likihama kila muda kutengemea hali ya
hewa (jua na mvua) kufuata kivuli wamelazimika kusomea nje kwenye
uchochoro ambao haujaezekwa kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa
shuleni hapo.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni katika shule hiyo, Mwalimu
Mkuu wa Shule ya Msingi Silabu, Mizeki Charahani alisema wanafunzi hao
wamelazimika kusomea nje kwa kuwa wanavyumba vinne tu vya madarasa
ambavyo havitoshelezi kwa mahitaji ya shule.
Akifafanua
zaidi alisema darasa hilo eneo lao maalumu la kusomea (darasa) ni
kwenye uchochoro unaotenganisha kati ya darasa moja na lingine, lakini
huwa wanahama jua linapozidi au mvua kunyesha na kwenda eneo lingine
linalokuwa na kivuli.
“Darasa
hili kwa kweli huwa linahama kulingana na hali ya hewa, jua likizidi
wanabeba madawati yao na kuhamia eneo lenye kivuli, mvua ikinyesa hivyo
hivyo wanahamia sehemu nyingine…lakini muda mwingine tunawahamishia
kwenye darasa moja na wenzao pale kunapokuwa hakuna mwingiliano wa
vipindi,” alisema Charahani.
Alisema
shule hiyo yenye darasa la kwanza hadi la saba unauhaba mkubwa wa
vyumba vya madarasa kwani hata darasa la kwanza na la pili wanasomea
kwenye darasa moja kwa kupokezana.
“Kutokana
na uhaba wa vyumba vya madarasa hata hatuna darasa la awali wala ofisi
ya walimu…na sisi ofisi yetu ipo hapa chini ya mti huu,” alisema Mwalimu
huyo huku akionesha eneo moja chini ya mti ulio mbele ya madarasa ya
shule hiyo.
Akizungumzia
hali hiyo, Ofisa Elimu Taaluma, Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Elius
Mkwizu alikiri kuwepo kwa tatizo hilo la uhaba wa vyumba vya madarasa
katika shule hiyo na kudai shule hiyo ni mpya hivyo ujenzi wake
haukwenda sambamba na ongezeko la wanafunzi kimadarasa.
Alisema
tayari uongozi wa idara hiyo kwa kushirikiana na wananchi unafanya
ujenzi wa madarasa mawili ambayo yatasaidia kupunguza uhaba wa vyumba
vya madarasa katika shule hiyo. Hata hivyo aliongeza ujenzi huo kwa sasa
umesimama baada ya fedha zilizotengwa kurejeshwa hazina kuu baada ya
kukaa kipindi kirefu bila kutumiwa.
Mwandishi
wa habari hizi alishuhudia moja ya ujenzi wa darasa lililosimama baada
ya kukosekana kwa fedha za kuliendeleaza. Akifafanua zaidi Mkwizu
alisema kulikuwa na mvutano kati ya viongozi waliokuwawakisimamia ujenzi
huo na wananchi hali iliozua mgogoro na ujenzi kusimama.
No comments:
Post a Comment