SHIRIKISHO
la Soka Tanzania (TFF), limesema litaanza kufanyia kazi kwa vitendo
tatizo la utumiaji wa dawa za kulevya hususan bangi unaodaiwa kufanywa
na baadhi ya wachezaji hapa nchini.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam jana, Rais wa TFF, Leodegar Tenga, alisema
miongoni mwa changamoto kubwa zinazowakabili ni kile kinachodaiwa kuwa
baadhi ya wachezaji wanatumia bangi, ingawa bado hawajapata ushahidi.
“Tunasikia,
lakini hatuna ushahidi, kwamba vijana wetu wanatafuna bangi, ila
viongozi wengi wamekuwa wakilisemea pembeni, sisi kama wazazi jukumu
letu ni kuwaelimisha juu ya athari zake, maana wao wanaotumia wanaweza
kuona inawaongezea hamasa, lakini hawajui madhara yake,” alisema Tenga.
Alisema
wameagiza suala hilo lianze kufanyiwa kazi katika timu ya taifa, Taifa
Stars na Ligi Kuu Bara, ambako viongozi wanapaswa kukaa chini na vijana
wao kuwapa elimu nasaha, kabla ya kuanza kuchukuliwa hatua.
“Bangi
na mpira ni vitu viwili tofauti, tumeagiza elimu ianze kutolewa kuanzia
national team (timu ya taifa) na Premier League (Ligi Kuu), ikiwezekana
waletewe hata wataalamu waweze kuwapa elimu kabla hatujaanza kuchukua
hatua, ambapo kutakuwa na testing (vipimo) ya kushtukiza na
atakayekataa, kanuni zinachukua mkondo wake mara moja,” alisisitiza
Tenga.
Tenga
aliongeza kuwa, suala hilo litawekwa katika kanuni za Ligi Kuu na
tayari Kamati ya Tiba imepewa maelekezo kuhusiana na hilo, ambapo
litaanza kufanyiwa kazi mara tu elimu itakapokuwa imetolewa kwa
walengwa.
Jumamosi
iliyopita, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenera Mukangara
pia aliwataka wachezaji chipukizi kutojiingiza katika utumiaji wa dawa
za kulevya wakati akitoa zawadi kwa washindi wa michuano ya BancABC
SUP8R, ambapo Simba walitwaa ubingwa.
Katika
hatua nyingine, Tenga ameelezea kufurahishwa na hamasa iliyoko katika
usajili hapa nchini, lakini akakosoa watu wasio wataalamu wa ufundi
kuendesha zoezi hilo, badala ya makocha au kamati za ufundi.
Alisema
walikubaliana kuruhusu usajili wa nyota kutoka nje kwa lengo la
kuhamasisha ushindani hapa nchini, kwani njia nzuri ya kumpa ujuzi
mchezaji ni kumpa nafasi kucheza na yule aliye mzuri zaidi.
“Utamaduni
duniani kote, usajili unafanywa na kocha, lakini hapa mchezaji
anasajiliwa na mdhamini au kiongozi, mambo ambayo hujiingiza kwenye
matatizo, timu ikifungwa wanachama wanakufuata nyumbani. Mi huwa
nashangaa timu ikifungwa watu wanavamia viongozi, kumbe hatujajiweka
vizuri,” alisema.
Tenga
alitaka wataalamu ndio wapewe jukumu hilo, huku akisisitiza kuwa,
vijana wenye vipaji ambao wapo hivi sasa hapa nchini wapewe nafasi na si
lazima kukimbilia nje, labda iwe kwa mchezaji mzuri zaidi.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment