Jeshi
la polisi mkoani Iringa linawashikilia watu watatu wakazi wa mkoani
hapa kwa tuhuma za kuhusika kwenye tukio la wizi wa ngombe ambalo
limetokea usiku wa kuamkia Agosti 27 mwaka huu.
Kamanda
wa polisi mkoani Iringa, Michael Kamhanda amewataja watuhumiwa hao kuwa
ni Onesmo Ndondole, mwenye umri wa miaka 30, mkazi wa kijiji cha
Kitelewasi, Titus Amon, umri miaka 25, mkazi wa Itimbo, wilayani Kilolo
na Isaya Muyinga mwenye umri wa miaka 18, mkazi wa Kigonzile, manispaa
ya Iringa.
Kamanda
Kamhanda amesema baada ya kufanyika kwa upelelezi jeshi la polisi
limefanikiwa kuwapata ng’ombe 4, kati ya saba ambao wameibiwa.
Kamanda
Kamhanda ameongeza kuwa mifugo hiyo ni mali ya Bw. Julius Mhandisi,
mkazi wa Ilula wilaya ya Iringa vijijini, ambao waliibiwa majira ya
usiku wakiwa kwenye zizi.
Wakati
huo huo, watu wawili wamefariki kwenye matukio mawili tofauti likiwemo
la kupigwa na watu wasiofahamika na miili yao kutelekezwa njiani ikiwa
na majeraha sehemu za kichwani.
Kamanda
wa polisi amemtaja Dicto Mballa, mwenye umri wa miaka 38, mkazi wa
kijiji cha Ugenza, amefariki baada ya kupigwa na kitu kizito kichwani.
Katika
tukio la pili Kamanda Kamhanda amesema Jutindus Kipesile, mwenye umri
wa miaka 38, mfanyabiashara wa kinyanambo B, amefariki baada ya kukatwa
na kitu chenye ncha kali kichwani na mwili wake kutelekezwa njiani.
Hata
hivyo hakuna mtu ambaye amekamatwa kuhusiana na matukio hayo, jeshi la
polisi linaendelea na uchunguzi ili kuwabaini watuhumiwa wa matukio hayo
na watuhumiwa wa wizi wanatarajia kufikishwa mahakani kujibu tuhuma
zinazowakabili.
No comments:
Post a Comment