HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWA WANANCHI, TAREHE 31 AGOSTI, 2012
Utangulizi
Ndugu Wananchi;
Kila mwisho wa mwezi nimekuwa nazungumza na taifa kuhusu masuala mbalimbali muhimu kwa taifa letu na watu wake. Leo nina mambo mawili ya kuzungumza nanyi. Lakini,
kama ilivyo mazoea yetu hatuna budi kwanza tumshukuru Mwenyezi Mungu,
muumba wetu, kwa kutujaalia baraka zake, za uhai na uzima na kutuwezesha
kuwasiliana leo tarehe 31 Agosti, 2012.
Ndugu Wananchi;
Jambo
la kwanza ninalotaka kuzungumzia leo ni zoezi la Sensa ya Watu na
Makazi lililoanza tarehe 26 Agosti, 2012 ambalo linatarajiwa kumalizika
tarehe 01 Septemba, 2012. Mtakumbuka
kuwa tarehe 25 Agosti, 2012 nilizungumza nanyi na kuwaomba mjitokeze
kwa wingi na muwape ushirikiano unaostahili Makarani wa Sensa
watakapopita majumbani mwenu kutekekeza wajibu wao. Tumebakisha siku moja kufikia kilele cha sehemu ya kwanza ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.
Napenda kuwashukuru kwa dhati Watanzania wenzangu wote kwa kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa. Mpaka
sasa mwelekeo ni mzuri na ugumu ulioonekana kuwepo pale mwanzoni
uliendelea kupungua siku hadi siku kadri utekelezaji wa zoezi ulivyokuwa
unaendelea. Kwa mwenendo huu nina matumaini makubwa kuwa Sensa ya mwaka huu itakuwa na mafanikio mazuri.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kutumia nafasi hii kutoa wito kwa wale wote ambao hawajahesabiwa
wafanye hivyo. Naomba waitumie siku moja iliyosalia yaani tarehe 1
Septemba, 2012 kufanya hivyo. Aidha,
namuomba Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi Kuu ya Takwimu ya Serikali ya
Muungano na Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kuhakikisha kuwa kasoro zo zote zilizopo mahali po pote zinatafutiwa
ufumbuzi ili mambo yakamilike bila upungufu wowote.
Ndugu Wananchi;
Baada
ya kazi ya Makarani wa Sensa kuhesabu watu kufikia kilele chake, tarehe
2 Septemba, 2012, linaanza zoezi la kuwashughulikia wale ndugu zetu
ambao watakuwa bado hawajahesabiwa. Itakuwepo fursa ya siku saba kwa watu hao kuhesabiwa. Watatakiwa wao wenyewe kupeleka taarifa zao kwa Wenyeviti wao wa Serikali za Mitaa au Vijiji. Taarifa hizo zitafikishwa kwa Kamishna wa Sensa kwa ajili ya kujumuishwa. Baada ya muda huo kwisha, zoezi la kuhesabu watu litakuwa limefika mwisho. Yule ambaye atakuwa hakutumia fursa hizo mbili atakuwa amekosa kuingizwa katika hesabu ya Watanzania ya mwaka 2012. Napenda kuwasihi ndugu zangu, Watanzania wenzangu kutumia siku ya tarehe 1 Septemba, 2012 kuhesabiwa
na kama hapana budi basi tumia fursa ya kupeleka taarifa zako kwa
Mwenyekiti wako wa Mtaa au Kijiji katika siku saba zinazofuatia siku
hiyo ili nawe ujumuishwe.
Ndugu Wananchi;
Baada
ya kazi ya kuhesabu watu kwa namna zote mbili kufikia mwisho, itaanza
kazi ya uchambuzi na kuunganisha takwimu na taarifa zilizokusanywa. Kazi
hiyo ni muhimu na ni kubwa hivyo inahitaji umakini na uangalifu wa hali
ya juu sana, kwani ikikosewa zoezi zima la Sensa litaingia dosari. Nafarijika
kuhakikishiwa na Viongozi wa Sensa na Wakuu wa Idara za Takwimu za
Serikali zetu mbili, kwamba wanatambua ukweli huo na wajibu wao. Wameniarifu
kwamba kama mambo yatakwenda kama ilivyopangwa, matokeo ya awali ya
Sensa ya Watu na Makazi kuhusu idadi ya watu na jinsia zao yatatolewa
mwishoni mwa mwaka huu. Taarifa nyingine zitafuata baadaye. Narejea kuwasihi Watanzania wenzangu kuwapa nafasi wataalamu wetu wafanye kazi yao kwa ufanisi ili tupate matokeo yaliyo sahihi.
Mpaka na Malawi
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ninalotaka kuzungumza nanyi leo ni kuhusu mpaka baina ya Tanzania na Malawi katika Ziwa Nyasa. Kama mjuavyo, kwa miaka mingi nchi zetu mbili zinatofautiana kuhusu wapi hasa mpaka uwe. Sisi,
Tanzania, tunasema mpaka upo katikati ya ziwa wakati wenzetu wa Malawi
wanasema upo kwenye ufukwe wa ziwa upande wa Tanzania. Kwa maneno mengine wanasema ziwa lote ni mali ya nchi yao.
Utata kuhusu mpaka wetu katika Ziwa Nyasa haujaanza leo. Ulikuwepo tangu wakati nchi zetu mbili zikiwa bado zinatawaliwa na wakoloni na kuendelea baada ya Uhuru wa nchi zetu mpaka sasa. Jambo kubwa lililo tofauti na jipya ni kwamba hivi sasa, nchi zetu mbili zimeamua kukaa mezani na tunalizungumza suala hilo.
Chimbuko la Mzozo
Ndugu Wananchi;
Chimbuko
la mzozo wa mpaka uliopo sasa, baina ya nchi zetu mbili jirani, rafiki
na ambazo watu wake ni ndugu, ni makubaliano baina ya Waingereza na
Wajerumani kuhusu mpaka baina ya nchi zetu yaliyofanywa tarehe 1 Julai,
1890. Makubaliano hayo
yajulikanayo kama Mkataba wa Heligoland, (The Anglo-Germany Heligoland
Treaty) yalitiwa saini kule Berlin, nchini Ujerumani baina ya Waingereza
na Wajerumani. Wakoloni hao walikubaliana kuhusu mipaka baina ya makoloni yao na baina yao na wakoloni wengine waliopakana nao. Kwetu sisi hayo ndiyo makubaliano yaliyoweka mipaka ya Tanganyika na ile ya Zanzibar na majirani zake. Kwa upande wa Ziwa Nyasa, Waingereza na Wajerumani walikubaliana kuwa mpaka uwe kwenye ufukwe wa nchi yetu. Kwa maana hiyo ziwa lote likapewa nchi ya Malawi. Kwa upande wa Mto Songwe mpaka ulikuwa ufukweni upande wa Malawi kwa maana hiyo mto wote ukawa upande wa Tanzania.
Ndugu Wananchi;
Katika
kipengele cha Sita (Article VI) cha Mkataba huo, wakoloni hao
walikubaliana kufanya marekebisho ya mpaka mahali popote kama itakuwa ni
lazima kufanya hivyo, kulingana na mazingira na hali halisi ya mahali
hapo. Kwa mujibu wa kutekeleza matakwa ya kipengele hicho mwaka 1898 Tume ya Mipaka iliundwa. Ilianzia
kazi katika Mto Songwe kuhakiki mpaka baina ya nchi yetu na Malawi.
Tume ilikubaliana kuhamisha mpaka kutoka ufukweni mwa Mto Songwe upande
wa Malawi na kuwa katikati ya mto. Baada ya uhakiki katika eneo hilo kukamilika, mwaka 1901 mkataba mpya ulisainiwa kuhusu mpaka huo.
Tume
iliendelea na kazi yake katika Ziwa Tanganyika na kuhamisha mpaka
kutoka ufukweni hadi katikati ya ziwa na mkataba mpya kusainiwa mwaka
1910. Tume iliendelea katika ziwa Jipe ambapo mpaka ulihamishwa pia hadi katikati ya ziwa.
Ndugu Wananchi;
Bahati
mbaya Tume hiyo haikufanikiwa kufanya uhakiki wa mpaka katika Ziwa
Nyasa kutokana na kutokea kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kati ya mwaka
1914 - 1918. Kama tunavyokumbuka, Waingereza na Wajerumani waligeuka kuwa maadui na kupigana hata hapa nchini. Baada
ya vita hivyo na Ujerumani kushindwa, Baraza la Umoja wa Mataifa (The
League of Nations) liliikabidhi Uingereza udhamini wa Tanganyika. Hivyo,
Uingereza ikawa inatawala Malawi na Tanganyika.
Ndugu Wananchi;
Wakati Tume ya Uingereza na Ujerumani ilipokuwa imekufa, Tume ya Mipaka kati ya Uingereza na Ureno iliendelea na kazi. Matokeo
yake, mwaka 1954, Uingereza na Ureno zilitengua mkataba wao wa mwaka
1891 ulioweka mpaka wa Ziwa Nyasa katika ufukwe wa mashariki ya Ziwa,
yaani kwenye ufukwe wa Msumbiji, na kuuhamishia katikati ya ziwa.
Ndugu Wananchi;
Jambo
la kustaajabisha ni kuwa, Waingereza walioona umuhimu na busara ya
kurekebisha mpaka kati ya Malawi na Msumbiji, hawakuona umuhimu wa
kufanya hivyo kati ya nchi yetu na Malawi. Inashangaza,
kwa sababu wakati huo Uingereza ilikuwa mtawala wa nchi zetu mbili
hivyo kazi ya marekebisho ingekuwa rahisi, lakini hawakufanya hivyo. Na, baya zaidi ni kuwa hata pale watu wa nchi yetu walipotaka kupatiwa ufafanuzi na kutaka ukweli uwekwe wazi kuhusu mpaka hawakusikilizwa. Watu
walitaka ufafanuzi kwa sababu inasemekana kati ya mwaka 1925 na 1938,
taarifa ya Uingereza kwa Umoja wa Mataifa ziliweka mpaka katikati ya
ziwa. Lakini, kuanzia mwaka 1948 mpaka ukawekwa tena ufukweni.
Ndugu Wananchi;
Mwaka
1959, 1960 na 1962, suala la mpaka wa Malawi lilijitokeza tena na
kujadiliwa na Bunge la Tanganyika, wakati ule lilijulikana kuwa Baraza
la Kutunga Sheria, (Legislative Council – LEGCO). Hoja
ya Wabunge wa Tanganyika ilikuwa kwamba mpaka kuwekwa kwenye ufukwe
wetu kunawanyima wananchi wa Tanganyika wanaoishi kando kando ya ziwa
haki yao ya msingi ya kutumia maji kwa kunywa, kuoga, kuvua samaki na
kupata manufaa mengine yatokanayo na ziwa bila ya kuomba ridhaa ya
Serikali ya Koloni la Nyasaland kama Malawi ilivyokuwa inajulikana
wakati ule. Hoja
iliyotolewa ilikuwa kwamba Serikali ya Tanganyika ijadiliane na Serikali
ya Nyasaland kupitia Serikali ya Malkia wa Uingereza ili ufumbuzi
upatikane. Wakoloni
hawakujali na wala hakuna hatua zilizochukuliwa mpaka Tanganyika ikapata
uhuru wake tarehe 9 Desemba, 1961 na Malawi kupata uhuru wake mwaka
1964.
Juhudi za Kubadili Mpaka wa Ziwa Nyasa Baada ya Uhuru
Ndugu Wananchi;
Wakati
tulipopata Uhuru mwaka 1961, mjadala kuhusu mpaka wa Tanganyika na
Malawi uliendelea Bungeni, ambapo ilitolewa hoja kwamba zifanyike juhudi
za makusudi za kuanzisha na kuendeleza mazungumzo ya kurekebisha mpaka
huo kwa manufaa ya wananchi wote wanaoishi pembezoni mwa ziwa. Iliamuliwa kwamba tusubiri mpaka wenzetu wa Malawi wapate uhuru ili yafanyike mazungumzo baina ya nchi mbili huru. Kulijengeka matumaini kuwa mambo yangekuwa rahisi. Bahati mbaya haikuwa hivyo na kwamba mambo yakageuka na kuwa magumu na ya uhasama. Miaka
mitatu baada ya Malawi kupata Uhuru wake (1964), kunako tarehe 3
Januari 1967, Serikali ya Tanzania iliandika barua kwa Serikali ya
Malawi kuelezea tatizo la mpaka wa ziwani na kupendekeza nchi zetu mbili
zizungumze na kulitafutia ufumbuzi.
Ndugu Wananchi;
Bahati
nzuri tarehe 24 Januari, 1967, Serikali ya Malawi ikajibu kukiri
kupokea barua hiyo na kuahidi kuwa itatoa majibu baada ya muda si mrefu. Hata hivyo, tarehe 27 Juni, 1967, Rais Kamuzu Banda akilihutubia Bunge la Malawi, alikataa maombi ya Tanzania. Alisema hayana msingi na alidai kuwa kihistoria Songea, Mbeya na Njombe ni sehemu ya Malawi. Hivyo basi, mazungumzo yakafa.
Tanzania haikukata tamaa. Alipochaguliwa
Rais wa Pili wa Malawi, Mheshimiwa Bakili Muluzi, juhudi zilifanyika
lakini nazo hazikufika mbali. Bahati nzuri tarehe 9 Juni, 2005, Rais wa
Tatu wa Malawi, Mheshimiwa Bingu Wa Mutharika, ambaye sasa ni marehemu,
alimuandikia barua aliyekuwa Rais wa nchi yetu wakati ule, Mheshimiwa
Benjamin William Mkapa, kushauri nchi zetu zifanye mazungumzo kuhusu
mpaka wa ziwani. Alipendekeza iundwe Tume ya Pamoja itakayojumuisha Mawaziri na Wataalamu kutoka nchi zetu mbili. Tume hiyo itatoa mapendekezo kwa Marais wa nchi zetu mbili ambayo yatakuwa msingi wa majadiliano baina yao. Alisisitiza umuhimu wa kulipatia ufumbuzi suala hilo.
Ndugu Wananchi;
Kwa
kuwa ilikuwa kipindi cha mpito kuelekea kuchaguliwa Serikali ya Awamu
ya Nne, Rais Benjamin Mkapa hakuwahi kuishughulikia barua hiyo.
Nilipoletewa barua hiyo nikaijibu kukubali ushauri na mapendekezo yake. Aidha, nilipendekeza Wizara na Idara zipi za Serikali zetu zishirikishwe katika Tume hiyo. Bahati nzuri Rais wa Malawi alikubali mapendekezo yangu pamoja na lile la kwamba Malawi waitishe mkutano wa kwanza wa Tume hiyo.
Ndugu Wananchi;
Mpaka sasa mikutano mitatu ya Tume ya Pamoja imeshafanyika, wa kwanza ulifanyika tarehe 8 – 10 Septemba, 2010. Mkutano
wa pili ukafanyika tarehe 27 – 28 Julai, 2012 hapa Dar es Salaam na wa
tatu ukafanyika Mzuzu na Lilongwe tarehe 20 – 27 Agosti, 2012. Hatua
kadhaa zimepigwa lakini bado muafaka haujapatikana kwa maana ya madai
yetu ya kutaka mpaka uwe katikati ya ziwa na madai yao kuwa mpaka ubaki
ufukweni kwetu kama ilivyo kwenye Mkataba wa Heligoland wa Julai 1, 1890. Hoja ya wenzetu ni kuwa huo ndiyo mpaka tuliorithi wakati wa uhuru. Wanataka
tuthibitishe hivyo na kwamba tuzingatie kauli ya OAU ya kuheshimu
mipaka tuliyorithi kwa wakoloni. Wananukuu kauli ya Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere akisisitiza hoja hiyo katika mkutano wa OAU mwaka
1963.
Hoja za Msingi za Kutaka Mpaka Uwe Katikati ya Ziwa
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wetu tumekuwa na hoja kadhaa za kutaka mpaka uwe katikati ya ziwa. Ya
msingi kabisa ni ukweli kwamba Mkataba wa Heligoland umekosewa kwa
kuamua kuwanyima wananchi wa Tanzania wanaoishi ufukweni mwa ziwa haki
yao ya msingi ya kutumia maji na rasilimali zilizomo katika Ziwa Nyasa. Zipo sababu kadhaa kwa upande wetu kudai hivyo. Mojawapo
ni sheria ya kimataifa inayoelekeza kwamba popote kwenye maji ya asili
kama vile ziwa na mito iliyopo kati ya nchi mbili mpaka huwa katikati. Ndiyo utaratibu unaotumika duniani kote, na mifano iko tele. Kwa nini iwe tofauti katika ziwa Nyasa na kwa upande wa Tanzania tu wakati kwa upande wa Msumbiji mpaka upo katikati ya ziwa?
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa Mto Songwe, mpaka baina ya nchi zetu mbili upo katikati. Iweje hapa kanuni hiyo itambulike na kuheshimiwa lakini isiwe hivyo ziwani? Kama
nilivyoeleza awali, mwanzoni Mto Songwe wote ulikuwa umewekwa upande
wetu, lakini Tume ya Mipaka iliyoundwa mwaka 1898 ilifanya marekebisho
na kuweka mpaka katikati ya mto. Kama
nilivyokwishagusia kwenye ziwa hilo hilo la Nyasa kwa upande wa
Msumbiji mwaka 1954 mkataba wa mwaka 1891 ulioipa Malawi ziwa lote
ulirekebishwa na mpaka kuwekwa katikati. Kwa nini isifanyike hivyo hivyo kwa upande wa Tanzania? Hivi
hasa ni kipi ambacho wenzetu wa Msumbiji walichotuzidi na kustahili
kupata haki yao ya msingi ya kumiliki na kutumia maji ya Ziwa Nyasa
ambacho sisi Tanzania tumepungukiwa?
Ndugu Wananchi;
Maji ni zawadi ya Mwenyezi Mungu kwa wanadamu wake, waitumie kwa uhai na maendeleo yao. Iweje
leo, kwa watu wanaoishi pembeni mwa ziwa hilo hilo wengine wapewe na
wengine wanyimwe haki ya kulimiliki na kulitumia? Kwa nini wanyimwe haki
ya kunufaika na zawadi hiyo? Hivi kauli ya wakoloni waliokaa Berlin ya
kusema fulani apate na fulani asipate inatosha? Hivi kweli ni rahisi kiasi hicho?
Mpaka wa kwenye maji ni tofauti na ule wa nchi kavu. Huu una rasilimali ambayo huwezi kuamua kumnyima mwanadamu mwingine anayeishi pembeni yake kwa vile haina badala yake. Unapowaambia
watu wa Mbamba Bay, Liuli, Lituhi, Manda, Ngonga, Matema, Mwaya, Itungi
na wengineo waishio kando ya ziwa kuwa maji hayo si yao bali ni mali ya
Malawi hawakuelewi na watakushangaa sana. Watadhani umechanganyikiwa kwani tangu waumbwe wamekuwepo hapo wanamiliki na kutumia maji ya Ziwa. Unataka wafanyeje? Waende Malawi kuomba kibali cha kuyatumia? Wao
watakuuliza swali moja tu “hivi hao wenzao wanaoishi ng’ambo ya pili
wamewazidi nini katika ubinadamu wao hata wapewe maji yote na wao
wanyimwe?”
Ndugu Wananchi;
Kwa
maana halisi ya Mkataba wa Heligoland tangu tarehe 1 Julai, 1890,
wananchi wa upande wa Tanzania wamekuwa wanakunywa, kuoga, kuvua samaki
na kusafiri katika maji ya Ziwa yasiyokuwa yao bali ya nchi nyingine. Na
kwa kuwa wamekuwa wanafanya hivyo bila ya kupata kibali cha Malawi
wamekuwa wanaiba maji na samaki wa Malawi na kusafiri isivyo halali
katika nchi ya watu. Jambo hili haliingii akilini hata kidogo. Ndiyo maana tunadai haki yetu stahili.
Ndugu Wananchi;
Na hiyo pia, ndiyo maana, busara na hekima ya Sheria ya Kimataifa kuhusu mpaka wa kwenye maji kuwa katikati. Sheria
hii inazingatia hali halisi ya maisha ya jamii inayozunguka ziwa ambayo
imekuwa inalitegemea maisha yao yote kwa shughuli zao za kuwapatia uhai
na maendeleo yao. Haiwezekani kuwatenganisha watu waishio kando ya Ziwa Nyasa kumiliki na kutumia maji hayo na rasilimali zake. Hawataelewa wala kukubali kuambiwa kuwa wanatumia maji na rasilimali za ziwani kwa hisani ya nchi ya Malawi.
Kwa
watu waliokuwepo tangu Mungu anawaumba wao na wenzao wa ng’ambo ya
pili, siyo sawa na siyo haki hata kidogo kuwafanyia hivyo. Kwe kweli ni unyanyasaji wa hali ya juu. Ndiyo maana wazee wetu walidai suala hili liwekwe sawa wakati wa ukoloni, kabla na baada ya Uhuru. Na ndiyo maana na sisi tunafuata nyayo zao katika madai haya ya haki.
Ndugu Wananchi;
Kuna mambo mengine mawili ambayo yanatufanya tudai haki ya kumiliki na kutumia Ziwa Nyasa. La kwanza ni ule ukweli kwamba mito mingi ya Tanzania nayo inachangia kujaza maji katika ziwa. Iweje
leo maji yanayojaza ziwa ni jambo jema, lakini yakishaingia ziwani,
ziwa hilo si mali yao wenye mito hiyo tena na wakiyatumia wanaiba mali
ya watu wengine. Hivi
kweli ndivyo wanavyostahili kufanyiwa watu wanaotunza vyanzo vya mito
hiyo na kuruhusu maji yake kutiririka na kuingia ziwani?
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ni kwamba mpaka wa Tanzania na Malawi kuwa ufukweni kunafanya ukubwa wa nchi zetu kuwa haujulikani kwa uhakika. Unategemea mabadiliko kutokana na kujaa na kupungua kwa maji ziwani. Kunafanya mpaka wa nchi kuwa hautabiriki na unaweza kuwa tatizo siku moja mbele ya safari. Isitoshe kuwa na nchi isiyojulikana ukubwa wake nalo ni tatizo la aina yake. Ndiyo maana mpaka kuwa katikati ya ziwa ni bora zaidi.
Ndugu Wananchi;
Kama nilivyokwishasema, chimbuko la mzozo huu ni mkataba wa Heligoland ambao umepanda mbegu ya fitina baina ya nchi zetu. Bahati
mbaya sana Tume ya Mipaka haikumaliza kazi ya kuhakiki mipaka yote ya
nchi yetu na majirani zake kufuatia kuzuka kwa Vita Kuu ya Kwanza mwaka
1914. Ujerumani ikashindwa vita na koloni lake kuwa sehemu ya himaya ya Uingereza. Bahati
mbaya kwetu Waingereza waliotawala nchi zetu mbili tangu 1918
hawakuchukua hatua za kurekebisha mpaka kabla ya uhuru wa nchi zetu. Ni maoni yetu kuwa nchi zetu sasa zifanye kile ambacho hakikufanywa na Tume ya Mipaka ya wakoloni – Waingereza na Wajerumani. Tukifanye sisi wenyewe kama nchi mbili huru kwa njia ya mazungumzo.
Bahati mbaya majaribio ya mwaka 1967 hayakufanikiwa. Bahati nzuri kufuatia uamuzi wa kijasiri wa marehemu Rais Bingu wa Mutharika nchi zetu sasa zinazungumza. Bado hatujafikia muafaka kuhusu kurekebisha mpaka na huenda ikatuwia vigumu kufikia muafaka. Jambo linaloleta faraja, hata hivyo, ni kuwa sote wawili tumekubaliana kuwa tutafute mtu wa kutusuluhisha.
Ndugu Wananchi;
Hayo
ndiyo matokeo ya mazungumzo ya Tume yetu ya pamoja tangu ngazi ya
Wataalamu, Makatibu Wakuu mpaka kwa Mawaziri, katika vikao vya Mzuzu na
Lilongwe kati ya tarehe 20 – 27 Agosti, 2012. Katika
mkutano wao wa tarehe 27 Agosti, 2012 Mawaziri husika wa nchi zetu
chini ya uongozi wa pamoja wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi,
Mheshimiwa Ephraim Chiume na mwenzake wa Tanzania, Mheshimiwa Bernard
Membe, wameafiki mapendekezo hayo. Aidha,
wamekubaliana kuwa pande zote mbili wakutane tena Dar es Salaam kati ya
tarehe 10 – 15 Septemba, 2012 kukubaliana juu ya usuluhishi wa aina
gani unafaa.
Ndugu Wananchi;
Mtakubaliana nami kuwa tumepiga hatua muhimu kuelekea kwenye kupata ufumbuzi wa kudumu wa suala hili. Hata hivyo, bado safari ni ndefu na huenda ikawa na magumu mengi. Maombi yangu kwa viongozi na wananchi wa Tanzania na Malawi ni kuendelea kuunga mkono jitihada hizi. Tuwaunge mkono wataalamu na Mawaziri wetu ili wafanikishe vizuri jukumu lao. Tuzingatie
na kuheshimu walichokubaliana Lilongwe kuwa viongozi na wananchi wa
nchi zetu wajiepushe na kutoa kauli au kufanya vitendo vinavyoweza
kuchafua hali ya hewa, kuleta uchochezi na kuathiri majadiliano
yanayoendelea.
Nawasihi
Watanzania wenzangu kuzingatia ushauri na rai hiyo ya Mawaziri na
wataalamu wetu, ili kuwe na mazingira mazuri ya mazungumzo na kuwezesha
mzozo huu kuisha kwa amani na kirafiki.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Kabla
ya kumaliza hotuba yangu, napenda kusisitiza kuwa si makusudio yangu
wala ya Serikali yetu kutafuta suluhisho la suala hili kwa nguvu ya
kijeshi. Nawahakikishia
Watanzania wenzangu kuwa hatuko vitani na Malawi na wala hakuna
maandalizi ya vita dhidi ya jirani zetu hawa kwa sababu ya mzozo wetu wa
mpaka katika Ziwa. Ondoeni hofu na endeleeni na shughuli zenu za ujenzi wa taifa letu kama kawaida.
Nilimhakikishia hivyo Rais wa Malawi, Mheshimiwa Joyce Banda nilipokutana naye Maputo, Msumbiji tarehe 18 Agosti, 2012. Tanzania haina mpango wa kuingia vitani na Malawi. Mimi
na wenzangu Serikalini tunaona kuwa fursa tuliyoitafuta miaka mingi ya
kukaa na ndugu zetu Malawi kuzungumzia suala hili lenye maslahi kwetu
sote sasa tumeipata. Hatuna budi kuitumia ipasavyo. Naamini,
tukifanya hivyo, inaweza kutufikisha pale tunapopataka. Ni muhimu, kwa
ajili hiyo kwa pande zetu mbili, kuipa fursa ya mazungumzo nafasi ya
kuendelea bila ya vikwazo visivyokuwa vya lazima.
Ndugu Wananchi;
Kwa
sababu hiyo basi, napenda kutumia nafasi hii kuwasihi ndugu zetu wa
vyombo vya habari na wanasiasa wenzangu tuepuke kauli au matendo
yatakayovuruga mazungumzo na kuchochea uhasama kati ya nchi zetu mbili
jirani na rafiki. Kuna manufaa makubwa ya kumaliza mzozo wetu kwa njia ya mazungumzo kuliko kwa njia ya vita. Kufikiria sasa kutumia njia nyinginezo hasa za nguvu za kujeshi, si wakati wake muafaka. Aidha, tukitumia njia ya vita, badala ya kuwa tumepata suluhisho inaweza kuwa ndiyo mwanzo wa mgogoro mpana zaidi. Tuendelee kuwaunga mkono wawakilishi wetu katika Tume yetu ya pamoja. Naahidi, Serikali itakuwa inawapa taarifa kadri mazungumzo yetu na wenzetu wa Malawi yatakavyokuwa yanaendelea. Nina hakika tutamaliza salama.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!
Asanteni kwa Kunisikiliza
No comments:
Post a Comment