Mafunzo SC |
Na Ally Mohamed,
Zanzibar
PAZIA la Ligi
Kuu Zanzibar, limefunguliwa jana kwa mechi mbili kuchezwa katika viwanja viwili
tofauti, kwenye Uwanja wa Amaan kisiwani Unguja, Mabaharia wa KMKM walikutana
na Mafunzo, ambapo mechi hiyo imemalizika kwa Mafunzo kuchomoza na ushindi wa
bao 1-0, bao hilo pekee likipatikana katika dakika ya tano, mfungaji Mohammed
Abdulrahman.
Huko
kisiwani Pemba nako ilipigwa mechi moja ikiwakutanisha mabingwa watetezi wa
ligi hiyo, Super Falcon na Chipukizi ambapo kwa mara nyengine tena Super Falcon
ambao ni wawakilishi wa Zanzibar katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani,
wamefungwa 2-0.
Hii ni mechi
ya sita mfululizo Super Falcon wanapokea kipigo, wakianzia katika michuano ya
BancABC Super 8, ambapo walipoteza mechi zao zote 3 za hatua ya makundi, kabla
ya kukubali kipigo cha 3-1 kutoka kwa Jamhuri katika mechi ya Ngao ya Jamii
iliyochezwa Septemba 1, mwaka huu Uwanja wa Amaan na juzi wakicheza na Coastal
Union ya jijini Tanga katika mechi ya kirafiki, mchezo uliochezwa Uwanja wa
Ngome, Fuoni, Wilaya ya Magharibi, Unguja walifungwa 2-0.
Ligi hiyo
inatarajia kuendelea tena leo kwa mechi mbili, katika Uwanja wa Amaan kisiwani
unguja, Klabu ya Malindi ambao wamenunua daraja kutoka kwa Miembeni SC
watacheza na timu iliyopanda daraja msimu huu, Bandari na katika Uwanja wa
Gombani, kisiwani Pemba washindi wa pili wa ligi iliyopita, Jamhuri wakicheza
na Duma, mechi zota zinatarajiwa kuanza saa 10:30 jioni.
Ligi kuu ya
Zanzibar, ambayo msimu huu inafahamika kwa jina la Zanzibar Grand Malt Premier
League kutokana na mdhamini kinywaji cha Grand Malt, inashirikisha timu 12,
huku timu 8 zikitoka kisiwani Unguja na timu 4 zikitoka kisiwani Pemba, timu
zinazotoka kisiwani Unguja ni Bandari,
Chuoni, KMKM, Mafunzo, Malindi, Mundu ambao wamenunua daraja kutoka kwa Miembeni
United, Mtende iliyopanda daraja msimu huu na Zimamoto.
Kwa upande
wa kisiwani Pemba ni Chipukizi, Duma, Jamhuri na Mabinwa watetezi, Super
Falcon.
No comments:
Post a Comment