Marehemu Meja jenerali Kamazima enzi za uhai wake.
Rais
Jakaya Mrisho Kikwete akiweka saini katika kitabu cha maombolezo
nyumbani kwa Marehemu Meja jenerali Kamazima Tegeta, Dar es salaam, leo.
TAARIFA KWA UMMA
Rais
Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za pole Mkuu wa Majeshi Jenerali
Davis Mwamunyange kufuatia kifo cha Meja Jenerali Anatory Ruta Kamazima
(Mstaafu) aliyefariki jana tarehe 25 Septemba, 2012 katika hospitali ya
Taifa ya Muhimbili. “Nimepokea kwa mshituko na huzuni nyingi habari za
kifo cha Meja Jenerali Kamazima, ni pigo kubwa sana kwa Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Taifa kwa ujumla” Rais amesema katika
salamu hizo.
Mchana wa
leo Rais ameitembelea familia ya marehemu nyumbani kwao Tegeta
kuwafariji wafiwa. Marehemu alizaliwa mwaka 1946 katika kijiji cha
Maruku, Mkoani Kagera. Alijiunga na Jeshi mwaka 1967, mara baada ya
kuhitimu Chuo Kikuu mwaka 1966.
Marehemu
Kamazima amesoma kozi mbalimbali za kijeshi hapa nchini na nchi za
China, India, Uingereza na Misri na kulitumikia Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) katika ngazi mbalimbali ambapo mwaka 1989, aliteuliwa
kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Kuzuia Rushwa Tanzania, hadi alipostaafu
Juni 2003.
Rais
amemuelezea marehemu Kamazima kama mzalendo na mtu aliyeipenda na
kuitumikia nchi yake kwa weledi mkubwa, uaminifu na moyo
mmoja. “Nimemfahamu Marehemu kwa miaka yote ya utumishi wake jeshini na
serikalini kama mzalendo, muaminifu na mwenye moyo wa kulinda nchi yake
wakati wote” amesema “Marehemu Kamazima alikua mtu wa kutumainiwa sana
katika nchi yetu na kamwe hatutamsahau kwa utumishi wake uliotukuka”.
“Tutamkumbuka
na kumuenzi siku zote, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa yote na
tunamuombea mapumziko mema Marehemu Kamazima. Amina”. Rais ameongeza.
Marehemu ameacha mjane, watoto na wajukuu.
Imetolewa na:
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Ikulu.
DAR ES SALAAM
26 Septemba, 2012
No comments:
Post a Comment