Rais
Dr.Jakaya Mrisho Kikwete na mwenyeji wake Sultani wa Oman Qaboos bin
Said Al Said wakipokea heshima za viongozi muda muda mfupi baada ya Rais
Kikwete kuwasili jijini Muscat Oman leo mchana kwa ziara rasmi(State
Visit) ya siku tatu nchini Oman.
Rais
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na mwenyeji wake Sultani wa Oman
Qaboos bin Said Al Said katika kasri la Sultani jijini Muscat leo(Picha
na Freddy Maro)
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
(pichani) anaanza ziara rasmi ya Kiserikali ya siku nne katika Taifa la
Kifalme la Oman, ikiwa ni ziara ya kwanza ya Kiserikali kufanywa na Rais
wa Tanzania katika nchi hiyo.
Rais
Kikwete na ujumbe wake ameondoka mjini Dar es Salaam asubuhi ya leo,
Jumatatu, Oktoba 15, 2012, kwenda Oman kuanza ziara hiyo inayofanyika
kwa mwaliko wa Kiongozi wa Ufalme wa Oman, Mfalme Qaboos bin Said,
ambaye atakuwa mwenyeji wake kwa siku zote nne.
Kwenye
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Muscat, Rais Kikwete anatarajiwa
kulakiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Mheshimiwa Yousef bin
Abdullah bin Alawi ambaye ataandamana naye hadi Jumba la Muscat Gate
ambako Rais atapokelewa na Mfalme Qaboos. Kutoka hapo wataandamana hadi
Kasri ya Kifalme ya Al Alam ambako atapokelewa rasmi kwa heshima zote za
Kiserikali.
Shughuli
kubwa ya jioni ya leo ya Mheshimiwa Rais itakuwa ni kufanya mazungumzo
rasmi ya Kiserikali kati ya Serikali za Tanzania na Ufalme wa Oman na
pia kuhudhuria dhifa rasmi ambayo Mfalme Qaboos atamwandalia mgeni wake
kwenye Kasri ya Al Alam.
Kesho,
Jumanne, Oktoba 16, 2012, Rais Kikwete atatembelea Jumba la Makumbusho
la Majeshi ya Ulinzi ya Oman, atafungua Mkutano wa Wafanyabiashara wa
Tanzania na Oman, atashuhudia utiaji saini makubaliano ya mikataba
miwili kati ya nchi hizo mbili, ukiwamo ule wa kuundwa kwa Baraza la
Biashara la Tanzania na Oman na ule wa Kuendeleza na Kulinda Uwekezaji
katika nchi hizo mbili.
Jioni, Rais Kikwete atatunukiwa nishani ya juu kabisa ambayo Ufalme wa Oman hutoa kwa viongozi wa nchi za nje ya First Order Medal kwenye Chakula Maalum cha Usiku kitakachoandaliwa na Mfalme Qaboos kwa heshima ya Rais Kikwete.
Rais
Kikwete na ujumbe wake pia utakutana na kuzungumza na Watanzania
wanaoishi Oman katika mkutano utakaofanyika kwenye Hoteli ya Kifalme ya
Al Bustan.
Hii
itakuwa mara ya pili kwa Mheshimiwa Kikwete kutembelea Oman.
Aliitembelea nchi hiyo mara ya kwanza mwaka 1998, wakati huo akiwa ni
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
15 Oktoba, 2012
hyo omni ilikuwaga mkoa wa bongo tu
ReplyDelete