Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Sunday, October 7, 2012

Vita ya Sumaye, Lowassa leo



              vs       

WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, leo
anatarajia kufanya kile alichoahidi mara baada ya
kuangushwa na Dk. Mary Nagu katika uchaguzi wa
kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC)
ya CCM, kupitia Wilaya ya Hanang. Habari kutoka kwa watu wa karibu na Sumaye,
zilisema kuwa Waziri Mkuu huyo wa zamani
anatarajia kuzungumza na vyombo vya habari
katika Hoteli ya Court Yard jijini Dar es Salaam leo,
kuanzia majira ya saa sita mchana. Kwa mujibu wa habari hizo, Sumaye amepanga
kueleza mwenendo mzima wa uchaguzi huo na
jinsi Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa
alivyoingiza mkono na kusababisha aangukie pua. Alipoulizwa nini hasa anataka kusema, Sumaye
alisema: “Ukiweza kuja, utasikia mwenyewe
nitakachozungumza.” Ingawa hakuna aliyeweza kutoboa siri ya nini
Sumaye anataka kuwaeleza Watanzania, lakini ni
dhahiri kwamba ameamua kujifunga bomu na
kujilipua kwa kueleza kile anachoamini njama za
kummaliza kisiasa anazodai kufanyiwa na
Lowassa. Siku chache zilizopita mara baada ya kushindwa
kwenye uchaguzi wa NEC, Sumaye alimtangazia
vita Lowassa. Sumaye ambaye hajatangaza rasmi kuwania kiti
cha urais, anatarajiwa kupasua jipu leo kueleza
kilichotokea Hanang na msimamo wake, na
kwamba yuko tayari kuwania urais mwaka 2015
endapo Lowassa atajitosa. Sumaye aliangushwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Nagu,
katika kuwania nafasi ya ujumbe wa NEC wilaya ya
Hanang, matokeo ambayo anaamini yana mkono
wa Lowassa. Pamoja na Sumaye kushindwa na Dk. Nagu kwa
zaidi ya kura 167, amepokea matokeo hayo kwa
shingo upande kwa kile alichoeleza kuwa ushindi
huo ni wa mafisadi. Inaelezwa kwamba tayari mwanasiasa huyo
amefanya mazungumzo na baadhi ya wanasiasa
wenye ushawishi wanaojipambanua kama
wapiganaji wa ufisadi ili kuunganisha nguvu kwa
ajili ya kukabiliana na kambi ya Lowassa. Mbali ya kundi la Sumaye na wanasiasa wengine
kuanza mkakati huo, wapo pia wanasiasa wenye
majina makubwa ndani ya chama, serikali na
wastaafu wanaotajwa kuingia kwenye muungano
huo. Akijibu tuhuma hizo kwa kifupi, Lowassa alisema
endapo Sumaye ataitisha mkutano na waandishi
wa habari na kutoa tuhuma hizo, nitajibu. Hata hivyo, baadhi ya wafuasi wa Sumaye na
watendaji wa ndani ya serikali wamesema
kuanguka kwa mwanasiasa huyo mkongwe katika
uchaguzi wa wilaya kunamuweka vizuri zaidi
kisiasa kutokana na mazingira tete ya kisiasa ndani
ya CCM, chama ambacho kimechokwa na umma. Uchaguzi huo ulifanyika siku chache baada ya CCM
kupitisha majina ya walioomba nafasi hizo huku
wanachama wengi wakienguliwa kutokana na
kukosa sifa katika kikao kilichomalizika mjini
Dodoma hivi karibuni. Wakati Sumaye akijipanga kupasua jipu leo, CCM
kwa upande wake inasubiri kwa hamu kumsikia
atakachosema. Tangu Sumaye alipodokeza kwamba atazungumza
na waandishi na kupasua jipu, baadhi ya viongozi
wa CCM wamekuwa wakifuatilia kwa makini siku
atakayozungumza na waandishi. Sumaye na Lowassa wanatajwa kuwa miongoni
mwa makada wanaofikiria kutaka kuwania urais
mwaka 2015.
Source:tanzania daima

No comments:

Post a Comment