Matajiri
wawili wakubwa duniani jana, Jumanne, Oktoba 2, 2012, wameichangia
Tanzania kiasi cha sh. bilioni 24.1 (sawa na dola za Marekani milioni
15.5) kwa ajili ya kuendeleza afya ya akinamama na kusaidia uzazi salama
hasa katika maeneo ya vijijini.
Matajiri
hao, Mheshimiwa Michael Bloomberg ambaye ni Meya wa Jiji la New York,
Marekani na Mama Helen Agerup wa Sweden, wametangaza mchango wao huo
mkubwa kwa Tanzania kwenye mkutano maalum wa waandishi wa habari
uliofanyika kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York,
Marekani.
Pamoja na
matajiri hao kwenye mkutano huo wa waandishi wa habari walikuwa ni Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Ban Ki Moon.
Kati ya
fedha hizo, Meya Bloomberg wa Jiji la New York lenye wakazi milioni 8.4,
anatoa kiasi cha dola za Marekani milioni nane kupitia Taasisi yake ya
Bloomberg Philanthropies wakati Mama Agerup anatoa kiasi cha dola
milioni 7.5 kupitia taasisi yake na mumewe ya H&B Agerup Foundation.
Meja
Bloomberg amekuwa anasaidia afya ya akinamama na juhudi za uzazi salama
katika maeneo ya vijijini katika Tanzania tokea mwaka 2006 wakati hii
itakuwa mara ya kwanza kwa Taasisi ya H&B kuungana na Bloomberg
Philanthropies kusaidia sekta ya afya katika Tanzania.
Akizungumza
kwenye shughuli hiyo muhimu, Meya Bloomberg amesema kuwa yeye na
taasisi yake wameamua kuendelea kuunga mkono jithada za Tanzania katika
kuinua afya ya akinamama na kupunguza vifo vya uzazi kwa sababu ya
matokeo mazuri ambayo yamepatikana tokea Bloomberg Philanthropies ianze
kuunga mkono jitihada hizo za Serikali mwaka 2006.
Amesema
kuwa taasisi yake inajihusisha katika maeneo mawili makubwa. Eneo moja
ni kujenga na kukarabati vituo vya afya na zahanati katika maeneo ya
vijijini na pili ni kutoa mafunzo kwa watu wasiokuwa watalaam wa afya
pamoja na wakunga kuweza kusaidia uzazi salama vijijini. Mpaka sasa
taasisi hiyo imefundisha kiasi cha watu 106 kuweza kufanya kazi ya uzazi
salama na ukunga chini ya msaada wake kwa Tanzania.
“Tunaona
matokeo ya kuvutia sana. Hata kama idadi ya akinamama wanaopoteza
maisha haijawa ya chini –akinamama 13 kati ya 1,000- kama ile ya
Marekani lakini dhahiri kuwa idadi inapungua kwa kiasi cha kutia moyo”.
Ameongeza Meja Bloomberg: “Zaidi
tunaifanya kazi hii katika Tanzania kwa sababu tunashughulika na Rais
Kikwete, kiongozi mbunifu, kiongozi mkweli na muadilifu, kiongozi
mchapakazi na anayetaka kuonyesha tofauti katika maisha ya wananchi
wake.”
Naye Mama
Helen Agerup amesema kuwa alitembelea Tanzania mwaka jana baada ya
kushawishiwa na binti yake ambaye alikuwa ametembelea Tanzania mapema na
kuvutiwa na jitihada za Serikali na zile za Taasisi ya Bloomberg kuhusu
afya ya akinamama.
“Nilivutiwa
sana na kazi inayofanywa na Serikali ya Tanzania na Taasisi ya
Bloomberg kuzuia vifo vinavyosababishwa na mambo yanayoweza kuzuilika
yaani kutokwa damu kupita kiasi na magonjwa ya kuambukiza kutokana hasa
na tatizo la ukimwi,” amesema mama huyo.
Naye Rais
Kikwete ameshukuru sana Meya Bloomberg na Mama Agerup akisema kuwa
misaada yao inaleta tofauti kubwa katika afya za akinamama katika
Tanzania.
“Katika
nchi ambako uwiano wa daktari mmoja na wagonjwa ni daktari mmoja kwa
wagonjwa 30,000 na mganga mmoja kwa wagonjwa 23,000 na ambako akinamama
waja wazito wanatembea zaidi ya kilomita tano kwenye uchungu, misaada ya
namna hii ni muhimu sana kwa nchi yetu. Tunawashukuru sana.”
Amesema
kuwa umuhimu wa kuboresha afya ya akinamama ni moja ya maeneo ya
kipaumbele cha Serikali na hali hiyo itaendelea mpaka tatizo la vifo vya
uzazi litakapopungua sana.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
3 Oktoba, 2012
No comments:
Post a Comment