Ibrahim Haruna Lipumba -Mwenyekiti Chama Cha Wananchi CUF
----
Siku ya Alhamis nikielekea Muhimbili
kumpeleka shangazi yangu hospitali nilipata taarifa kuwa Imam wa
msikiti wa Masjid Haq (ulioko jirani na Afisi Kuu ya CUF na ambapo
nasali sala ya Ijumaa nikiwa Afisi Kuu) na watu wengine watatu akiwemo
Sheikh Ramadhan S. Sanze (ambaye namfahamu kwa muda mrefu). Sadik Gogo
na Mzee Abdillah wamekamatwa na wamefikishwa kituo cha polisi cha kati
(Central Police Station). Nilistushwa na kamata kamata hii na nikahofia
kuwa inaweza kuongeza jazba miongoni mwa waumini wa Kiislam. Baada ya
shangazi kupata tiba katika hospitali ya Muhimbili nilimrudisha nyumbani
na nikampigia simu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na mahusiano ya umma,
Abdul Kambaya, tukutane kituo cha polisi cha kati kuulizia sababu za
kukamatwa Imam wa Masjid Haq na wenzake watatu na kama tunaweza
kuwawekea dhamana.
Tulipofika
kituo cha polisi tulibaini kuwa Imam wa Msikiti wa Masjid Haq
hajakamatwa bali kuna muumini mwingine kwa jina la Mkadam Swalehe ndiye
aliyekamatwa. Tulizungumza na RPC Kova na RCO Msangi kuhusu kuachiliwa
kwa wale waliokamatwa. Tukafahamishwa kuwa itabidi wafanyiwe mahojiano
na baadaye wataachiliwa isipokuwa Mkadam Swalehe ambaye ana faili
jingine pale polisi linaloendelea kufanyiwa upelelezi. Tulifahamishwa
kuwa nitume mtu saa 10:30 jioni ili aweze kufuatilia utaratibu wa
kuachiliwa watuhumiwa watatu akiwemo Sheikh Ramadhan Sanze, Sadik Gogo
na Mzee Abdillah.
Nilishauriana
na Wakurugenzi wa CUF walioko Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu,
Julius Mtatiro hatua za kuchukua. Taarifa za kukamatwa Sheikh Ramadhan
Sanze na wenzake zilikuwa zinaenea na kupandisha jazba ya Waislam wengi.
Tulipata wasiwasi kuwa jazba hii inaweza kupelekea Waislam wengi
kuandamana baada ya sala ya Ijumaa. Ikiwa Sheikh Ramadhan Sanze na
wenzake wataachiwa na Waislam wakapata taarifa hiyo inaweza kusaidia
kupunguza jazba na watu wasishiriki maandamano baada ya sala ya Ijumaa.
Nilimpa
jukum Abdul Kambaya afuatilie Central PoliceStation, suala la
kuachiliwa Sheikh Sanze na wenzake. Niliwasiliana naye kwa simu na
kuzungumza na RCO na nikaamini kuwa Sheikh Ramadhan Sanze, Sadik Gogo na
Mzee Abdillah wataachiwa baada ya kukamilisha mahojiano. Ilikuwa
inakaribia saa 12 jioni. Muda wa kuitisha Press Conference haukuwepo.
Tukakubaliana
Naibu Katibu Mkuu awasiliane na wahariri wa habari wa vituo vya
televisheni Channel 10, TBC1, Star TV, Mlimani TV na ITV ili niweze
kutoa taarifa ya kuwasihi Waislam warudi majumbani na kwenye shughuli
zao baada ya sala ya Ijumaa.
Niliweza
kufanya mahojiano na Channel 10, TBC1, na ITV. Kwa bahati mbaya Camera
person wa Star TV alikuwa kwenye shughuli nyingine na kwa hiyo sikuweza
kufanya mahojiano na Star TV. Vilevile wapiga picha wa Mlimani TV
hawakuwepo kwenye studio. Pia nilipata bahati ya kuzungumza na Radio
Iman inayosikilizwa na Waislam wengi na kueleza maoni yangu kuwa Waislam
wasiandamane baada ya sala ya Ijumaa.
Baada
ya kutoa taarifa kwenye vituo vitatu vya televisheni na Radio Iman kuwa
Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake wataachiliwa na kuwasihi Waislam
wasishiriki maandamano baada ya sala ya Ijumaa nilimpigia simu Abdul
Kambaya kuulizia kama naweza kuzungumza na Sheikh Ramadhan Sanze.
Kambaya akanieleza mambo yamebadilika na hawajaachiwa. Niliwasiliana na
RCO na nikabaini kuwa suala hilo haliko tena chini ya uamuzi wake na
litakamilishwa siku ijayo.
Usiku
wa alhamisi kuamkia Ijumaa nilijaribu kuwasiliana na Rais Kikwete
kupitia wasaidizi wake ili nimfahamishe mantiki na sababu ya hatua
nilizochukua na atumie uwezo wake alionao Sheikh Ramadhan Sanze na
wenzake waachiliwe. Kwa bahati msaidizi mmoja alipata ujumbe wangu wa
simu na akanipigia simu saa 6:50 usiku na kunifahamisha atajitahidi
kuufikisha ujumbe wangu kwa Mhe. Rais ili nipate kuongea naye kuhusu
jamaa wanaoshikiliwa na polisi waachiwe ili kupunguza jazba na kuepusha
shari. Niliyezungumza naye alikuwa Dodoma na Rais alikuwa Arusha na
ratiba yake ilikuwa imebana sana na kwa hiyo hakuweza kupata fursa ya
kunipigia simu siku hiyo ya Ijumaa.
Siku
ya Ijumaa Abdul Kambaya aliendelea kufuatilia kuachiwa kwa Sheikh
Ramadhan Sanze na wenzake Central Police Station. Nami katika kuhangaika
ili waliokamatwa waachiliwe nilipata fursa ya kuzungumza na IGP na
kumfahamisha sababu ya juhudi nilizochukua na mategemeo yangu kuwa
Sheikh Sanze na wenzake wangeachiwa. Ninakiri kuwa katika mazungumzo ya
simu, IGP Mwema alikuwa msikivu na mkarimu sana katika kauli yake.
Alinishukuru kwa kauli niliyoitoa katika vituo vya televisheni na kuwa
atafuatilia suala nililomueleza. Hatimaye Sheikh Ramadhan Sanze na
wenzake waliachiwa.
Naamini
kama Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake wangeachiwa ingesaidia sana
kupunguza jazba. Hata hivyo Waislam wengi na wananchi wengine kwa ujumla
walipokea vizuri wito wangu na hawakushiriki katika maandamano. Baadhi
wamenikosoa na kushauri kuwa ilifaa nisubiri mpaka baada ya maandamano
kufanyika na kama patatokea majeruhi na vifo ndipo nitoe tamko la
kulaani vitendo vya polisi na serikali.
Katika
mitandao ya kijamii wengine wamekejeli juhudi zangu. Nilikubali
kushiriki katika kipindi cha Makutano show kinachoendeshwa na Bi. Fina
ambapo hupata maswali toka Jamii Forum. Moja ya swali lililotolewa ni
“Muulize very very solid, kuna agenda gani kati ya Cuf na uislam? mtaani
leo wanasema kauli ya Lipumba ya jana kusitisha maandamano wameitii, na
ukiangalia mikutano yake pale jangwani utafikiri kuna mawaidha ni
balaghashia na baibui.” Fina hakupata muda wa kuniuliza swali hili. Jibu
lake ni la wazi.
CUF
inasimamia Haki Sawa kwa Wananchi Wote. Kuna Watanzania wengi ambao ni
Waislam na wao pia wanastahiki kutendewa haki katika nchi yao. Kuhusu
balaghashia na baibui ni vyema vijana wakatazama picha za umati wa watu
uliokuwa unahutubiwa na Mwalimu Nyerere wakati wa kupigania uhuru wa
nchi hii. Picha hizo pia zinaonyesha waliokuwa wakipigania uhuru wengi
walivaa balaghashia na baibui hata Mwalimu Nyerere alipewa zawadi nyingi
za balaghashia na akaamua kuzivaa.
Kushamiri
kwa demokrasia ya kweli msingi wake mkubwa ni amani na utulivu. Amani
ya kweli haipatikani bila kuwepo haki. Kesi ya Sheikh Ponda msingi wake
na madai ya kiwanja. Ki msingi kesi ya madai ya kusuluhishwa na Mahakama
ya ardhi. Sheikh Ponda ana haki ya msingi ya kupewa dhamana hata kama
kauli zake haziifurahishi serikali.
Nasikitika
sana katika kipindi hiki tete, viongozi wa serikali wameshindwa
kuchukua juhudi za makusudi kuzungumza na Maimam wa misikiti na viongozi
wa asasi za Kiislam kupunguza jazba. Badala yake wameachia kauli za
vitisho vya Kamanda Kova ndiyo viwe mawasiliano kati ya serikali na
Waislam. Ni vyema serikali ikatumia busara na kuwasiliana na Maimamu wa
misikiti na viongozi wa asasi za Kiislam kuelewa hoja na malalamiko yao.
Hatimaye
nimepata fursa ya kuzungumza na Mheshimiwa Rais leo asubuhi na
nikamueleza juhudi nilizozichukua kuweza kupunguza jazba na kuwaomba
Waislam wasishiriki kwenye maandamano baada ya sala ya Ijumaa. Ni wazi
hali hii ya mtafaruku ndani ya jamii inamsononesha sana Mheshimiwa Rais
na ninaamini atajitahidi kwa uwezo wake wote kutafuta suluhisho.
Katika
kutafuta suluhu ya mtafaruku huu nitaendelea na jitihada za kutafuta
fursa niweze kubadilishana mawazo na Rais Kikwete. Nitazungumza na
viongozi wa asasi za Kiislam. Nitazungumza na viongozi wa Makanisa ya
Kikristo. Madhumuni ya mazungumzo yangu ni kuwafahamisha mantiki ya
juhudi nilizofanya na kushauriana misingi muhimu ya Waumini wote
kuheshimiana na kuvumiliana ili tujenge Tanzania yenye haki sawa kwa
wote.
Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti
Novemba 4 2012
Mwenyekiti
Novemba 4 2012
No comments:
Post a Comment