KESI ya msanii wa fani ya filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu, imeendelea kupigwa kalenda kutokana na upelelezi wake kutokukamilika.Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji ya msanii mwenzake, Steven Kanumba, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akidaiwa kutenda kosa hilo nyumbani kwa marehemu Aprili 7, mwaka huu.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Agustina Mmbando, jana ilitajwa mahakamani hapo lakini kwa mara nyingine upande wa mashtaka uliendelea kudai kuwa upelelezi haujakamilika.Wakati kesi hiyo ilipotajwa Novemba 5, mwaka huu kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilisha ili hatua nyingine ziweze kufuata, Wakili wa Serikali, Seth Sekwao alidai upelelezi haujakamilika.
Kutokana na taarifa hiyo ya upande wa mashtaka, mmoja wa mawakili wanaomtetea mshtakiwa, Peter Kibatala alitaka kuharakisha upelelezi wa kesi hiyo, ili iweze kusonga mbele.
Wakili Kibatala, ambaye pia ni Makamu Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alidai kila mara upande wa mashtaka umekuwa ukidai upelelezi haujakamilika, jambo ambalo linaifanya kesi hiyo ishindwe kuendelea katika hatua nyingine.
“Ni muda mrefu sasa, kesi hii imekuwa ikitajwa mara kwa mara upande wa mashtaka umekuwa ukidai upelelezi haujakamilika. Hivyo tunawakumbusha upande wa mashtaka ujitahidi kuharakisha upelelezi ili iweze kusonga mbele,” alidai Wakili Kibatala.
Upande wa mashtaka uliiomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Mmbando aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 3, mwaka huu itakapotajwa tena kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika.Lulu alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Aprili 11, mwaka huu na kusomewa shtaka moja la mauaji ya msanii mwenzake, Kanumba.
Akimsomea shtaka hilo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Elizabeth Kaganda alidai Aprili 7, mwaka huu eneo la Sinza Vatcan alimuua msanii, Steven Kanumba.
No comments:
Post a Comment