Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, December 12, 2012

SENENE ZALETA KIZAA ZAA IRINGA, WALIMU WADAIWA KUTOA ADHABU YA KUKUSANYA SENENE KWA WANAFUNZI


wanafunzi  wa shule za msingi mjini Iringa wakienda shule na senene
Gari lenye namba za usajili T 356 BXK likiwa limebeba senene  kupeleka sokoni Iringa  kuuza
Kijana akiwa amebeba magunia ya Senene katika mkokoteni akielekea kusaka  wateja
Senene  wakiwa wamezagaa katika  jengo la Asas
Mvua  kubwa  iliyonyesha usiku  wa kuamkia leo   katika  mji  wa Iringa  imeshusha neema kwa wakazi wa  mji wa Iringa ambao ni wapenzi  wa  Senene  baada ya  baadhi ya  wamiliki wa nyumba  kudaiwa  kuwazuia wapangaji  wao  kuokota  senene katika nyumba  zao huku walimu pamoja na watumishi  wa umma  wakichelewa  kuingia makazini kutokana na zoezi la  kuokota  senene hao.

Uchunguzi  uliofanywa na mwandishi  wa habari hizi katika  shule mbali mbali  za Manispaa ya Iringa asubuhi ya jana umebaini  kuwa idadi kubwa ya  wanafunzi na  walimu  wao  walionekana katika maeneo ya shule  hizo   wakikusanya  senene  huku baadhi ya  wazazi  wakilalamikia baadhi ya  walimu  kuwapa adhabu  ya  kukamata  senene kwa wanafunzi  waliochelewa  kufika shule.

Mmoja kati ya  wazazi ambaye alijitambulisha kwa  jina la Jackson Ndelwa alisema  kuwa anashangazwa na utaratibu  wa  walimu  wa  shule  mbali mbali za msingi katika Manispaa ya Iringa  kuwaacha  wanafunzi  wakiendelea  kukamata  senene katika maeneo ya  shule hadi mida ya saa 4 asubuhi  wakati kwa kawaida muda huo wanafunzi  wanapaswa  kuwa madarasani .

Hivyo  aliuomba  uongozi  wa  elimu  katika Manispaa ya Iringa  kufuatilia mahudhurio ya  wanafunzi na  walimu  wao kwa  siku ya jana na iwapo itabainika kuwa wanafunzi  hawakuingia madarasani kwa ajili ya  kufanya shughuli za kukamata  senene  za walimu  basi  walimu  waliohusika kuwapa wanafunzi adhabu ya  kukamata  senene  wakati wa mvua  kuchukuliwa hatua kali.

Mmoja kati ya  walimu  wa  shule  za msingi mjini Iringa ambae aliomba  jina lake na  shule  yake  kuhifadhiwa kwa  kuwa  si msemaji  wa walimu  mjini Iringa alisema  kuwa madai ya  wazazi kuhusu  wanafunzi  kutumwa na  walimu  wao wa madarasa  kuokota  senene ni ya kweli na  kuwa badhi ya  walimu na  wanafunzi kwa muda wa asubuhi  walikuwa  wakishindana  kufukuza  senene kama  kitoweo .

Pia  alisema  kwa  siku ya jana hata adhabu  za kawaida  ambazo walimu  wamekuwa  wakizitoa kwa  wanafunzi wanaochelewa  kama adhabu ya  viboko haikuwepo na badala yake  wanafunzi  waliochelewa  walikuwa  wakipewa adhabu  ya  kukusanya  senene kwa ajili ya kitoweo cha walimu na sehemu ya senene  wanafunzi wamekuwa  wakipewa .

Wakati   wazazi wa  wanafunzi hao  wakilalamikia  hatua ya walimu  wa shule za msingi  kuwatumia wanafunzi katika   kuokota senene kwa  upande  wao  baadhi ya  wamiliki  wa  nyumba katika mji wa Iringa wamedaiwa  kuwanyanyasa   wapangaji  wao kwa  kuwazuia  kuokota  senene  zinazoanguka katika  nyumba  zao  kwa madai  kuwa senene  hizo ni mali ya mwenye nyumba na iwapo  wanataka  basi kutoka  nje ya uzio wa nyumba  hizo usiku kwenda kusaka senene mitaani . 

Mbali ya  wanafunzi hao  na  baadhi ya wamiliki  wa nyumba mjini Iringa kuonyesha  kugombea senene  hao badhi ya  wananchi  wameweza kunufaika  zaidi ya senene hao kwa  kuokota magunia kwa magunia ya  senene na  kuwauza kati ya shilingi  35,000 hadi 50,000 huku  walinzi wa maeneo mbali mbali ya biashara  mjini hapa  wakiacha malindo  yao na kukusanyika eneo la jengo la mfanyabiashara Salim Abri Asas kukusanya senene hadi mida ya saa 7 mchana  kutokana na eneo hilo kuwekwa taa zenye mwanga mkali  zaidi.

No comments:

Post a Comment