Makamu wa rais nchini Venezuela Nicolas Maduro ameapishwa kuwa rais wa muda wanchi hiyo, muda mfupi baada ya maziko ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Hugo Chavez, katika ibada iliyofanyika katika Chuo cha Kijeshi mjini Caracas.
Hata hivyo, upande wa upinzani umesema kuapishwa kwa Maduro kumekiuka katiba, ambayo inasema ni spika wa bunge aliestahili kukaimu urais.
Maduro ameitaka tume ya uchaguzi kuitisha uchaguzi mpya haraka na kuwatahadharisha wapinzani dhidi ya kuususia.
Viongozi kadhaa wa dunia walihudhuria msiba wa Chavez, wakiwemo marais wa Iran, Mahmoud Ahmadnejad na Raul Castro wa Cuba.
 Maelfu ya waombolezaji pia walijipanga katika mitaa nje ya chuo cha kijeshi kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi wao wa miaka 14.
Chavez alifariki siku ya Jumanne akiwa na umri wa miaka 58, baada ya kuungua ugonjwa wa saratani kwa miaka miwili.