Mjumbe wa
Kamati Kuu ya Chadema, Mabele Marando akizungumza na waandishi wa
habari Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam leo juu ya
matukio makubwa yaliyotokea nchini Tanzania yakiwemo yale ya kuchomwa
kwa makanisa, maandamano ya wafuasi wa dini ya Kiislamu pamoja na tukio
la kutoweka kwa Sheikh Farid wa Zanzibar ambaye kwa sasa amepatikana
akiwa hai.
CHAMA
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeibua siri nzito ya mtandao wa
mawasiliano ya watu 10 wakiwamo vigogo wa Serikali, wanaodaiwa kupanga
njama za vitendo vya ugaidi, kuteka watu, kujeruhi, kuua na kuchafua
chama hicho.
Kutokana
na kupatikana mtandao huo, chama hicho kimesema kitawasilisha ombi
maalum la kuomba amri ya mahakama, kuziagiza kampuni za simu za mkononi
kuvipatia vyombo vya sheria taarifa za watu hao ili haki itendeke pamoja
na jamii ijue ukweli wa mambo hayo.
Akizungumza na waandishi wa
habari mjini Dar es Salaam jana, mwanasheria mwandamizi wa chama hicho,
Mabere Marando alisema haikuwa kazi nyepesi kupata mawasiliano na
nyaraka za watu hao, ambazo zina ushahidi wa kutosha, huku nyingine
zikionyesha vikao vilivyokuwa vikifanyika katika hoteli mbalimbali mjini
Dar es Salaam.
Bila
kificho, Marando alitaja majina 10 ya vigogo hao na namba zao
(MTANZANIA tunazo) jinsi walivyokuwa wakiwasiliana kwa nyakati tofauti
na kutumiana fedha, huku wengine wakikutana katika Hoteli ya Sea Cliff
na Tamal.
Vigogo
hao, ni kutoka Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), Baraza la Mawaziri,
Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliokuwa wanachama wa Chadema na waandishi
wa habari.
Ukiwaacha
vigogo watano wa Idara ya Usalama wa Taifa na mawaziri, Marando
alimtaja Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba ambaye alionekana
kutumia simu tano tofauti za kiganjani, kuwasiliana na idara hiyo kwa
nyakati tofauti pamoja na mtoto wa kiongozi mkubwa nchini.
Mbali
ya vigogo hao, Marando alimtaja mmoja wa wafanyakazi wa Chadema, Saumu
Malungu aliyefukuzwa hivi karibuni baada ya kudaiwa alikuwa akifanya
mawasiliano ya mara kwa mara na Nchemba na maofisa wa Idara ya Usalama
wa Taifa.
“Kwa
kauli moja, chama kiliamua kumfukuza Malungu kutokana na kuwa na
mawasiliano na Nchemba na maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa, ambao
walikuwa wanampa kazi ya kuwarubuni vijana wa Chadema ili kutoa ushahidi
wa uongo juu ya video vya Lwakatare,” alisema Marando.
Alisema
namba za simu za Nchemba, zimebainika kuwasiliana na Ludovick
Rwezahula, ambaye ni mtuhumiwa namba mbili wa kesi ya ugaidi.
Alisema
namba hiyo, pia imeonekana wazi kuwa ilihusika kupanga mipango ya
kumteka aliyekuwa Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Steven
Ulimboka.
“Lakini
si hilo tu, tumebaini Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, Dennis
Msaky anayedai kutaka kutekwa na Lwakatare, ameonekana kuwa na
mawasiliano ya mara kadhaa na Ludovick hadi kukutana pamoja, Desemba
mwaka jana katika Hoteli ya Tamal iliyopo Mwenge na kufanya mazungumzo,
ambapo alipigwa picha wakinywa vinywaji.
Alisema
Machi 29, mwaka huu, Ofisa wa Usalama wa Taifa (jina tunalo),
alimrubuni Ofisa wa Usalama wa Chadema, Ahmed Sabula akimtaka wakutane
na wenzake katika hoteli ya Sea Cliff ambapo walifanya mkutano.
Katika
mkutano huo, walimshawishi Sabula kukubali kutumika kutoa taarifa za
Chadema makao makuu na mipango ya viongozi wa kitaifa na kumhakikishia
wangemlipa kitita cha Sh milioni 30 ndani ya wiki mbili.
Alisema
katika mazungumzo hayo, maofisa hao walimwahidi kumlipa tena Sabula Sh
500,000 kila mwezi ikiwa ni malipo ya kupeleka nyaraka za Chadema.
“Katika
makubaliano hayo, maofisa usalama walimtaka Sabula awe mpole na
mvumilivu kwani atapotea kwa miezi mitano au sita kabla ya kurudi kwenye
majukumu yake ndani ya Chadema.
“Uchunguzi
huu, tumeufanya kabla ya kukamatwa kwa Mkurungezi wetu wa Ulinzi na
Usalama, Wilifred Lwakatare ambaye hivi sasa anashitakiwa kwa tuhuma za
ugaidi….tumebaini kuwapo genge la watu kutoka ndani ya Serikali ya CCM,
familia ya kiongozi mkubwa wa nchi hii na chama hicho.
“Tumefanya
hivyo kwa kuangalia maslahi mapana ya taifa na chama hivi sasa, tunazo
nyaraka nyingi za mawasiliano na nyingine za picha kama mnavyoziona hapa
zikionyesha mambo yote yalivyokuwa yakipangwa.
“Mipango
yao yote ilikuwa ya kishetani, huku wakilenga kukisingizia Chadema,
watu hao kwa nyakati tofauti wameonekana kuanza mpango huo tangu mwaka
jana.
“Wamo
walioshiriki tukio la kutekwa Dk. Ulimboka na Mhariri Mtendaji Mkuu wa
Kampuni ya New Habari (2006), Absalom Kibanda,” alisema.
“Cha
ajabu kila walipokuwa wakiwasiliana na watu hao kwa nyakati tofauti,
lazima tukio linatokea, ukiangalia tukio la Kibanda utabaini siku moja
kabla kumekuwapo na mawasiliano ya watu hao, hivyo hivyo na kwa Dk.
Ulimboka.
“Tumebaini
fedha ya kurekodi video ya Lwakatare ilitoka Ikulu, Chadema tunashukuru
ushirikiano tulioupata kutoka kwa watu wa usalama, ndio maana tunasema
ndani ya CCM tupo, jeshini tupo, polisi tupo kitendo cha kusema chama
kitakufa wasahau hilo, Watanzania bado wana imani kubwa.
“Kesi
ya Lwakatare, imetufungua macho na kugundua mkakati mbaya wa Serikali,
ndiyo maana chama kimekaa na kuona uzito wa mkakati huu na kuniteua
kesho (leo), kuongoza jopo la mawakili wenzangu Profesa Abdallah Safari,
Tundu Lissu, Edson Mbogoro, Peter Kibatala na Nyaronyo Kichere kwa
ajili ya kumtetea Lwakatare.
“Nyaraka
tulizonazo, zinaonyesha jinsi vigogo wa idara ya usalama wa taifa
ilivyokuwa ikiwasiliana na viongozi wa CCM, hizi taarifa tutaziwasilisha
mbele ya mahakama na tunafurahi kesi kupelekwa huko.
“Hata
polisi au Usalama wa Taifa, wakifika sasa wakizitaka nitawapa kwani
zimeandaliwa nyingi za kutosha tunachoomba mahakama itende haki ili
ukweli ujulikane kwa Watanzania.
“Bahati
nzuri chama kimejipanga kukabiliana na mikakati michafu ya CCM,
kimeamua kuunda kanda maalum, Profesa Safari amepewa uenyekiti wa Kanda
ya Pwani, mimi msaidizi wake na Halima Mdee ni katibu, lengo ni
kuhakikisha 2015 majimbo ya Dar es Salaam na Pwani yanachukuliwa na
Chadema, tunataka tuwaonyeshe hatushindwi,” alisema.
Alisema
kuwa wakati wanafuatilia kupata mawasiliano katika kampuni za simu za
mikononi, wamepewa taarifa za watumishi wa Kampuni ya Vodacom, kuwa
Nchemba amekuwa akiwaomba kumfutia taarifa zake zote za awali katika
namba zake anazotumia (MTANZANIA tunazo).
“Miongoni
mwa mawasiliano ambayo yanahusika na ujambazi huu ni yale ya Desemba
28, siku ambayo mkanda wa Lwakatare ulirekodiwa pia Machi 4 hadi 6,
mwaka huu, siku moja kabla Kibanda kutekwa, taarifa hizo zinaonyesha
wazi, watusubiri mahakamani.
Marando
alisema hakubaliani na kitendo cha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA), kupiga marufuku watu kufuatilia mawasiliano ya watu wengine
ambapo alisisitiza kuendelea na uchunguzi kwa kuwa ni haki kwa raia
yeyote. NA http://www.mtanzania.co.tz
Taja hayo majina we mwandishi wa mtanzania kama yeye ameyataja hadharani wewe unaogopa nini?.basi inaonekana hii habari umeipika umelipwa pesa upike habari.wewe ni muongo na kama we ni mkweli andika hayo majina usilete uhasama hapa.....
ReplyDeletewewe soma habari kwa umakini usikurupuke kuhukumu,mabere ndo kaongea hayo maneno sio mimi,
ReplyDelete