MKUU wa
Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo ameamuru polisi kumkamata Mbunge wa
Arusha Mjini, Godbless Lema pamoja na wanafunzi walioshiriki kurusha
mawe baada ya kutokea vurugu zilizotokana na kifo cha mwanafunzi wa
mwaka wa pili, Chuo cha Uhasibu Arusha, Henry Kago (22).
Naibu
Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Faraji Kasidi jana alitangaza kufunga
chuo hicho kwa muda usiojulikana kutokana na vurugu zilizotokea chuoni
hapo, ikiwemo ukiukwaji wa nidhamu na urushwaji wa mawe uliofanywa na
wanafunzi hao kwa Mkuu wa Mkoa na kamati ya ulinzi na usalama.
Mulongo alitoa amri hiyo baada ya Lema kudaiwa kuingia chuoni hapo jana asubuhi na kufanya siasa bila kufuata utaratibu.
“Si jambo
jema kwa Mbunge kuingia chuoni na kuhamasisha siasa kwenye jambo hilo
la kifo badala ya kuwatuliza wanafunzi ili tujue kiini cha tatizo hili,"
alisema mkuu wa mkoa na kushutumu kwamba jambo hilo linabadilika badala
ya msiba linawekwa chuki za siasa na wanafunzi nao kuingia kwenye
mkumbo.
Kwa
mujibu wa mkuu wa mkoa, upo utata wa kifo cha Kago kutokana na wengine
kudai ameuliwa na bodaboda eneo la Esami na Kanisa la Waadventista
Wasabato karibu na chuo huku wengine wakidai alitoka eneo la Bugaluu.
Alisema polisi inachunguza utata wa kifo hicho cha mwanafunzi huyo aliyekutwa na simu yake ya mkononi.
"Naagiza
polisi kumkamata Lema popote alipo na wanafunzi wengine pamoja na
wakili wake,” alisema Mkuu wa Mkoa bila kutaja jina la wakili.
Kwa
mujibu pia wa RADIO FIVE ya jijini Arusha, Mkuu huyo wa mkoa wa
Arusha bwana Mulongo amenukuliwa kwa nyakati tofauti tangu jana
akitaja uwezekano wa Lema kusababisha kifo cha mwanafunzi ili apate
nafasi ya kufanya siasa chuoni hapo.
Credit: Habarileo na Radio five
No comments:
Post a Comment