Na Saleh Ally
MGOGORO wa kimuziki kati ya msanii Judith Wambura Mbibo ‘Lady Jaydee’ na kituo kimoja cha redio umezidi kuchukua kasi huku makundi mawili, kila moja likitengeneza ngome yake na kuamini linachoamini.
MGOGORO wa kimuziki kati ya msanii Judith Wambura Mbibo ‘Lady Jaydee’ na kituo kimoja cha redio umezidi kuchukua kasi huku makundi mawili, kila moja likitengeneza ngome yake na kuamini linachoamini.
Kundi ambalo linamuunga mkono Jaydee na kumuona ni mkombozi,
anazungumza kwa niaba yake na wasanii wengine, la pili ni lile
linalobaki upande unaoshambuliwa, linatetea ngome yake.
Jaydee anashutumu kubaniwa nyimbo zake na kituo hicho ambacho kupitia
mitandao kadhaa ya kijamii ameeleza wazi kuwa wanambania, wanaziponda
lakini hata watangazaji wake wamekuwa wakionyesha chuki binafsi dhidi
yake.
Jaydee pia aliwaponda wasanii Ben Pol na Linah anayetokea THT kwamba
walishindwa kutokea kwenye uzinduzi wa video ya wimbo wake wa Joto
Hasira, kwa madai walizuiwa na bosi wao.
Ujasiri huu wa Jaydee ndiyo kitu bora ambacho kimekuwa kikitakiwa kufanyika kutoka kwa wasanii, yaani wapigane kutetea muziki wa Tanzania hasa kama kuna watu au kundi la watu limejikita katika kuuangamiza.
Lakini ni tofauti kidogo, kwani wasanii wengi wamekuwa imara na kuwa
tayari kujitetea wenyewe tu na si vingine. Nasisitiza mara nyingi, wao
ndiyo wahusika wa kwanza na wanapaswa kuanzisha mapinduzi kuanzia kwao,
mfano kusema naonewa si kitu kibaya lakini je, umewahi kupigania
wanaoonewa?
Kujitetea pekee unaweza kufanya, lakini vipi utafanikiwa kama asilimia
kubwa ya kundi la wanamuziki linaendelea kuonewa. Ukibaki hauonewi pekee
na asilimia kubwa ya wasanii au wanamuziki inaonewa, kunaweza kuwa na
mapinduzi sahihi?
Ndiyo
maana nashangazwa kusikia Jaydee leo anaona ubovu wa kituo hicho,
anathubutu kusema hadharani akionyesha wazi ameumia. Lakini miaka 10 au
zaidi iliyopita, Jaydee alikuwa kimya na hakuwaza kusema kwamba kituo
hicho kinawabania wasanii wengine na ‘kumtukuza’ yeye hata kama muziki
wake haukuwa wa kiwango kilichokuwa kinazungumzwa.
Siwezi kusema muziki wa Jaydee ni mbaya, nimekuwa kati ya mashabiki
wake. Lakini yoyote atanichekesha akisema nyimbo albamu zake zote
alizotoa zilikuwa katika kiwango cha juu sana na ndiyo maana leo ni
maarufu.
Hakuna asiyejua kwamba miaka nenda rudi, wasanii wamekuwa wanaongoza
kwa unafiki, kutopendana wenyewe, kugeukana na hata kujenga makundi
lukuki, ndiyo maana kila kukicha wamekuwa wakishambuliwa maana katika
maisha yao hawana umoja.
Jaydee alianza kuwa mtangazaji katika kituo hicho baada ya kuacha
kurap, akaamua kuachana na kurap na mwisho kuwa msanii wa nyimbo za
kubembeleza, mara ya kwanza akianza kutikisa na albamu ya Machozi, Solo
Thang anaweza kuhadithia vizuri kuhusu hili.
Kuanzia albamu ya Machozi, kituo hicho ndicho kilisimama kuhakikisha
anakuwa bora hata kama muziki wake haukuwa ukimzidi kila mwanadada
wakati huo.
Angalia, kulikuwa wasanii kama Stara Thomas, Carola Kinasha ambao
kiuwezo walikuwa juu kuliko Jaydee, lakini hawakupewa nafasi ya kutosha,
badala yake Jaydee ambaye hakuthubutu kuwatetea hata kidogo akaendelea
‘kubebwa’ na watu wakaamini ni bora kuliko yoyote kwa upande wa akina
dada au kina mama katika kuimba, haikuwa hivyo.
Angalia albamu ya Binti, karibu nyimbo zote zilikuwa na ujumbe mmoja,
ulikuwa ukimshambulia mwaname mmoja ambaye alikuwa amemuumiza Jaydee.
Takribani ujumbe wa nyimbo karibu zote ulikuwa ni mmoja, lakini ilibebwa
na kuonekana ni moja ya albamu bora kabisa kuwahi kuwepo katika muziki
wa Tanzania, kitu ambacho hakikuwa sahihi.
Wakati huo wasanii lukuki walilia kubaniwa, mmoja wao alikuwa ni Joseph
Mbilinyi ‘Sugu’ ambaye ndiye alimtambulisha mwanadada huyo
alipomshirikisha katika wimbo wa Mambo ya Fedha, kabla ya hapo hakuwa na
jina. Jaydee hakuwahi kuungana naye hata kidogo hata kwa mstari mmoja
wa kumtetea au kuunga mkono kutetea muziki wa Tanzania, kuonyesha
anapinga mwenendo wa wanaolazimisha kuwabagua wasanii au kufanya mambo
kwa mabavu kwa kuwa wameshika mpini.
Hakuna aliyesikia kilio cha Sugu, wasanii wanaochipukia bila ya kujua
wasemacho, kisa nyimbo zao zinapigwa redioni, ili kuonyesha shukrani za
dhati wakaanza kutangaza Sugu anatapatapa na amekwisha kimuziki!
Ajabu, asilimia kubwa ya maneno yake ndiyo yanayozungumzwa leo, ndiyo
yanatumiwa na kila msanii anayebanwa au kuhisi kaonewa. Angalia, hata
Jaydee naye ameingia huko! Swali langu hapa je, Jaydee na wengine
wanaolalamika, wamekwisha kisanii?
Ndiyo maana nasema, tasnia ya muziki hasa muziki wa kizazi kipya
umejaza watu wavivu kufikiri, wenye mioyo ya ‘Kichina’, wasio na uwezo
wa kuthubutu hata kidogo ambao wanasubiri wayumbe au kuumizwa wao ili
wamtafute wa kumuangushia lawama.
Jiulize, kama Jaydee alibebwa kwa miaka 10, halafu leo analalamika
atakuwa sahihi? Sitaki kumpinga kwa kuwa kuna kitu anakiona lakini
ninaamini alikiona tokea mapema, akauchuna.
Bado nasisitiza, yeye na wengine wote wanaolia baada ya kuguswa wao
nawaita wanafiki, wanapigana kwa ajili yao na si kwa muziki
wanaoutumikia. Iwapo wangekuwa tayari kupambana kwa ajili ya muziki huo,
msanii kama Jaydee asingeanza vita leo.
NARUDI KWA JAYDEE
Sijawahi kuingia naye katika malumbano zaidi ya miaka 10 tokea alipokuwa mwanahabari mwenzangu na sasa msanii. Lakini nathubutu kumueleza kuwa ni kati ya wasanii wasiojali muziki wa Tanzania na wanajiangalia wao zaidi.
Sijawahi kuingia naye katika malumbano zaidi ya miaka 10 tokea alipokuwa mwanahabari mwenzangu na sasa msanii. Lakini nathubutu kumueleza kuwa ni kati ya wasanii wasiojali muziki wa Tanzania na wanajiangalia wao zaidi.
Picha ya unafiki na kujiangalia mwenyewe inaonekana sasa ingawa
takribani miaka mitano iliyopita nilianza kuinusa. Leo analia, anabaniwa
na anauona moto unaounguza muziki wa Tanzania ulivyo mkali.
Naamini aliuona miaka kibao nyuma, lakini kwa kuwa alikuwa akitetewa
hakuweza kuangalia kwamba rafiki zake, wasanii waliombeba kabla walikuwa
wakiungua. Akaendelea kuwapita kwa raha zake mustarehe.
Tungeweza kumuita Jaydee ni mpambanaji kama angewakosoa hao anawakosoa
sasa katika kipindi walichokuwa wamempa mbeleko yeye, basi kweli
ingeonekana anapigania muziki wa Tanzania. Sasa anapigania chake tu!
Jaydee amefika mbali kimuziki, alikuwa bora jukwaani na nyimbo kadhaa
na nyingi zikapewa ‘over promotion’ lakini bado ninaweza kumuita
mkongwe. Ajabu alibaki chipukizi hadi leo katika suala la kutetea haki
za wasanii na muziki wenyewe.
Sitaki kumkatisha tamaa kwa mapambano aliyoyaanza, ninaamini ana nafasi
ya kuanza kuusaidia muziki ambao umemsaidia. Lakini ndiyo kipindi
ambacho anaweza kupata machungu waliyopata wasanii wenzake kunyeshewa
mvua na kuunguzwa na jua wakati akiwa kivulini kwa ‘msaada’.
Anachokifanya leo Jaydee ni nyongeza tu ya walichokifanya Sugu au
Afande Sele au wasanii wachache walioamua kuwa wakweli au wale walioamua
kuwa wabunifu kama Ambwene Yessaya ‘AY’, aliyekimbia vita ya redio na
kuingia katika kurekodi video bora zilizoendelea kumng’arisha.
Simzuii, Jaydee kuendelea kupambana, lakini namuasa anachokifanya kama ni kwa ajili ya muziki akipozwa tena, asirudi nyuma.
Ninachomkumbusha, hata yeye amekuwa kundi moja na analowalaumu ambao
angeweza kuwashauri mapema ‘ndani ya mjengo’ kama angekuwa na nia nzuri
na muziki wa kizazi kipya. Msisitizo ‘Joto Hasira’ liwe la kweli.
source bongoclantz
source bongoclantz
EEEEEEEeeee kweli umefunguka na umeongea sense sana...good
ReplyDelete