1. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Kufuatia marekebisho kadhaa ya kanuni hususan zinazolenga kwa sasa
Utaratibu wa Kutunga Sheria kuhusiana na mambo ya fedha, nasi kama Kambi
Rasmi ya Upinzani tutafanya marekebisho katika utaratibu tutakaotumia
katika kutoa maoni yetu kwa Serikali.
Kwa muda mrefu, kufuatia utaratibu wa mfumo wa bajeti ulivyokuwa huko
nyuma, tulitumia muda mwingi kuishauri serikali namna bora ya kuboresha
bajeti na utendaji wake wa kazi. Hata hivyo, kwa bahati mbaya sana,
serikali hii imekuwa siyo sikivu vya kutosha hata kama pale ambapo
ushauri unaotolewa uko wazi kwa masilahi na mustakabali mwema wa Taifa
letu.
Aidha, pale ambapo Serikali imechukua maoni yetu, mara nyingi imekuwa
haina ustaarabu wa kutambua, kukiri na kushukuru mchango wa Kambi ya
Upinzani, bali mbele ya macho ya umma imeendelea kutoa kebehi kujaribu
kuuaminisha umma kuwa vyama vya upinzani havina ufumbuzi mbadala kwa
matatizo yanayolikabili Taifa.
Mheshimiwa Spika,
Tatizo kubwa la Serikali inayoongozwa na CCM ni kukosa weledi wa
kutekeleza kikamilifu vipaumbele vyake pamoja na kuviainisha kupitia
Mpango wake wa miaka 5, bajeti na programu mbalimbali. Hali hii inaweza
kutafsiriwa kama uwezo duni wa kusoma alama za nyakati ikiwemo kubuni na
kusimamia inachokiamini. Ni dhahiri vilevile unapolazimika kufanya
jambo usiloliamini au lisilo kipaumbele chako, bali cha kulazimishwa na
mazingira unatekeleza bila kujua undani wake na hatma yake ni kuharibu
zaidi.
Mheshimiwa Spika,
Kwa kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ni mtambuka, Mwaka huu tutajielekeza
kuzungumzia mambo makuu machache ambayo sisi tunaamini ni vipaumbele
muhimu ambavyo Waziri Mkuu na wasaidizi wake wanapashwa kuja na majibu
ya kueleweka kwa Watanzania. Aidha, mengine yatawasilishwa kupitia
hotuba zetu mbalimbali katika Wizara husika.
2. TUME YA MABADILIKO YA KATIBA, NA MCHAKATO WA KATIBA MPYA NA MSTAKABALI WA TAIFA
Mheshimiwa Spika,
Tarehe 18 Novemba, 2011 Bunge lako tukufu lilipitisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011.
Kufuatana malalamiko mengi kuhusu utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa
Sheria hiyo na kufuatia vikao kati ya Mheshimiwa Rais na Kamati Maalum
ya CHADEMA pamoja na wadau wengine, Sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho
wakati wa Mkutano wa Sita wa Bunge hili uliofanyika mwezi Februari mwaka
2012.
Marekebisho hayo yalikuwa ni awamu ya kwanza ya awamu tatu za
marekebisho ya Sheria hiyo kwa mujibu wa makubaliano yetu na Mheshimiwa
Rais. Awamu nyingine mbili za marekebisho zilitarajiwa kukamilika kabla
ya mwisho wa mwaka jana, yaani 2012. Hata hivyo, hadi nasoma maoni haya
leo hii, Sheria ya Marekebisho ya Katiba haijafanyiwa marekebisho
mengine yoyote.
Mheshimiwa Spika,
Mara baada ya marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kupitishwa
mwaka jana, Mheshimiwa Rais alifanya uteuzi wa wajumbe na watendaji
wakuu wa Tume na Tume yenyewe ilianza kazi mwezi Mei, 2012. Kwa maana
hiyo, hadi kufikia leo Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeshafanya kazi kwa
karibu mwaka mmoja.
Kwa masikitiko makubwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda
kulijulisha Bunge lako tukufu kwamba katika kipindi hiki mtiririko wa
matukio kadhaa ndani na nje ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba
imethibitisha kwamba haina weledi, dhamira au nia ya kusimamia mchakato
huru usiofungamana na upande wowote.
Katika mwaka wa kwanza wa mchakato wa upatikanaji Katiba mpya, Tume ya
Mabadiliko ya Katiba imethibitisha hofu tuliyokuwa nayo toka mwanzo
kwamba lengo la mchakato wa Katiba Mpya uliowekwa kwa mujibu wa Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba ni kuhakikisha kwamba mabadiliko pekee
yakayokuwepo ni yale yenye kulinda matakwa ya CCM na Serikali yake au
yale pekee yatakayokuwa na Baraka za “Status Quo”.
Mheshimiwa Spika,
Kwanza, Tume haikuweka utaratibu wowote madhubuti wa kutoa elimu kwa
wananchi juu ya masuala yote yanayohusu Katiba Mpya ili kuwaandaa
wananchi kuchangia maoni yao kwa Tume wakiwa na uelewa wa kutosha.
Badala yake, wakati wa mikutano ya Tume ya kupokea maoni ya wananchi,
wajumbe wa Tume walipewa jukumu la kuwaeleza wananchi juu ya Katiba Mpya
kwa muda usiozidi nusu saa!
Kwa kulinganisha, Tume ya Katiba ya Kenya ilifanya kazi ya kutoa elimu
kwa umma kwa nchi nzima kwa muda wa miezi sita kabla ya kuanza kukusanya
maoni ya wananchi wa Kenya juu ya Katiba Mpya. Matokeo yake ni kwamba
mchakato wa Katiba Mpya wa Kenya umeiletea nchi hiyo Katiba Mpya ya
mwaka 2010 ambayo imeanza kudhihirisha ubora wake kwa jinsi ambavyo
mambo yatokanayo na Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo wa hivi karibuni
yalivyotatuliwa.
Mheshimiwa Spika,
Pili, muda uliowekwa na Tume wa kukusanya maoni ya wananchi ulikuwa
mdogo sana ukilinganisha na ukubwa wa nchi yetu na wingi wa Watanzania.
Katika Majimbo karibu yote ya uchaguzi Tanzania Bara, Tume iliendesha
wastani wa mikutano saba kwa kila jimbo kwa lengo la kukusanya maoni ya
wananchi.
Katika mikutano hiyo wananchi walitakiwa kutoa maoni yao kuhusu Katiba Mpya kwa muda wa dakika tano kila
mmoja na mikutano yenyewe ilichukua muda wa masaa matatu ikiwa ni
pamoja na muda wa kutambulishana wajumbe wa Tume na mambo mengine yaliyo
nje ya kuchukua maoni ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, matokeo yake ni kwamba kwa mujibu wa maelezo ya
Mwenyekiti wa Tume Jaji Joseph Sinde Warioba kwa waandishi habari
tarehe 5 Januari mwaka huu, hadi awamu nne za kukusanya maoni ya
wananchi zinakamilika tarehe 19 Desemba, 2012, Tume ilikwisha kufanya
mikutano 1,776 kwa nchi nzima. Aidha, kwa mujibu wa maelezo ya
Mwenyekiti Warioba, hadi kufikia kipindi hicho wananchi wapatao 64,737
walikwishatoa maoni yao kwa kuzungumza wakati wananchi 253,486 walitoa
maoni kwa njia ya maandishi, na wengine 16,261 walitumia njia ya “posta,
tovuti ya Tume, mitandao ya kijamii na ujumbe mfupi wa simu za
mkononi....” Kwa hiyo, kwa mujibu wa taarifa hizi za Mwenyekiti wa Tume,
kati ya Watanzania takriban milioni 45, ni Watanzania 334,484 ndio
waliotoa maoni juu ya Katiba Mpya hadi kufikia tarehe 4 Januari, 2013.
Idadi hii ni sawa na asilimia 0.7 ya Watanzania wote! Na hao ndio waliotoa maoni yao kwa muda wa dakika tano kila mmoja, wakiwamo waheshimiwa Wabunge wa Bunge hili tukufu.
Mheshimiwa Spika, ni wazi, kwa takwimu hizi za Tume ya Mabadiliko
ya Katiba na kwa vyovyote vile, Katiba Mpya itakayotokana na maoni haya
haiwezi kuwa Katiba Mpya ya Watanzania wote. Utaratibu wa hovyo namna
hii utazaa Katiba Mpya ya hovyo!!! Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inaamini kwamba utaratibu huu wa hovyo hauwezi kutupatia Katiba Mpya
yenye maridhiano ya kitaifa kwa ajili ya kutatua migogoro mingi ya
kisiasa, kijamii na kidini ambayo inaikabili nchi yetu kwa sasa.
Mheshimiwa Spika,
Tatu, licha ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kutangaza kuwa Tume
itakuwa huru katika utekelezaji wa majukumu yake, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inaona kila dalili za Tume kutokuwa huru au kuutafsiri
uhuru vibaya. Kwa mfano, kuna ushahidi kwamba Tume imekuwa na
mawasiliano ya karibu na Serikali na Ofisi ya Rais kwa namna ambayo
inaashiria Tume kutokuwa huru. Ndio maana katika hotuba yake ya kumaliza
mwaka uliopita na kufungua Mwaka Mpya, Rais Jakaya Kikwete
alilitangazia taifa ratiba ya kazi za Tume ambayo Tume yenyewe ilikuwa
haijawahi kuitoa hadharani.
Katika hotuba yake hiyo, Rais Kikwete alitangaza sio tu kumalizika kwa
awamu za kukusanya maoni ya wananchi, bali pia alitangaza ratiba ya Tume
kuanza kuchukua maoni ya vyama vya siasa, taasisi nyingine na ‘makundi
maalum’, tarehe ya kutolewa kwa Rasimu ya Kwanza ya Katiba Mpya,
Mikutano ya Mabaraza ya Katiba na Bunge Maalum la Katiba na hata tarehe
ya kura ya maoni na upitishwaji wa kura ya maoni kuihalalisha Katiba
Mpya.
Mheshimiwa Spika, Rais asingeweza kufahamu ratiba hii yote bila
kupatiwa taarifa ama na Tume yenyewe ama na watendaji au watumishi wake
au na wajumbe wa Tume. Mbali na taarifa ya kwisha kwa awamu ya tatu ya
zoezi la kukusanya maoni ya wananchi, taarifa hizi hazikuwa zimetolewa
hadharani na Tume kabla ya hotuba ya Mwaka Mpya ya Rais Kikwete!
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imetambua siku zote kwamba msemaji rasmi
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni Mwenyekiti wa Tume Joseph Warioba.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haijawahi kusikia wala kuona mahali
popote ambapo Sheria ya Mabadiliko ya Katiba imempa Rais Kikwete jukumu
la kuwa msemaji wa Tume. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji kama
Rais anaweza kupatiwa taarifa za kina namna hiyo kuhusiana na shughuli
za Tume, kuna uhakika gani kwamba yeye au Serikali yake hawatoi kwa Tume
maelekezo ya kichinichini juu ya nini cha kufanya, kwa namna gani na
kwa wakati gani.
Mheshimiwa Spika,
Nne, wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba ikitoa taarifa za kina juu ya
shughuli zake kwa Rais Kikwete na Serikali yake, Tume hiyo hiyo
imetangaza wazi wazi kwamba haiwajibiki kwa Bunge kuhusu utekelezaji wa
majukumu yake kwa mujibu wa Sheria. Zaidi ya kumtuma Naibu Katibu wa
Tume, viongozi wa Tume kama vile Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na
wajumbe wa Tume wamekataa kuhudhuria vikao vya Kamati ya Bunge ya
Katiba, Sheria na Utawala ili kuieleza Kamati juu ya utekelezaji wa
majukumu yake kwa mujibu wa Sheria na Katiba ya Nchi.
Katika hili, Tume imeungwa mkono na Serikali hiyo hiyo inayoelekea
kupata taarifa za kina juu ya utekelezaji wa kazi zake! Hii ni licha ya
kupatiwa jumla ya shilingi bilioni 33.944 za walipa kodi wa Tanzania
zilizoidhinishwa na Bunge katika mwaka wa fedha 2012/2013 kwa ajili ya
kutekeleza majukumu yake. Kwa hiyo, wakati Tume inaharibu mchakato wa
Katiba Mpya kama tulivyoonyesha hapa, Bunge – kwa kupitia kwa Kamati
yake – limezuiliwa kuhoji shughuli za Tume kwa hoja kwamba Tume iko
huru.
Mheshimiwa Spika, hii inaweza kuwa mara ya kwanza kwa chombo cha
umma kinachotumia mabilioni ya fedha za umma kilichopewa majukumu ya
umma na Sheria iliyotungwa na Bunge hili tukufu kukataa kuwa chini ya
usimamizi wa kikatiba wa Bunge (parliamentary oversight)!
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imesikitishwa sana na kushindwa
kwa Kamati husika ya Bunge kudai madaraka yake ya usimamizi yasipuuzwe
na Tume na/au Serikali. Udhaifu huu wa Bunge na Kamati unaweza
kuligharimu Taifa endapo mchakato wa Katiba Mpya utachakachuliwa na
kuliingiza Taifa katika machafuko ya kisiasa, kidini au kijamii.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli mbele ya
Bunge hili tukufu juu ya uwajibikaji wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa
matumizi ya mabilioni ya fedha za umma iliyoyaidhinishiwa mwaka jana na
inayoyaomba mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Spika,
Tano, Tume imetengeneza utaratibu wa mabaraza ya kikatiba ambao kwa
ushahidi wa mwanzo tu unaonyesha kwamba hayo ni mabaraza ya CCM na sio
mabaraza ya katiba ya Watanzania wote. Hili limefanyika kwa kupitiaMwongozo
Kuhusu Muundo, Utaratibu wa Kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya
Wilaya (Mamlaka za Serikali za Mitaa) na Uendeshaji Wake, uliotolewa
na Tume mwezi Februari mwaka huu. Kwa mujibu wa Muundo huu, wajumbe wa
Mabaraza ya Katiba ya Wilaya watachaguliwa na Kamati za Maendeleo za
Kata (maarufu kama ‘WDC’) baada ya kuwa wamechaguliwa moja kwa moja na
wananchi katika vijiji na mitaa. Wajumbe wa WDC ni Madiwani wa Kata
ambao ni Wenyeviti wake, Watendaji wa Kata ambao ni Makatibu na
Wenyeviti wa Vijiji au Mitaa.
Mheshimiwa Spika, kwa kufuatana na chaguzi za vijiji na mitaa za
mwaka 2009, zaidi ya asilimia 90 ya vijiji na mitaa inaongozwa na
wenyeviti ambao ni wanaCCM. Aidha, kutokana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2010, zaidi ya asilimia 80 ya Kata zote nchini zinaongozwa na madiwani
wa CCM. Hawa ndio waliochagua wajumbe wa Mabaraza ya Wilaya ya Katiba
tangu mwanzoni mwa wiki iliyopita. Matokeo yake, kwa taarifa ilizo nazo
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kutoka sehemu mbali mbali za nchi yetu,
kila mahali wagombea ambao hawakuwa wanaCCM walienguliwa katika ngazi ya
uchaguzi wa vijiji au mitaa au wameenguliwa na WDC baada ya kushinda
katika ngazi hizo.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina ushahidi kwamba viongozi wa
kiserikali kama vile Wakuu wa Wilaya na wa Mikoa waliwahamasisha
wenyeviti wa vijiji, mitaa na madiwani kuhakikisha kwamba wagombea wote
wasiokuwa wa CCM, hasa wa CHADEMA, wanaenguliwa katika chaguzi za
vijiji, mitaa au kata. Mfano mzuri ni wa Mkuu wa Wilaya ya Musoma
Jackson Msome aliyeitisha mkutano wa wenyeviti wote wa mitaa ya Musoma
Mjini na kuwapa maelekezo ya kuhakikisha kwamba watu wasiokuwa wanachama
wa CCM hawapati nafasi katika Mabaraza ya Katiba ya Wilaya au Manispaa
hiyo.
Mheshimiwa Spika, licha ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kupatiwa
maoni ya wadau kwamba utaratibu huo utaharibu mchakato wa Katiba Mpya,
Tume ilikataa kata kata kuubadilisha Muundo wa Mabaraza haya. Ni wazi
kwamba Tume inafahamu inachokifanya.
Ni wazi vile vile kwamba Tume inafahamu matokeo ya hicho inachokifanya,
yaani kuundwa kwa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ambayo ni ya wanaCCM. Na
wala haihitaji shahada ya uzamivu kufahamu kwamba Mabaraza ya Katiba ya
Wilaya yenye kutawaliwa kwa kiasi hicho na wanaCCM yatatoa maoni ya aina
gani juu ya Rasimu ya Katiba Mpya yatakayoijadili. Itakuwa ni Katiba
Mpya kwa jina tu, mambo mengine ya msingi yatabaki vile vile. Kwa maneno
mengine, itakuwa ni Katiba ile ile, ya watu wale wale, wa chama kile
kile.
Mheshimiwa Spika, Uchakachuaji wa mchakato wa Katiba Mpya wa aina
hii ndio ulioiingiza Zimbabwe katika machafuko makubwa ya kisiasa toka
mwaka 1998 na Kenya mwaka 2007/2008. Kwa utaratibu huu wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, inaelekea Serikali ya CCM inaelekea kutotaka
kujifunza kutokana na yaliyowakuta jirani zetu wa Kenya na marafiki zetu
wa Zimbabwe.
Mheshimiwa Spika,
Sita, Serikali imekataa ama imeshindwa kuheshimu makubaliano iliyofikia
na wadau mbali mbali ikiwemo CHADEMA, kufanya marekebisho zaidi ya
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa sababu hiyo, bado haijulikani
wajumbe mia moja na sitini na sita watakaotokana na taasisi mbali mbali
zilizotajwa na Sheria hiyo watateuliwa kwa utaratibu gani na nani
atakayefanya uteuzi huo.
Vile vile, bado hakuna muafaka juu ya uhalali wa idadi kubwa ya wajumbe
wa Bunge Maalum la Katiba kutoka Zanzibar kushiriki katika mjadala wa
Katiba Mpya kwenye masuala yasiyokuwa ya Muungano ya Tanzania Bara
wakati hakuna mjumbe hata mmoja wa Tanzania Bara anayeweza kushiriki
katika mijadala ya kikatiba inayohusu masuala ya Zanzibar yasiyokuwa
Mambo ya Muungano.
Zaidi ya hayo, bado hakuna majibu yanayotosheleza yanayompa Rais mamlaka
ya kuliitisha upya Bunge Maalum la Katiba na kulielekeza ‘kuboresha’
masharti ya Katiba Mpya mara baada ya Bunge hilo kuipitisha. Aidha,
haijulikani ni uhalali upi wa kisheria na kikatiba utakaoiruhusu Tume ya
Taifa ya Uchaguzi kusimamia na kuendesha kura ya maoni ya kuhalalisha
Katiba Mpya kwa sababu Katiba na Sheria za Uchaguzi za sasa hazitambui
wala kuweka utaratibu wa kuendesha kura ya maoni.
Mheshimiwa Spika, kushindwa kwa Serikali kuleta Muswada wa
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili kufanya marekebisho
katika maeneo tajwa ni ushahidi wa wazi kwamba Serikali ya CCM haina nia
ya dhati na dhamira safi ya kuhakikisha Tanzania inapata Katiba Mpya
inayoistahili.
Aidha, si nia ya CHADEMA kuendelea kushiriki na kubariki mchakato huu
kama ulivyo sasa kwani ishara zote ziko wazi kuwa Katiba inayokusudiwa
ni ile tu itakayokidhi matakwa ya Wana- CCM na Washirika wake na hivyo
kutokutimiza azma ya kuwa na Katiba itakayoponya majeraha mbalimbali na
kurejesha uzalendo, mshikamano na upendo wa dhati miongoni mwa
Watanzania na kisha mfumo wa Utawala utakaokidhi mahitaji ya wakati.
Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inatangaza rasmi kwamba: CHADEMA
itajitoa ushiriki wake katika mchakato wa Katiba Mpya endapo mambo
yafuatayo hayatapatiwa ufumbuzi hadi kufikia mwisho wa mwezi huu, yaani
tarehe 30 Aprili, 2013:
- Kufutwa kwa uteuzi/uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ya wilaya ya Katiba uliofanywa na Kamati za Maendeleo za Kata, na badala yake wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya wachaguliwe moja kwa moja na wananchi wa Kata husika bila kuchujwa na WDC;
- Serikali ilete mbele ya Bunge hili tukufu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba yatayofanyia maeneo yafuatayo marekebisho:
- Vifungu vyote vinavyohusu uwakilishi katika Bunge Maalum la Katiba wa taasisi zilizoainishwa katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba;
- Vifungu vyote vinavyohusu ushirikishi wa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka Zanzibar katika mijadala inayohusu mambo yasiyokuwa ya muungano ya Tanzania Bara;
- Vifungu vyote vinavyohusu mamlaka ya Rais kuitisha tena Bunge Maalum la Katiba baada ya Bunge hilo kuwa limeshapitisha Rasimu ya Katiba Mpya kwa lengo la kufanya marekebisho katika Rasimu kabla haijapelekwa kwenye kura ya maoni;
- Vifungu vyote vinavyohusu mamlaka ya kikatiba nay a kisheria yatakayoiwezesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuendesha na kusimamia kura ya maoni;
3. ANGUKO LA ELIMU TANZANIA: ANGAMIZO LA KIZAZI NA JANGA LA TAIFA.
Mheshimiwa Spika,
Nianze kuzungumzia umuhimu wa elimu kwa kumnukuu Rais wa 55 wa Marekani, John F.Kennedy (1917 – 1963);
“Our progress as a nation can be no swifter than our progress in education. The human mind is our fundamental resource”
Mheshimiwa Spika,
Siku za karibuni kumekuwepo mjadala mzito sana kuhusiana na hali ya
elimu nchini. Pamekuwepo na malalamiko mengi sana yakiwemo yaliyomtaka
Waziri wa Elimu Mhe. Shukuru Kawambwa na Naibu wake Mhe Phillip Mulugo
wajiuzulu kama ishara ya uwajibikaji wa kisiasa. Ni dhahiri kuwa elimu
yetu kama Taifa imeporomoka kwa kiasi kikubwa cha sasa kuhatarisha
mustakabali wetu kama Taifa.
Mheshimiwa Spika, ni mwaka mmoja tu umepita tangu Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA itoe angalizo kali kwa Serikali
juu ya kasi kubwa ya kuporokoka kwa Elimu ya Tanzania na hivyo kuitaka
Serikali kuchukua hatua madhubuti ili kuliepusha Taifa na balaa hilo.
Hata hivyo, Serikali hii ya CCM imeendelea kupuuza ushauri mzuri
inayopewa bure na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na matokeo yake ni
kwamba anguko la mwaka huu ni kubwa kuliko maanguko yote yaliyowahi
kutokea katika Historia ya Tanzania ambapo asilimia 60.6 (240,903) ya
wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne wamepata daraja sifuri na
wengine asilimia 26.02 (103,327) daraja la nne. Jumla ya kufeli huku ni
zaidi ya asilimia 86.62 au sawa na
Mheshimiwa Spika, kufuatia kufeli huku kwa kutisha kwa wahitimu
wa kidato cha nne mwaka 2012, wadau wengi walitaka baadhi ya viongozi wa
sekta ya elimu akiwemo waziri kuwajibika. Ni bahati mbaya sana kuwa
Waziri Mkuu ni mmoja wapo wa viongozi Wakuu aliyestahili kuchukua hatua
za kuwawajibisha wahusika lakini hakufanya hivyo. Badala yake,
akakimbilia kuunda tume ya uchunguzi, ilhali yeye mwenyewe Waziri Mkuu,
Waziri wake wa elimu na serikali yake yote ikijua fika nini
kinasababisha kuporomoka kwa elimu yetu. Yumkini, kama kweli serikali
hadi leo haijui sababu ya kuporomoka kwa elimu yetu, basi haina tena
sifa wala weledi wa kusimamia siyo tu elimu, bali maisha ya kila siku ya
Watanzania.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa kufeli huku hakuwezi
kuchukuliwa kama bahati mbaya hasa ikiwekwa maanani kuwa mserereko wa
watoto wetu kufeli umeshika kasi chini ya utawala wa Serikali ya awamu
ya nne hasa kuanzia mwaka 2007.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2007, ufaulu wa vijana wetu wa kidato cha
nne ilikuwa (90.3%), 2008 (83.6%), 2009 (72.5%) na 2010 (50.4%).
Kufuatia mserereko huu wa kufeli, serikali iliunda timu iliyoshirikisha
wataalam kadhaa kubaini chanzo chake na tiba ya muda mfupi, muda wa kati
na muda mrefu. Timu hii iliyokuwa chini ya Uenyekiti wa Bw. Francis M.
Liboy wa TAMISEMI ilikamilisha ripoti yake mwaka 2011 na kutoa
mapendekezo kadhaa kwa serikali. Waziri wa Elimu Mhe. Shukuru Kawambwa
anaijua ripoti hii kwani ndiye aliyeandika dibaji yake. (Angalia kiambatanisho A)
Mheshimiwa Spika, mbali na ushauri wetu wa mara kwa mara,
serikali hii imebeza kwa nguvu zote juhudi mbalimbali zinazofanywa na
wadau wengine wenye kuumizwa na kusikitishwa na kuporomoka huku kwa
elimu. Watanzania ni mashahidi namna katika Mkutano wa Kumi wa Bunge,
hoja binafsi ya Mheshimiwa James Mbatia (Mb) kuhusu udhaifu ulioko
katika sekta ya elimu ilivyochukuliwa kimzaha na kutolewa majibu mepesi
na Serikali kinyume na kanuni za bunge na hatimaye kuyazima maazimio ya
bunge ya kuinusuru elimu ya Tanzania yaliyokuwa yamependekezwa katika
hoja hiyo. Ni katika mkutano huohuo wa Bunge ambapo hoja binafsi ya
Mheshimiwa Joshua Nassari (Mb) kuhusu Baraza la Mitihani linavyoathiri
elimu ya Tanzania iliondolewa katika orodha ya shughuli za mkutano wa
kumi wa Bunge bila ridhaa ya mtoa hoja kinyume na kanuni ya 58(5).
Mheshimiwa Spika, kitendo cha Serikali ya CCM chini ya mwavuli wa
wingi wa wabunge wake bungeni, cha kuzivuruga hoja hizi na hivyo
kusababisha maazimio ya bunge juu ya hoja hizi kutotekelezwa ni udhaifu
mkubwa sana kwa chama kinacho tawala cha CCM na Serikali yake na ni
ushahidi uliokamilika kwamba Elimu kwao sio kipaumbele cha taifa.
Mheshimiwa Spika, Serikali ambayo Elimu sio kipaumbele chake,
haiwafai Watanzania kwa karne hii. Kuendelea kuukumbatia utawala na aina
hii ni kukaribisha maafa yasiyoepukika kwa Taifa. Mbali na
kulisababishia Taifa hili aibu kubwa mbele ya majirani zetu na jamii ya
kimataifa kwa vijana walio wengi wa Kitanzania kuonekana kuwa na elimu
ya mashaka na isiyoweza kuhimili ushindani wa soko la ajira, ubovu wetu
wa elimu umedumaza uwezo wetu wa ndani wa kusimamia rasilimali za Taifa,
Aidha kambi Rasmi ya Upinzani inawapa angalizo wananchi wote wa
Tanzania kwamba haya yote yanatokea kwa kuwa Serikali ya CCM haijaiweka
Elimu kuwa kipaumbele cha taifa na kwamba umefika wakati wa kufanya
mabadiliko makubwa ya mfumo wa utawala kwa kuchagua chama chenye nia ya
dhati ya kuleta mabadilko kitakachounda Serikali inayojali elimu ya
watoto wao na bila shaka chama hicho hakiwezi kuwa CCM tena.
Mheshimiwa Spika, Taifa kupitia hotuba hii linataka kujua
Serikali ina nini cha kusema kuhusiana na utafiti huu iliofanya mwaka
2011, imetekeleza mangapi kati ya mapendekezo 27 yaliyotolewa. Aidha ni
kwa nini imeunda tume nyingine kwa kutumia fedha za walipa kodi wa nchi
hii ingali ripoti nyingine inayohusu somo hilo hilo ikiwa mkononi.
4. UNYANYAPAA WA FIKRA VYUO VIKUU
Mheshimiwa Spika, pamoja
na nia njema ya katiba ya nchi yetu kuheshimu haki ya uhuru wa mawazo
kama ilivyowekwa bayana katika Ibara ya 18(a) na Ibara ya 20(1) kwa
kutoa uhuru wa mtu kushirikiana na wengine, kumekuwepo na propaganda
mbalimbali hasa kwenye taasisi za elimu ya juu, zenye kuminya nafasi na
uhuru wa vyama vya upinzani kuendesha shughuli zake kwa usawa, uwazi na
kwa haki katika ngazi ya elimu ya juu kama ambavyo chama tawala
kimejiwekea na kujitengenezea mazingira hayo.
Mheshimiwa Spika, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema hivi: "Lakini
kutoa uongozi maana yake siyo kuwanyang'anya watu wenyewe mamlaka yao.
Watu lazima wafanye uamuzi wao wenyewe kuhusu maisha yao ya baadae kwa
kufuata njia za demokrasia. Uongozi hauwezi kuchukua nafasi ya
demokrasi; uongozi lazima uwe sehemu ya demokrasi"
Mheshimiwa Spika, tafakuri ya nukuu hii imekuja wakati ambao
ushiriki wa wanafunzi wa elimu ya juu katika siasa unaonekana kulemea
upande moja tu wa kukipendelea na kukipa uwezo chama tawala katika
shughuli zake kwenye taasisi hizo. CCM wamefikiri na kuamua kuanzisha
mkoa maalumu kwa sasa wakitambua kuwa vyuo (hasa vyuo vikuu)
haviruhusiwi kuendesha shughuli za siasa vyuoni, kama ilivyo majeshi,
makanisa au misikiti na ili kuthibitisha hilo wameelekeza pia shughuli
za mkoa maalumu ulioanzishwa zifanyike nje ya chuo. Lakini tujiulize na
kutafakari zaidi kuhusu mshindo (impact) wa shughuli za mkoa maalumu wa kisiasa ndani ya himaya za vyuo vikuu na elimu ya juu nchini.
Mheshimiwa Spika, ni ngumu kuamini kuwa shughuli za siasa vyuoni,
ambazo Tanzania Commission of University Act imeweka bayana kuwa ni
kosa, zitaweza kudhibitiwa ikiwa vyama vingine vinajiwekea uhalali na
mazingira ya kuingiza wanavyuo kwenye siasa, jambo ambalo udhibiti wake
ni mgumu kwa mamlaka husika hasa vyuoni kwa kuwa wanavyuo hufanya vikao
vya siasa kwa siri, na kwa nyakati ambazo uongozi wa vyuo hauna taarifa.
Mheshimiwa Spika, kwa uangalifu mkubwa, ningependa kutoa angalizo
kuwa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haitokubali unyanyapaa wa fikra
wa aina yoyote utakaoendana na kujenga matabaka kutokana na utofauti wa
mitazamo baina ya jamii ya wasomi kwa kuwa, kutoka taasisi mbalimbali za
elimu ya juu , chimbuko la viongozi mahiri wa nchi hii pamoja na nchi
nyingine mbalimbali duniani limechipukia. Kambi Rasmi ya Upinzani,
itaendelea na juhudi zake za kuhakikisha kuwa taifa kwa kupitia
wanafunzi wa elimu ya juu, wanapata fursa mbalimbali za kuikomboa jamii
ya kitanzania ambayo inadumazwa kwa unyanyapaa wa fikra.
Mheshimiwa Spika, njia pekee ya kufuta unyanyapaa wa fikra kwa
vijana waliopo kwenye elimu ya juu ni kwa Serikali kurejesha rasmi na
kuruhusu uwepo wa siasa katika elimu ya juu na vyuo vikuu vyote nchini
kama shughuli ambazo ni nje ya masomo ili kusaidia kujenga uwanja wa
demokrasia katika serikali za vyuo na vile vile itasaidia katika kuweka
mazingira ambapo wasomi wetu wanaanza kujifunza mbinu na utendaji wa
kisiasa katika mazingira ya elimu ili waweze kujifunza kuishi pamoja,
kupingana kwa hoja na kujua jinsi ya kuvumiliana katika mazingira ya
tofauti mbalimbali za kiitikadi, imani, na mtazamo kama ilivyoainishwa
katika Ilani ya Uchaguzi ya CHADEMA ya mwaka 2010. Hapa nikisisitiza
maneno ya baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere juu ya kuboresha maisha ya
Watanzania:
"Tukiwasaidia watu wa Tanzania kuendelea, ndiyo tunaiendeleza
Tanzania. Maana Tanzania Ni ya Watanzania Na Watanzania Ni wote, Hakuna
mtu mwenye haki ya kusema "Mimi ndiyo watu". Wala hakuna Mtanzania
mwenye haki ya kusema " Najua linalowafaa watanzania na wengine lazima
wafuate".
ITAENDELEA....
No comments:
Post a Comment