Picha zote na maktaba
WATU wanaodhaniwa
kuwa ni vibaka kutoka katika machimbo ya dhahabu ya Nyangarata na Mwime
wilayani Kahama mkoani Shinyanga,ambayo yamekwisha uzalishaji wake,wamemuua
askari wa Usalama barabarani;Salum Mtepa mwenye cheo cha Staff Sajenti,kwa
kumpiga na kitu kizito kifuani.
Tukio hilo limetokea
nyumbani kwake eneo la Majengo mjini Kahama usiku wa kuamkia leo baada ya watu
hao wanaokadiriwa kuwa wanne kufika nyumbani kwake na kuvunja kibanda cha
biashara kwa lengo la kuiba ndipo askari huyo alipotoka nje kwenda kupambana
nao.
Kwa mujibu wa taarifa
ya Mkuu wa Polisi wilaya ya Kahama George Simba,askari huyo alipigwa na kifaa
hicho kifuani wakati akijaribu kupambana na vibaka hao,hali iliyopelekea kuvuja
damu nyingi ndani ya kifua na kusababisha kifo chake.
Simba amesema hali ya
vibaka katika mji wa Kahama ni mbaya kwani wameongezeka kutokana na machimbo ya
Nyangarata kujaa maji na Mwime kuisha uzalishaji wake,hali iliyofanya vijana
wengi kutoka kwenye maeneo hayo bila kuwa na fedha.
Amesema hivi sasa
wimbi la vibaka hao limekuwa tishio huku akiahidi kupambana nao ikiwa ni pamoja
na kuwasaka kwa nguvu zote vibaka waliohusika na kifo cha askari huyo wa
usalama barabarani,ingawa hadi jana hakuna mtu yeyote aliyekuwa amekamatwa juu
ya kuhusika na tukio hilo.
source shinyangayetu blog
No comments:
Post a Comment