Mtwara. Wakati
mtu mwingine akiripotiwa kufa, hali bado ni tete katika Mji wa Mtwara
kutokana na mabomu ya machozi na risasi za moto kuendelea kurindima
kwenye mitaa kadhaa wakati polisi wakipambana na makundi ya vijana
wanaopinga mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kwenda Dar es Salaam.
Kaimu
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Mohamedi Kodi
alithibitisha kupokea mwili wa mjamzito ukiwa na tundu tumboni,
linaloaminika kuwa linatokana na risasi.
“Ni kweli
kwa leo tumepokea maiti moja ya mwanamke ambaye ni mjamzito wa miezi
saba akiwa amepigwa risasi tumboni,” alisema Dk Kodi. Inadaiwa kwamba
mjamzito huyo ambaye jina lake halikufahamika, ameuawa akiwa nyumbani
kwake. Kifo hicho ni cha pili baada ya Karim Shaibu (22), mkazi wa
Chikongola kuuawa juzi.
Aidha,
kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa kuwa mtu mwingine ambaye jinsia
yake haikujulikana aliuawa kwa bomu la machozi na mwili wake kutawanyika
barabarani.
Kuhusu
majeruhi, Dk Kodi alisema wamefikia watu 18... “Majeruhi wa mwisho
tuliyempokea ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Chuno. Alikuwa
amevunjwa miguu yote kwa risasi.”
Waomba hifadhi hospitalini
Umati wa
watu wengi wao wakiwa kinamama na watoto umemiminika kwenye Hospitali ya
Ligula kukimbia msako wa nyumba kwa nyumba unaofanywa na polisi na
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Wakizungumza
na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, wakazi hao wamelalamikia
kitendo cha polisi kuingia katika makazi yao, kuwapiga na kuwapora mali
zao.
“Magomeni
A hatuna amani, askari wanaingia nyumbani kwetu, wanatupiga na
kutunyang’anya simu, yaani huku Magomeni hatuna amani kabisa,
tumepotezana na watoto na hatujui hata waume zetu wako wapi,” alisema
Paulina Idd.
Hata
hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa alisema hali
ni shwari na kuwataka wananchi kuendelea na shughuli zao kama kawaida.
Hadi sasa
huduma za kijamii zimesimama, hakuna maduka yaliyofunguliwa, hakuna
usafiri wa daladala wala pikipiki, mji upo kimya huku sauti za milio ya
mabomu na bunduki ikitawala, wanajeshi waliovalia sare wametapakaa
sehemu mbalimbali za mji wakiwa katika magari na pikipiki.
Nchimbi atua Mtwara, jeshi lamwaga vifaa
Dk
Nchimbi aliwasili jana jioni kwa helikopta na kukutana na viongozi wa
Mkoa wa Mtwara walioongozwa na Mkuu wa Mkoa, Kanali Joseph Simbakalia
kujadili suala hilo.
Pia ndege kubwa ya jeshi nayo ilitua huko na wanajeshi walikuwa wakipakua vitu mbalimbali vilivyoaminika kuwa vifaa.
Jeshi hilo limeombwa kuongeza kukabiliana na vurugu hizo ambazo zimesambaa sehemu mbalimbali za Mtwara.
No comments:
Post a Comment