MKURUGENZI
wa Mashitaka (DPP) amewasilisha maombi ya kupinga uamuzi wa Mahakama
Kuu Kanda ya Dar es Salaam, uliomfutia mashitaka ya ugaidi Mkurugenzi wa
Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare na mshitakiwa mwenzake
Ludovick Joseph.
Katika ombi hilo lililowasilishwa juzi katika Mahakama ya Rufaa, DPP
anaomba mahakama ifanye marejeo ya uamuzi huo na kuamuru kuwa haukuwa
sahihi kisheria. Mei 8 mwaka huu, Jaji Lawrence Kaduri alifuta mashitaka
matatu ya ugaidi dhidi ya washitakiwa hao kwa kuwa hati ya mashitaka
iliyofunguliwa na DPP, haielezi uhalisia wa kosa hilo na washitakiwa
wanahusika vipi kufanya ugaidi.
Katika ombi hilo, Mkurugenzi Mashitaka anaiomba mahakama hiyo iite na
kuangalia rekodi za Mahakama Kuu kwa nia ya kujiridhisha usahihi,
uhalali wa uamuzi huo pamoja na amri zilizotolewa.
Aidha anaomba mahakama kufuta uamuzi kuhusu uhalali wa mashitaka
wanayodai yalikuwa ya awali, ione kuwa walalamikiwa walikuwa hawajaitwa
kujibu mashitaka yao, pia haikuwa sahihi kwa mahakama hiyo kuamua kuhusu
uhalali huo.
Anaomba mahakama ione kwenye sababu zilizoombwa na walalamikiwa katika
ombi lao, hakuna ombi la kufuta mashitaka dhidi yao, pia hakuna taarifa
zilizowasilishwa na walalamikiwa ambazo Mahakama Kuu ingeamua uhalali wa
mashitaka au kuwepo kwa mapungufu.
DPP anaomba mahakama iamuru kuwa uamuzi wa Mahakama Kuu, kufuta baadhi
ya mashitaka kwenye hati ya mashitaka ya muda haukuwa sahihi kisheria.
Machi 22 mwaka huu, Lwakatare kupitia kwa mawakili wake aliwasilisha
ombi la kutaka mahakama hiyo ifanye marejeo ya mwenendo wa kesi ya
ugaidi, inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya
DPP kufuta mashitaka dhidi yao, kisha kuwakamata na kuwasomea upya.
Washitakiwa hao walifutiwa mashitaka ya kupanga njama za kufanya kitendo
cha ugaidi cha kumteka Mhariri wa gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky
kupanga na kushiriki mkutano wenye lengo la kutenda kitendo cha ugaidi
ambacho ni kumteka Msacky.
Lwakatare alifutiwa mashitaka ya kuruhusu mkutano kati yake na Joseph,
kufanyika nyumbani kwake katika eneo la King’ongo, Kimara Stop Over, kwa
lengo la kuhamasisha vitendo vya ugaidi.
Kutokana na uamuzi huo, sasa washitakiwa hao wanadaiwa Desemba 28 mwaka
jana katika eneo la King’ongo, Kinondoni, Dar es Salaam walipanga njama
ya kutenda kosa la jinai la kutumia sumu kumdhuru Msacky. Shitaka hilo
lina dhamana.
CHANZO : HABARI LEO
No comments:
Post a Comment