skip to main |
skip to sidebar
Mwandishi wa habari apigwa risasi, ajeruhiwa vibaya Kismayu
Watu wenye silaha walimpiga risasi na kumjeruhi vibaya mwandishi mmoja
wa habari mjini Kismayu siku ya Jumatano (tarehe 29 Mei), yakiwa ni
mashambulizi ya karibuni kabisa katika msururu wa mashambulizi dhidi ya
vyombo vya habari nchini Somalia.
Abdikadir
Abdirasak Sofe, mpasha habari wa kituo cha Royal TV chenye makao yake
makuu jijini London, alipigwa risasi wakati akielekea nyumbani kwake
baada ya kazi jioni ya Jumatano. "Watu wawili, mmoja wao akiwa na
bunduki aina ya AK-47, walifyatua risasi," shahidi Ali Mohamed
aliliambia shirika la habari la AFP.
Mpasha habari huyo, anayefahamika pia kwa jina la utani la "Jijile",
alikimbizwa hospitalini akiwa na majeraha kadhaa ya risasi kwenye sehemu
ya juu ya mwili wake.
Watu wawili walikamatwa baadaye kwa jaribio hilo la mauaji, lakini
lengo lao halikujulikana mara moja, alisema afisa wa jeshi la Somalia.
Mohamed Saleban.
Kwa uchachewaandishi wa habari wanne wameuawa nchini Somalia mwaka huu.
"Tunalaani vikali mashambulizi haya dhidi ya mwenzetu," alisema Mohamed Ibrahim wa Jumuiya ya Waandishi wa Habari ya Somalia.
Mashambulizi hayo dhidi ya Sofe yanakuja huku Mkutano wa Kikanda juu
ya Amani na Usalama kwa Vyombo vya Habari vya Somalia ulimalizika siku
ya Alhamisi mjini Addis Ababa.
"Ni muhimu sana kukumbuka wakati wote masaibu ya waandishi wa habari
nchini Somalia wanaoteseka kwenye mikono ya al-Shabaab na makundi
mengine ya waasi," alisema Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Waandishi
wa Habari, Jim Boumelha, katika taarifa kwa vyombo vya habari. "Jamii ya
waandishi wa habari imekuwa ikilengwa mara kwa mara na waandishi wengi
wamepoteza maisha yao wakiwa kwenye juhudi ya kuwapa taarifa raia. Hili
lazima likome."
"Katika wito wa amani, mkutano huu umekuja [wakati mzuri na] pia
unatoa wito wa haki kwa waandishi wa habari na familia zao," alisema.
Mkutano huo, uliowaleta pamoja waandishi wa habari kutoka Somalia
nzima, pia uliwavutia washiriki kutoka majirani wa Somalia zikiwemo
Djibouti, Ethiopia, Kenya, Sudan, Rwanda, Burundi na Uganda.
No comments:
Post a Comment