Na Abdi Moalim, Mogadishu
Serikali ya Somalia wiki iliyopita ilianza kampeni ya awamu tatu ya kuondosha vizuizi haramu vya barabarani vilivyowekwa na wanachama wanamgambo katika barabara zinazounganisha Mogadishu kwenda mji mkuu wa Shabelle ya Chini wa Marka na mji mkuu wa Bakol wa Baidoawa miaka mingi, vizuizi hivi vya barabarani vimekuwa vikifanya usafiri kuwa wa gharama na hatari kwa wafanyabiashara, madereva wa mabasi na wananchi wa kawaida ambao husafiri kama kawaida baina ya Mogadishu na miji mikuu ya mikoa, mara nyingi kuwaacha wameibiwa vitu vyao na mara nyingine kuwafika mabaya zaidi.
Wananchi kwa muda wa miezi miwili iliyopita wameitaka serikali kuondosha vizuizi hivi vya barabarani, lakini hakuna kilichofanywa. Ili kuishinikiza serikali, Kamati ya Jumuiya ya Usafiri ya Shabelle ya Chini, jumuiya ya eneo hilo ambayo inawawakilisha madereva wa biashara, ilipeleka wasiwasi wao kwa serikali na kuandaa mgomo ulioanza tarehe 12 Mei. Serikali ilijibu siku ya pili yake.
"Tumechagua vikosi maalumu vya kuondosha vizuizi ambavyo vimewekwa barabarani," Jenerali Abdirisaq Khalif Elmi, kamanda wa vikosi vya jeshi la Somalia, aliwaambia waandishi wa habari tarehe 13 Mei.
Mwenyekiti wa jumuiya ya usafiri Yusuf Abdi Omar alisema kuwa hatua ya serikali ni hatua nzuri.
"Maafisa wa kijeshi walituambia kuwa watafanya operesheni ya kupambana na vizuizi vya barabarani katika awamu tatu," Omar aliiambia Sabahi. "Katika awamu ya kwanza, vizuizi vya barabarani baina ya Afgoye na Mogadishu vitaondoshwa. Katika awamu ya pili, watashughulikia barabara baina ya Mogadishu na Marka na awamu ya tatu itakuwa baina ya Afgoye na Baidoa."
"Vizuizi vya barabarani vilivyoko baina ya Afgoye na Mogadishu vimeondolewa, isipokuwa kwa vizuizi viwili vya Lafole na Bar Ismail, ambako kodi za kisheria zitakuwa zikikusanywa," alisema.
Bado safari ni ndefu sana
Khadar Mufow mwenye umri wa miaka 34, dereva wa basi la kila siku anaendesha basi dogo la watu 20 kwa umbali wa kilomita 250 baina ya Baidoa na Mogadishu. Alisema kuwa juhudi za serikali zimepokelewa vyema lakini zinahitaji kupanuliwa."Utawala umefanya mambo ya maendeleo hadi sasa katika kupunguza idadi ya vizuizi haramu vya barabarani, lakini bado inapaswa ifanikiwe kikamilifu kwa kuondosha tatizo la vizuizi hivi linaloukumba usafiri," aliiambia Sabahi. "Bado kuna tatizo kubwa linalotukabili barabarani, hasa wakati tunapotaka kusafiri kwenda Baidoa. Tunatumia zaidi ya shilingi milioni moja za Somalia (dola 55) kwa vizuizi haramu vya barabarani baina ya Baidoa na Afgoye wakati wa kila safari ya kwenda na kurudi."
Mohamud Sultan, dereva anayefanyakazi katika barabara inayounganisha Mogadishu na Marka, alisema madereva mara nyingi hujeruhiwa na kuibiwa na wanachama wanamgambo.
"Madereva wawili waliuliwa wiki mbili zilizopita na kikundi cha waendesha pikipiki na abiria walijeruhiwa baada ya kupigwa risasi ghafla na wanamgambo waliovalia sare za kijeshi. Gari za abiria pia huibiwa kama kawaida," aliiambia Sabahi.
Ardo Ali, mfanyabiashara wa kike mwenye umri wa miaka 50 anayesafirisha vyakula baina ya Mogadishu na Marka, alisema kuwa serikali imechukua hatua chanya katika kupambana na wanamgambo ambao huweka vizuizi barabarani.
"Tunakuwa na hofu kubwa kila tunapoondoka Mogadishu kusafiri kuelekea Shabelle ya Chini kwa sababu tunaogopa kupigwa risasi na wanamgambo wanaotaka kusimamisha magari [na kutulazimisha kulipa]," aliiamabia Sabahi. "Majambazi wanataka fedha kutoka kwa magari [wanaopita katika vituo vya ukaguzi] ambazo hatuwezi kuzimudu, na wakati tunapokataa kulipa, wanatuibia na huchukua tulichonacho."
Nur Ahmed anasafiri kutoka nyumbani kwake Afgoye kila siku kuelekea Mogadishu, ambako anafanyakazi kama mlinzi binafsi wa shirika moja lisilo la faida ambalo linatoa chakula kwa watu waliokimbia makazi yao.
Ahmed alisema kuwa vizuizi vya barabarani kumeufanya usafiri kuwa mzigo wa fedha ambao hautabiriki kwa wasafiri kwa sababu wanachukua gharama kubwa ya ziada kwa kupanda na kushuka kwa bei ambazo wanatozwa kwa tiketi. "Tunaiomba serikali kuviondosha vizuizi vya barabarani vilivyobakia na kuzuia viziwekwe upya kwa kusimamia barabara kila wakati [baada ya operesheni kumalizika]," aliiambia Sabahi.
Mwezi Disemba uliopita, vikosi vya usalama vya Somalia vilifanikiwa kuondosha zaidi ya vizuizi haramu 60 vya barabarani Mogadishu kote.
No comments:
Post a Comment