Wakati mtu mwingine akiripotiwa kufa, hali
bado ni tete katika Mji wa Mtwara kutokana na mabomu ya machozi na
risasi za moto kuendelea kurindima kwenye mitaa kadhaa wakati polisi
wakipambana na makundi ya vijana wanaopinga mradi wa ujenzi wa bomba la
gesi kwenda Dar es Salaam.
Kaimu
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Mohamedi Kodi
alithibitisha kupokea mwili wa mjamzito ukiwa na tundu tumboni,
linaloaminika kuwa linatokana na risasi.
“Ni
kweli kwa leo tumepokea maiti moja ya mwanamke ambaye ni mjamzito wa
miezi saba akiwa amepigwa risasi tumboni,” alisema Dk Kodi. Inadaiwa
kwamba mjamzito huyo ambaye jina lake halikufahamika, ameuawa akiwa
nyumbani kwake. Kifo hicho ni cha pili baada ya Karim Shaibu (22), mkazi
wa Chikongola kuuawa juzi.
Aidha,
kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa kuwa mtu mwingine ambaye jinsia
yake haikujulikana aliuawa kwa bomu la machozi na mwili wake kutawanyika
barabarani.
Kuhusu
majeruhi, Dk Kodi alisema wamefikia watu 18... “Majeruhi wa mwisho
tuliyempokea ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Chuno. Alikuwa
amevunjwa miguu yote kwa risasi.”
Waomba hifadhi hospitalini
Umati wa
watu wengi wao wakiwa kinamama na watoto umemiminika kwenye Hospitali ya
Ligula kukimbia msako wa nyumba kwa nyumba unaofanywa na polisi na
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Wakizungumza
na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, wakazi hao wamelalamikia
kitendo cha polisi kuingia katika makazi yao, kuwapiga na kuwapora mali
zao.
“Magomeni
A hatuna amani, askari wanaingia nyumbani kwetu, wanatupiga na
kutunyang’anya simu, yaani huku Magomeni hatuna amani kabisa,
tumepotezana na watoto na hatujui hata waume zetu wako wapi,” alisema
Paulina Idd.
Hata
hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa alisema hali
ni shwari na kuwataka wananchi kuendelea na shughuli zao kama kawaida.
Hadi sasa
huduma za kijamii zimesimama, hakuna maduka yaliyofunguliwa, hakuna
usafiri wa daladala wala pikipiki, mji upo kimya huku sauti za milio ya
mabomu na bunduki ikitawala, wanajeshi waliovalia sare wametapakaa
sehemu mbalimbali za mji wakiwa katika magari na pikipiki.
No comments:
Post a Comment