Hatma
ya kufikishwa mahakamani kwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi
‘’Sugu”( Chadema), iko mikononi mwa Mwendesha Mashtaka wa
Serikali. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema
jana kuwa jeshi lake limekamilisha upelelezi kuhusu tuhuma zinazomuhusu
Sugu na kwamba wanasubiri maelekezo ya kumfikisha mahakamani. Mbilinyi
alikamatwa juzi mchana akiwa mjini Dodoma anakohudhuria vikao vya bunge
na habari zilisema anatuhumiwa kutoa maneno ya kashfa na uchochezi dhidi
ya Waziri, Mkuu Mizengo Pinda. Inadaiwa
kuwa mbunge huyo amefanya hivyo kupitia mtandao wa kijamii. Kamanda
huyo alisema jana Mbilinyi aliripoti katika Kituo cha Polisi Kati kama
alivyotakiwa na jeshi hilo na kuongezewa dhamana hadi leo anapotakiwa
kurudi tena kusikiliza hatma yake. Misime alisema “jeshi hilo liliamua
kumkamata mbunge huyo baada ya kugundulika kuandika maneno ya kumtukana
Waziri Mkuu kuhusu utendaji wake na kumdhalilisha katika siku ambayo
hakuitaja.” Taarifa zisizo rasmi zinaonyesha kuwa, mbunge huyo
anatuhumiwa kuandika maneno hayo ya kashfa kufuatia kauli ya Pinda hivi
karibuni kuhusu kuwataka polisi kuwapiga raia wasiotii sheria.
Alikuwa akijibu swali la papo kwa papo ndani ya Bunge wiki iliyopita
ambapo alisema Serikali imechoshwa na vitendo vya watu kutotii sheria na
kutoa mfano wa matukio ya Mtwara na Arusha. Huko Mtwara polisi
walitumia nguvu zaidi kuwadhibiti wananchi waliokuwa wakikataa gesi
isisafirishwe kwa njia ya bomba kwenda Dar es Salaam, wakati huko
Arusha, walifanya hivyo katika kuwatawanya wafuasi wa Chadema, waliokuwa
wakishiriki katika tukio la kuaga maiti. Baadhi ya watu wakiwamo
wanaharakati walisema kauli hiyo inaweza kuleta chuki kati ya polisi na
wananchi.
No comments:
Post a Comment