Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Friday, June 28, 2013

HUZUNI::MKURUGENZI WA KILOLO AKUTWA AMEKUFA

 
Aliyekuwa Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo Marehemu Mohamed Ngwalima, alipotembelea mto Ruaha mkuu eneo la Nyanzwa ambalo maji ya mto huo yamekauka.
-------------------------------------------
KATIKA hali isiyo ya kawaida, mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa, Mohamed Ngwalima amekutwa amekufa akiwa katika Kochi la nyumbani kwake, baada ya kutoka safarini, kifo ambacho kimeibua maswali mbalimbali kwa wananchi juu ya kifo hicho cha ghafla.

Akizungumzia kifo hicho cha ghafla mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo Joseph Muhumba alisema alishangazwa na taarifa ya kifo hicho kwani muda mfupi walikuwa wameachana na marehemu, kwani walikuwa wote jijini Dar es salaam ambako walikuwa katika kikao cha wadau wa zao la Chai.

“Tulikuwa wote Dar es salaam ambako tulikwenda kufuatilia masuala ya kiwanda chetu cha Chai, Mkurugenzi wangu  Mohamed Ngwalima alikuwa ni mzima, tulikuwa wote kwenye kikao na watu wa Chai, nimeachana nae mie nikielekea Dodoma,  lakini jana alikuwa ameanza safari ya kuja Kilolo, na asubuhi tumewasiliana naye akasema yupo Kibaha, lakini nikashangaa ninapewa taarifa kuwa amekufa ghafla, kwani sikupata maelezo yoyote ya awali kuwa ameumwa nini, kwa kweli tukio hili limetushitua sana sisi kama madiwani, watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo na wananchi wote kwa sababu limekuwa nila ghafla sana,” Alisema Muhumba.

Alisema taarifa aliyopokea ilisema marehemu alifariki akiwa amekaa katika Kiti (Kochi) la sebule ya nyumbani kwake, muda mfupi baada ya kufika akitokea  safarini Dar es salaamu, ambako alikwenda kufuatilia masuala ya mpango wa  wa kiwanda cha chai.

Muhumba alisema siku moja wakiwa katika ziara ya kikazi jijini Mwanza marehemu alimueleza kuwa anatatizo la ugonjwa wa Kisukari, lakini tangu kuanza kazi katika wilaya hiyo hajawahi kuugua, kwani alikuwa akijituma sana katika shughuli za maendeleo.

Aidha alisema Marehemu hakuwahi kutoa taarifa za kuumwa, na kuwa kifo chake ni pigo kwa Wilaya ya Kilolo na Taifa  zima na watamkumbuka kwa utendaji wake wa kazi kupitia maamuzi mbalimbali ya vikao, huku akiwa mfuatiliaji wa masuala ya kiuchumi.

Naye Benson Kilangi ofisa kilimo, mifugo na ushirika Wilaya ya Kilolo ambaye ni mratibu wa shughuli za mazishi alisema marehemu aliingia katika Wilaya ya Kilolo majira ya saa kumi na moja jioni akitokea safarini Dar es salaam ambapo hakuwa na dalili zozote za ugonjwa wala kuumwa.

Kilangi alisema muda mfupi baada ya kuachana na mkurugenzi huyo alipigiwa simu na mke wa marehemu akimueleza kuwa Ngwalima amezidiwa na baada ya kufika nyumbani hapo kwa marehemu walikuta tayari mkurugenzi huyo akiwa ameshafariki.

“Mkurugenzi aliingia hapa Kilolo majira ya saa kumi na moja jioni akitokea Dar es salaam, na alipofika alimwambia dereva ampeleke nyumbani na huko kwa mujibu wa maelezo ya mke wake marehemu alisema alifika na kukaa kwenye Kochi ambapo ndipo mahali alipofia, lakini mimi ni mtu wake wa jirani sana nilipoonana naye alikuwa na hali njema kabisa, kwani kama angekuwa alikuwa anaumwa ningemtambua na tungechukua jukumu la kumpeleka Hospitali kupata matibabu,” Alisema Kilangi.

Aidha alisema marehemu hakuweza kupatiwa matibabu yoyote, kwani hata walipomuita daktari walipata taarifa ya kuwa tayari mkurugenzi huyo alikuwa amekufa.

Alisema muda wa taarifa na kitendo cha kufika nyumbani hapo kwa marehemu haikumchukua muda mrefu kwani nyumba yake ipo jirani sana na jengo la Halmashauri ya Wilaya hiyo, na kuwa hatua ya kifo hicho cha ghafla ni pigo kubwa kwao na wananchi wa Wilaya hiyo.

Kilangi alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali yam Koa wa Iringa, na wanafanya mpango wa kusafirisha mwili wa marehemu kwenda Ikwiriri Rufiji kwa ajili ya mazishi.

Marehemu Mohamed Ngalima alizaliwa mwaka 57 katika kijiji cha Ikwiriri Rufiji, na alikuwa na elimu ya shahada ya Uchumi ambapo alifanya kazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara kama mchumi wa Wilaya hiyo, na mwaka 2007 aliteuliwa kuwa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu mkoani Arusha.

Na mwaka 2012  alihamishiwa Wilaya ya Mtwara ambapo mwaka 2013 alipelekwa katika Halmashauri ya Wilaya ya kilolo mkoani Iringa hadi unapomfika  umauti siku ya tarehe 25 mwezi sita 2013 saa moja kamili jioni, katika nyumba yake aliyokuwa akiishi na familia yake.

Na mwili wa marehemu unataraji kuzikwa kesho tarehe 27 mwezi june kwani taratimu za msafari zimeanza katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa, ambako mwili wa marehemu upo (Mortuary) huku watumishi mbalimbali wa serikali na sekta binafsi pamoja na wananchi mkoani Iringa wakiwa eneo hilo kwa ajili ya kutoa heshima zao za mwisho na kuuaga mwili wa marehemu ili kuanza safari ya kuelekea Rufiji katika makao ya milele.

BWANA ALITOA, BWANA AMETWAA, JINA LA BWANA HIHIMIDIWE.
AMINA.

No comments:

Post a Comment