Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Saturday, June 29, 2013

MATUKIO YALIYOJILI WAKATI SUGU AKIWA MAHAKAMANI JANA, DODOMA


MWENDESHA Mashitaka wa Serikali (DPP)  aliambulia patupu baada ya Hakimu wa Mahamaka ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Dodoma, kumwachia huru Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, (CHADEMA) ambaye alimfikisha kizimbani kujibu tuhuma za kumkashifu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kupitia mitandao ya jamii. Kulia kwake ni Mhe. Tundu Lissu wakati wakitoka Mahakamani
Photo: Mbunge Sugu aachiwa huru

Mahakama  ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dodoma, imemfutia mashtaka na kumwachia huru, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, (Chadema), maarufu Sugu baada ya kuthibitisha kuwa hati ya mashtaka ina mapungufu ya kisheria.

Hatua hiyo, iliyochukuliwa na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Elinaza Luvanda, baada ya mabishano ya kisheria kati ya Wakili wa mshtakiwa, Tundu Lissu na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Harieth Lopa.

Awali akisoma mashtaka, Lopa alidai kuwa Mbilinyi alitenda kosa hilo Juni 24, mwaka huu, Dodoma Mjini ambapo alidaiwa kuweka ujumbe mfupi wa maneno unaodaiwa kuwa wa matusi katika Mtandao wa Kijamii (Facebook), hali ambayo inaweza kuleta uvunjifu wa amani  kwa  Waziri Mkuu.

Lopa alidai kuwa upelelezi wa shtaka hilo bado unaendelea. Alipohojiwa na Hakimu Luvanda, Mbilinyi alikana kutenda kosa hilo.

Baada ya hatua hiyo,  Lissu alisimama na kuiomba mahakama hiyo kutupilia mbali shtaka hilo kwa sababu hati ya mashtaka iliyowasilishwa na serikali ina makosa. Alisema hati hiyo haijataja lugha hiyo ya matusi na badala yake imesema aliweka ujumbe katika Facebook ambao ungesababisha uvunjifu wa amani kwa Waziri Mkuu.

“Lugha gani, charge sheet (hati ya mashtaka),  ipo kimya, mshtakiwa atajiandaa kujitetea kwa lipi, ataandaa utetezi wa namna gani kwa ujumbe upi ambao ameuweka katika Facebook, si kila ujumbe unaokuwa katika Facebook,” alisema Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema).

Alisema kwa sababu hati hiyo ina makosa na dawa ya makosa kama hayo ni kuitupilia mbali ili upande wa mashtaka uende ukalete upya hati mashtaka inayoeleza kosa alilotenda mshtakiwa.

Aliiomba mahakama kuifutilia mbali hati hiyo na mshtakiwa aachiwe huru na kama serikali inataka ikajipange upya kuleta hati nyingine ya mashtaka.

Akijibu hoja hizo, Mwendesha Mashtaka, aliiomba mahakama hiyo kuendelea na kesi hiyo kwa sababu bado kesi haijaanza kusikilizwa. Lopa alisema wakati wa utetezi ukifika, mshtakiwa atapata nafasi nzuri ya kuandaa utetezi wake.

Akijibu hoja hiyo Lissu aliendelea kusisitiza kuwa hati hiyo haikidhi masharti ya kisheria ambayo yamo katika kifungu 132 cha mwenendo wa makosa ya jinai.

Lissu alisema kifungu hicho kinataka hati ya mashtaka kujitosheleza kwa taarifa ya kosa, kinyume na hati hiyo. Alisema hati hiyo si halali kwa mujibu wa kifungu hicho na iwapo mahakama itaitumia itakuwa ni makosa.

“Naiomba mahakama yako ifutilie mbali kesi hii na kama watataka wakajipange upya wailete tena kesho ama siku nyingine watakayoitaka,” alisema Lissu.

Akijibu hoja hizo, Hakimu Mfawidhi Luvanda, alikubaliana na hoja za Lissu kwa kuwa hati hiyo ina mapungufu. “Hati hii ina mapungufu na dawa ni kuifukuza mbali kwa kumwachia huru…mnaweza kumshtaki tena pale utakaporekebisha mapungufu haya,” alisema.

Akizungumza nje ya mahakama hiyo, Lissu alisema iwapo wanataka kumshtaki Mbilinyi kwamba alimtukana Pinda, wanatakiwa wamwambie aende kulalamika polisi.

“Aandike  maelezo (Pinda) na aje ayatolee maelezo mahakamani wasidhani watashtaki kuwa Waziri Mkuu ametukanwa kumbe yeye mwenyewe hajalalamika, hajaenda polisi kutoa maelezo ili kuisaidia,” alisema.

Kwa upande wake Mbilinyi, alimtaka Pinda kusikiliza jinsi kauli yake ilivyo na madhara kwa watu na mashirika haki za binadamu pamoja na mashirika ya nje za nchi. “Namtaka afute kauli yake kwamba wananchi wapigwe,” alisema na kuongeza kuwa hilo ndilo jambo la msingi la kufanyika.

Mbilinyi alisindikizwa na wabunge wawili wa Chadema ambao ni  Grace Kiwelu (Viti Maalum) na Ezekia Wenje (Nyamagana) pamoja na viongozi wengine wa chama hicho mkoani Dodoma.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment