MFUMO mpya wa Bunge kuanza na bajeti za kisekta na kumalizia na Bajeti
ya Serikali pamoja na uundwaji wa Kamati ya Bajeti, umeonesha makali
yake kiasi na kuilazimisha Serikali, kushusha kodi ya petroli na kufuta
ushuru wa kutuma na kupokea fedha kwa njia ya simu.
Kabla ya Serikali kufikia uamuzi huo jana saa sita usiku, Kamati ya
Bunge na wabunge walivutana na Serikali mara kadha wa kadha juu ya kodi
mbalimbali, na kulazimika Kamati hiyo na Serikali kukaa si chini ya mara
mbili, kujadili.
Katika vikao vyao, vikao viwili vya juzi na jana, Kamati ya Bajeti
inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), na
Waziri wa Fedha, William Mgimwa, naibu wake wawili na wataalamu wake wa
wizarani, walikaa kujadili tofauti zao mpaka saa sita usiku.
Mvutano wa Kwanza Mvutano wa kwanza ulianza mwanzoni mwa wiki hii, baada
ya Waziri Mgimwa kuanza kujibu hoja za wabunge kuhusu Bajeti ya
Serikali, ambayo ilipongezwa na kupingwa na Kamati ya Bajeti.
Hoja za wabunge na Kamati ya Bajeti, zilihusu punguzo la kodi katika
mishahara, petroli, huduma za simu na magari yenye umri wa kuanzia miaka
10 na kuendelea na kodi katika huduma za utalii.
Hata hivyo, Mgimwa alipokuwa akijibu hoja za wabunge kabla ya kuwaomba
wapitishe Bajeti ya Serikali, aliwataka wapitishe kwanza bajeti hiyo na
hizo hoja zao zijibiwe katika Muswada wa Sheria ya Fedha, hatua ambayo
wabunge waliiridhia na Bajeti ya Sh trilioni 18.2, ikapita.
Hata hivyo baada ya Bajeti kupita, Mgimwa aliwasilisha Muswada huo,
ambao uliacha baadhi ya kodi ikiwemo ya magari mabovu kuzidi miaka 10,
ya petroli na dizeli na ya simu.
Baada ya Mgimwa kumaliza kusoma Muswada huo, Chenge huku akiungwa mkono
na wabunge wengi, alipokuwa akisoma maoni ya Kamati ya Bajeti,
alisisitiza baadhi ya kodi zifutwe au kupunguzwa na kuielekeza Serikali
kutafuta vyanzo vipya katika ripoti ya Kamati ya Spika ya vyanzo mbadala
vya mapato ya Serikali.
Vikao vya saa sita usiku Kutokana na mvutano huo, Waziri wa Fedha na
Kamati ya Bajeti walikutana Jumatano wiki hii mpaka saa sita usiku na
hata walipotoka, walikuwa hawajaafikiana, kiasi cha Mgimwa kuja na
marekebisho kidogo, ikiwemo kuondoa kodi ya utalii, lakini Chenge akaja
na msimamo katika kodi ya petroli na utumaji na upokeaji fedha kwa njia
ya simu.
Baada ya maoni ya Chenge, wabunge saba walileta majedwali ya mabadiliko,
na kusababisha Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuitaka Kamati ya Bajeti,
Waziri wa Fedha na hao wabunge kurudi kutafuta suluhu juzi.
Katika kikao hicho cha suluhu cha juzi Alhamisi, Kamati hiyo na Waziri,
waliendelea kuvutana mpaka saa sita usiku tena ndipo wakaafikiana,
ambapo jana walikuja na kauli moja.
Suluhu
Kabla ya Mgimwa kutangaza mwafaka, Chenge alipewa nafasi na kumsifu
Waziri Mgimwa kwa kuwa msikivu na mtu asiyependa makuu na kusema,
wamefikia makubaliano ambayo ni habari njema kwa Watanzania.
Baada ya Chenge kutangaza habari hiyo njema, Mgimwa alisimama na kuanza
na kodi ya petroli, ambapo alisema Serikali imeridhia kutoongeza ushuru
wa bidhaa katika petroli wa Sh 61 na hivyo, itaendelea na ushuru uliopo
wa Sh 333.
Alisema pia wameridhia kusitisha kuongeza Sh 2 katika ushuru wa bidhaa
ya dizeli, na hivyo dizeli itaendelea na ushuru wa mwaka huu wa fedha
unaoisha Juni 30, mwaka huu wa Sh 215.
Mafuta ya taa pia, ushuru uliokuwepo ulikuwa Sh 430 na Serikali wakati
wa mvutano ilitaka uongezwe uwe Sh 475, lakini katika muafaka sasa
utateremka mpaka Sh 425, na bado utasaidia kuzuia uchakachuaji wa
mafuta, kwa kuwa utakuwa juu kuliko wa dizeli.
Hata hivyo, katika ushuru wa barabara unaotozwa katika petroli na
dizeli, walikubaliana katika petroli uongezwe kutoka Sh 200, hadi Sh 263
na katika dizeli kutoka Sh 200 hadi Sh 263, ili barabara za vijijini
zijengwe na nyingine zikarabatiwe.
Mgimwa alisema katika huduma za simu za kutuma na kupokea fedha, ushuru
wa asilimia 14.5 uliokuwa uwekwe, sasa umeondolewa na utabaki katika
kupiga simu, kutuma ujumbe mfupi na huduma zingine za simu.
Kodi ya magari yenye umri wa zaidi ya miaka 10, kwa magari ya kawaida
kutoka asilimia 20-25 na katika magari ya kazi asilimia 5, Kamati ya
Bunge pamoja na kuipinga, lakini ilikubaliana na msimamo wa Serikali.
Serikali pia imekubali kuchukua ushauri wa Bunge, wa kutafuta vyanzo
mbadala vya mapato kutoka katika uvuvi wa samaki katika bahari kuu,
uuzaji wa mashudu nje ya nchi na katika mashirika yenye tozo za moja kwa
moja kutoka katika mafuta ya petroli.
Hata hivyo, Serikali ilikataa kuondoa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa
(Tanapa) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, katika kuwajibika kulipa
asilimia 10 ya mapato ghafi yake au ya bajeti yake ya mwaka, katika
Mfuko Mkuu wa Serikali kama mashirika mengine ya umma.
Pinda, Makinda
Baada ya kumalizika kwa mvutano huo, Muswada wa Sheria ya Fedha
ulipitishwa kwa ndio na wabunge wote bila kujali vyama vyao, huku
Makinda akisifu kazi ya Kamati ya Bajeti, kwamba wanastahili kupata Phd
ya heshima, kwani imeibadili Bajeti ya Serikali, huku Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda, akisifu kuwa kazi nzuri imefanyika na kuisha salama.
“Wote mtakumbuka tumeanza Mkutano huu kwa changamoto kubwa ya mabadiliko
ya mzunguko mpya wa kuwasilisha Bajeti ya Serikali na pengine
kulikuwepo hoja ya mashaka kuhusu ufanisi wake. “Napenda kuliarifu Bunge
lako tukufu kwamba tumefanya vizuri sana, wote ni mashahidi kwamba
waheshimiwa wabunge wamejadili kwa kina na kutoa ushauri wao ambao kwa
kiasi kikubwa umezingatiwa na Serikali,” alisema Pinda.
Chanzo: Habari Leo
No comments:
Post a Comment