Majeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa kutumia helikopta
yameyashambulia maeneo ya waasi karibu na upande wa mashariki mwa mji wa
Goma, ikiwa siku ya tatu ya mapigano makali yaliyosabaisha wimbi la
ukimbizi.
Katika barua ilitumwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambayo
Shirila la habari la Reuters limepata nakala yake, Kongo imekituhumu
kikosi maalumu cha Rwanda kwa kuwasaidia waasi wa M23 katika mapigano
hayo. Lakini pia katika taarifa yao walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa
nchini Kongo wamekanusha madai ya Rwanda kwamba walifyatua makombora
dhidi ya nchi hiyo kutoka ardhi ya Kongo Jumatatu.Taarifa ya jeshi hilo la ulinzi wa amani lijulikalo kama MONUSCO, umesema wanajeshi wake hawajahusika na mapigano katika eneo la Goma na kwa hivyo hawawezi kuhusika katika kufyatua makombora kwenye mipaka ya Rwanda.
Malalamiko ya Rwanda
Katika taarifa tofauti iliyotolewa jumatatu kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Rwanda imelituhumu jeshi maalumu la ulinzi wa amani nchini Kongo kuwa linashirikiana na waasi wa Kihutu, wa kundi la FDLR, ambao wanahusishwa na mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994. Jeshi hilo jipya lina mamlaka ya kupigana na kuwanyang'anya silaha waasi katika eneo la mashariki mwa Kongo.
Mpaka sasa walinzi hao wa amani 3,000 kutoka Afrika Kusini, Tanzania na Malawi wanafanya doria lakini bado hawajajiingiza katika mapigano. Umoja wa Mataifa tayari umekwisha onya, kwamba utazuia shambulio lolote lenye kulenga Goma, mji wenye kiasi ya watu milioni moja, ambao mwezi Novemba ulitekwa na waasi kwa kipindi kifupi.
Mwandishi wa Reuters katika eneo la Mutaho, kiasi cha kilometa saba, kaskazini/mashariki mwa Goma amesema aliziona helikopta tatu za jeshi la Kongo zikishambulia eneo la waasi, mji wa Kibati ambao upo umbali ya kilometa 4 zaidi.
Msemaji wa Jeshi Kanali Olivier Hamuli aliliambia shirika hilo mjini Mutaho, kwamba hali hivi sasa imetulia. Akizungumzia operesheni ya asubuhi ya jana amesema walishambulia jana alfajiri lakini walijibu mapigo na kwamba lengo lao ni kuwasafisha waasi wote wa M23.
Awali Jumatatu Waasi na Majeshi ya Kongo walifyatuliana makombora karibu na kaskazini na magharibi mwa viunga vya mji wa Goma. Umoja wa mataifa unasema makombora hayo yalifika umbali wa mita 100 kutoka uwanja wa ndege wa Goma lakini hakuna hasara zozote zilizoripotiwa.
No comments:
Post a Comment