MFALME Mswati (III) wa Swaziland amewataka Watanzania kubadilika kwenda
sambamba na Soko la Pamoja la Afrika Mashariki kwa kubuni bidhaa
mbalimbali zenye ubora.
Alisema watanzania pia wanapaswa kuzipa kipaumbele bidhaa zinazozalishwa
nchini kwa lengo la kushindana katika biashara duniani.
Mswati aliyasema hayo jana wakati akifungua Maonyesho ya 37 ya Kimataifa
ya Biashara katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere, barabara ya Kilwa, Dar
es Salaam .
Alisema endapo wafanyabiashara wataibua bidhaa zenye ubora na
kuziendeleza itasaidia nchi kukua katika uchumi pamoja na kunufaika na
Soko la Pamoja la Afrika Mashariki (EAC).
Tanzania ni miongoni mwa nchi tajiri na endapo kama itazingatia bidhaa
zinazozalishwa na wananchi wake uchumi wa nchi utakuwa kwa kasi na nchi
itahesabika kama ni miongoni mwa nchi tajiri duniani.
“Maonyesho haya yanatoa fursa kwa watanzania kubuni na kujifunza mbinu
mbalimbali za biashara kufanya ushindani wa biashara duniani,”alisema
Mswati.
Pia alisema maonyesho hayo yanatoa fursa ya kuendeleza bidhaa zenye
ubora wa hali ya juu ikiwa ni miongoni mwa agenda kuu ya mdahalo
waliojadili viongozi mbalimbali wa ushirikiano wa biashara.
Alisema anaamini serikali ya Tanzania inatoa kipaumbele kwa bidhaa
zinazozalishwa nchini zinazoingizwa katika soko la ndani kwa sababu
kufanya hivyo kutasaidia kuinua uchumi wa nchi.
Mfalme Mswati alisema anaamini ushirikiano kati ya Tanzania na Swaziland
utadumu ikiwa ni pamoja na kutangaza bidhaa za ndani na kuutangaza
utamaduni wa nchi.
No comments:
Post a Comment