MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini, anayeunda kundi la Wateule, Taikuni Ally 'Moxie' jana amejitolea kuwasafirisha abiria bure kwenye maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Moxie amejikuta akisukumwa kuwasafirisha abiria maeneo mbalimbali ikiwa ni sehemu moja wapo ya kurudisha kwa jamii, kutokana na kile anachokifanya.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Moxie alieleza kuwa ameamua kukodi UDA moja kwa ajili ya kuwasafirisha abiria bure sehemu yoyote Dar es Salaam pale penye shida ya usafiri kwa siku nzima, lengo lake ikiwa ni kurudisha kwa jamii kutokana na kile anachokiamini kuwa bila mashabiki wake yeye asingekuwepo kwenye gemu la muziki.
Akizungumzia kwa nini ameamua kutoa huduma hiyo kwa siku ya Jumapili na asifanye siku ya Jumatatu ambayo watu wengi wanaamini kuwa ndiyo siku ambayo inashida ya usafiri hapa jijini, Moxie alisema kuwa kila siku jijini kuna shida ya usafiri na yeye amepata nafasi ya kutoa huduma hiyo kwa siku ya jana.
"Leo nazunguka jiji zima la Dar es Salaam, pale ambapo kunashida ya usafiri ndipo tunapowapeleka abiria bure ikiwa ni sehemu moja wapo ya kurudisha kwa jamii kutokana na kile wanachonifanyia hususani kwenye muziki wangu" alisema Moxie.
"Mashabiki wangu ndio wanaosababisha mimi niendelee kuwepo kwenye muziki na wao ndio wa kwanza kuingia katika shoo zangu, na hata kununua albamu zangu hivyo kufanya hivi ni jambo ambalo ni sahihi ingawa sitowafikia wote" aliongezea Moxie
Moxie ni msanii wa muziki wa kizazi kipya nchini miondoko ya Hip Hop , aliyekuwa ndani ya kundi la Wateule, ambaye alikuwa akitamba na nyimbo inayojulikana 'watu kibao'.
No comments:
Post a Comment