Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, July 18, 2013

Ujangili Tanzania! Tembo 475 wauwawa majangili 1215 wanaswa


Na Suleiman Msuya
WIZARA ya Maliasili  na Utalii kupitia Idara ya Wanyamapori imesema zaidi ya tembo 475 wameuwawa na majangili kwa kipindi cha mwaka 2012/13 ambapo watuhumiwa 1215 walikamatwa kwa makosa mbalimbali.
Mkurugenzi wa Wanyamapori, Profesa Alexander Songoro pamoja na watuhumiwa hao pia jumla ya bunduki 85 na risasi 215 za aina mbalimbali zilikamwata na kesi 670 zilifunguliwa katika mahakama za hapa nchini, ambapo kesi 272 zimekamilika kwa washitakiwa 247 kulipa faini ya jumla ya  Sh175,002,420 na washitakiwa 71 kupewa adhabu ya vifungo vya jumla ya miaka 99.
Alisema kesi 398 zenye jumla ya washitakiwa 897 bado zinaendelea katika mahakama mbalimbali nchini ambapo wanaamini kuwa zitakamilika hivi karibuni.
"Kimsingi ndugu zangu wanahabari hali ya ujangili ni kubwa sana kwani kwa kipindi cha mwaka jana zaidi ya tembo 475 waliuuwawa hali ambayo inahitaji juhudi zaidi ziongezeke ili kukabiliana na hali hiyo," alisema Profesa Songoro.
Alisema vita dhidi ya ujangili ni ngumu hasa ukizingatia kuwa baadhi ya watanzania wanaamini kuwa jukumu la kulinga wanyamapori ni la Serikali pekee hasa maofisa wanyama pori jambo ambalo ni dhana potofu.
Songoro alisema ni vema Watanzania wakatunza wanyamapori kwa kutambua kuwa asilimia 90 ya utalii hapa nchini unategemea wanyamapori kwa watalii wengi kutmbelea maeneo yenye wanyamapori.
Alisema utalii wa wanyamapori ndio umebeba uchumi wa Taifa kwa kutoa huduma mbalimbali kama vile madawa, vitabu na kujenga maabara na huduma zingine za kijamii.
Kaimu Mkurugenzi wa Msaidizi Kitengo cha Kuzuia Ujangili, John Muya alisema migogoro inayotokea katika maeneo ya hifadhi za wanayamapori inatokana ongezeko la binadamu na  wanyama jambo ambalo linachangia kuwepo kwa mwingiliano wa makazi .
Alisema binadamu wamekuwa wakiingia na kuweka makazi katika maeneo ambayo wanyama wapo jambo ambalo wakati mwingine linachangia vifo vya wananchi bila sababu za msingi.
Pia alisema ufinyu wa watumishi katika mapori yenye kuhifadhi wanyamapori ni moja ya sababu nyingine ya kukosekana kwa udhibiti wa wanyamapori ambao wanaingia katika makazi ya watu.
Muya alisema kuongezeka kwa ujangili wa nchini kunachangiwa na Watanzania wenyewe ambapo kuna wenye fikra potofu juu ya baadhi ya maeneo ya wanyama wanaouwawa ambapo tembo anaongoza.

No comments:

Post a Comment